Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Tanzania, mashindano ya kutafuta vipaji vipya vya muziki kupitia mtandao wa kijamii Instagram na youtube pekee yamezinduliwa. Mashindano haya, The Rising Star First Online Music Competition yanayoendeshwa na nPOiNT Online TV na kudhaminiwa na Radian Limited yataanza tarehe nane mwezi wa tisa mwaka 2023.
Ili kushiriki, utatakiwa kurekodi video isiyozidi sekunde 30 itakayo kuonyesha ukimba na kisha kuipandisha Instagram na kuishirikisha (tag) kurasa ya nPOiNT Online TV (@npointtz).
“Hakikisha sauti yako inasikika vizuri unaporekodi video yako,” alisema Janet Anthony Meneja Mradi na Mtangazaji wa nPOiNT Online TV, “lengo letu ni kupata sauti mpya, sura mpya, na msanii mkubwa mpya.” Zoezi la kupokea video litaisha tarehe 13 mwezi wa tisa 2023.
Akielezea lengo la shindano, Bi Anthony alisema, nPOiNT inafahamu wingi wa vipaji mtaani na changamoto ya kukosa nafasi za kujitangaza na kuonekana. “Baada ya kugundua changamoto, tumeandaa mashindano haya ambayo yatafanyika kila mwaka ili kuwapa jukwaa la kusikika wale wenye vipaji bila kuingia gharama za usafiri,” alisema.
Mshindi wa The Rising Star ataondoka na kitita cha Tshs 1,000,000 na mkataba wa kurekodi wimbo na video moja katika studio kongwe ya Bongo Recordz chini ya Producer P Funk Majani.
“P Funk ni kati ya wazalishaji muziki wanaoheshimika sana Tanzania. Majina ya wasanii aliofanya nao kazi na vipaji alivyoibua kwenye tasnia hii ni vingi. Fursa hii ni adimu,” alisema Bi Anthony, akibainisha kuwa wadhamini wa mashindano haya Radian wamewekeza takribani Tshs 15,000,000.
Mwakilishi wa Radian Ltd, alisema Radian imejikita katika kugusa maisha ya vijana na Watanzania kwa ujumla hivyo kusimamia slogan yao ya BEYOND TOMORROW, yaani kuleta mabadiliko zaidi ya kesho.
“Kwetu hii ni fursa kubwa kushiriki katika kuleta mabadiliko ya jinsi vipaji vitakavyokuwa vinapatikana. Shindano hili litawagusa vijana wengi kupitia mtandao mahali ambapo zaidi ya Watanzania 30m wapo" Bi Lina Matunda, Meneja Matukio, Radian Ltd.
Mwakilishi wa Bongo Recordz alisema ushiriki wa studio hiyo ni muendelezo wa jitihada zao za muda mrefu katika kukuza sanaa na kuibua vipaji vipya Tanzania.
“Tumefanya kazi kwa muda mrefu lakini hii ni mara ya kwanza mashindano ya namna hii yanafanyika. Hatujawahi kusaka vipaji kwa kutumia mtandao ya kijamii tu. Tunawahimiza wote wenye vipaji kushiriki. Tumia simu yako,” Alfred Rodgers..
The Rising Star itakuwa na majaji watatu, P Funk Majani, Paul Clement na Beda M. “Majaji wetu ni wasanii wenye uzoefu kwenye nyimbo za Bongo Fleva na za kidini. Kila mtu yupo huru kushiriki,” alisema.
Mashindano yatafanyika ndani ya wiki tano, hatua ya kwanza itakuwa ni upokeaji wa video, wiki ya pili ni robo fainali itakayohusisha washiriki 10 bora, wiki ya tatu ni nusu fainali itakayo ibua watu sita. Waimbaji watatu bora wataingia fainali wiki ya nne na mshindi atatangazwa wiki ya tano.
Meneja mradi wa mashindano ya kuimba ya The Rising Star First Online Music Competition, Janeth Anthony wa kampuni ya (nPOiNT Online TV (kushoto) akizungumziamashindano hayo ambapo mshindi atapata sh milioni moja. Kulia ni Meneja Matukio wa kampuni ya Radian, Lina Matunda.
Meneja Matukio wa kampuni ya Radian, Lina Matunda (kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya kusaka vipaji yajulikanayo kwa jina ;a The Rising Star First Online Music Competition yanayoandaliwa na kampuni ya (nPOiNT Online TV). Kulia ni mwakilishi wa kampuni ya Bongo Records Alfred Rogers.
Saturday, September 9, 2023
Vipaji vipya vya muziki kusakwa kimtandao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment