HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, October 23, 2023

Baba wa Mtanzania: Sina mawasiliano na mwanangu aliyepo Israel tangu mashambulizi ya Hamas


"Mara ya mwisho nimewasiliana na mwanangu ilikuwa ni tarehe 05 Oktoba, isipokuwa mara ya mwisho nilimuona ‘online’ tarehe 07 Oktoba saa nne na dakika tatu ya asubuhi. Kwa kweli sina furaha kabisa,” ameeleza Loitu Mollel ambaye ni baba mzazi wa Joshua, raia wa Tanzania aliyepo nchini Israel.

Hatua ya kufuatilia alipo mwanaye inakuja siku kadhaa baada ya Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kusema kuwa hauna mawasiliano na raia wawili wa nchi hiyo ambao wanaishi eneo la kusini mwa nchi hiyo ambalo lilishuhudia mapambano baina ya wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas pamoja na jeshi la Israeli.

Loitu ameileza BBC kuwa hafahamu Joshua yuko katika hali gani na kwamba anasubiri taarifa kutoka kwenye mamlaka za Tanzania

Alisema, "Sina furaha, familia haina furaha kwasababu hatumpati kwenye simu huyu kijana, mke wangu na ndugu zangu wanataka niongeze jitihada ili kufahamu alipo na yupo katika hali gani...

"…Jitihada ninazoendelea ni kufuatilia kupitia kwa ubalozi wa Tanzania nchini Israel licha ya kuwa na wao wamenieleza kuwa wanaendelea kufuatilia kufahamu alipo kijana wangu,” alisema Loitu ambaye ni baba wa watoto watano.

Kwa mujibu wa Loitu, Joshua alienda Israel mnamo Septemba 18 kwa ajili ya masomo kwa vitendo.

Mpaka jana, Ubalozi wa Tanzania ulisema kuwa bado haujaweza kufanikiwa kuwasiliana na vijana ambao walidai kutokuwa na mawasiliano nao.

Hivi karibuni, ubalozi wa Tanzania nchini Israel uliwarudisha Watanzania tisa waliokuwa nchini humo, hata hivyo bado wengine zaidi ya raia 350 wanaendelea kuishi katika maeneo mbalimbali nchini Israel.

Chanzo: BBC Swahili


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad