HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 19, 2023

Utafiti wa Mradi wa EFLOWS waonesha maji yanapungua kwenye mito

 

Na: Calvin Gwabara – Mbarali.

Matokeo ya Utafiti wa miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya Mto Mbarali
Mkoani Mbeya yameonesha kuwa Maji yanapungua na hii ni kutokana na ongezeko la
watu na mahitaji ya matumizi ya maji kuongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo
vya maji vya mto huo.
Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa miaka miwili wa Utafiti wa
Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa
Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa
Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) wakati
akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani
humo Mkoani Mbeya.

“Tulichokiona kwenye utafiti ni kwamba wingi wa maji kwenye mto unaendelea
kupungua, wahitaji wa maji wanaongezeka lakini pia mabadiliko ya tabia nchi nayo
yameathiri kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji na mvua kwenye maeneo haya na
hivyo kupelekea maji kupungua mtoni na athari zake hasi zikionekana kwenye mifumo
ikolojia ya mto hasa wakati wa kiangazi. Tumeona uwepo wa matumizi makubwa ya
maji bila vibali kwa kutumia pampu, na uzalishaji mkubwa wa mchanga wakati wa
mvua kutokana na shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo milimani na
kwenye mashamba” alisema Prof. Kashaigili.

Aliongeza” Shughuli za kibinadamu zinazofanyika Mbarali kwa maana ya makazi,
kilimo, ufugaji, ufyatuaji wa matofali kwenye vyanzo vya maji na mtoni, kilimo cha
vinyungu, moto na shughuli zingine za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa
mtawanyiko wa maji kwenye mto, lakini uchukuaji wa maji kwenye mto ndio
umeonekana kuongoza kwa athari hasi”.

Prof. Kashaigili amesema changamoto hiyo ya matumizi makubwa ya maji imepelekea
mto kukauka kabisa maeneo ya chini wakati maeneo ya juu ya mto na katikati ukifika
unakuta maji mengi yanatiririka ambayo hayafiki mwisho yanaishia njiani kutokana na
watu kuyachepusha na kuyachota kwaajili ya shughuli zao mbalimbali hususani kilimo
ambacho hakizingatii matumizi sahihi ya maji hayo.

“Kwa maana hii ni kwamba Mto Mbarali hauchangii chochote kwenye Mto Ruaha Mkuu
hasa wakati wa kiangazi kwenye maeneo ya uhifadhi na hii maana yake ikolojia ya
mto na uendelevu wake imeathirika na hivyo kushindwa kufikia malengo makubwa ya
Kidunia ya maendeleo endelevu na yale ya kitaifa ya kuifadhi na kuilinda baonuai ya
mto” alifafanua Mtafiti huyo Mkuu Prof. Kashaigili.

Mtafiti huyo aliyebobea kwenye tafiti za Masuala ya maji na Mazingira Duniani
amesema pamoja na Utafiti kutoa matokeo hayo kwa wadau hao muhimu pia
wameainisha njia na mikakati ya kufanya ambayo ikifanyika itasaidia kupunguza athari
zilizojitokeza na kusaidia kurejesha afya ya mto na mtiririko wa maji kwenye Mto
Mbarali na mingine nchini kwa kuwa changamoto zinafanana.

Amesema moja kati ya mikakati hiyo ilikuwa kurejesha uoto wa asili kwenye vyanzo
vyote vya maji vilivyoathirika na kingo za mito, ambapo mradi kwa kuanzia umesaidia
kuanzisha vitalu vikubwa viwili vya miti rafiki wa maji kwenye wilaya ya
Wanging’ombe Mkoani Njombe na Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutumia elimu asili na
kufanikiwa kupanda miti zaidi ya elfu 45 kwenye vyanzo na kingo za mito pamoja na
kuanzisha ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuongezea kipato cha jumuiya za watumia
maji wanaosimamia madakio pamoja na kuongezea uhifadhi.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama ambaye alikuwa anaangalia afya ya mto na
usalama wa maji kupitia mradi huo amesema matokeo yameonesha maji
yanayotiririka kwenye mto huo bado ni salama kwa kuwa baada ya kufanya utafiti
wamekuta viumbe ambao hawawezi kuishi kwenye maji ambayo sio salama.

“Viumbe wadogo wanaoishi majini pamoja na samaki wanauwezo mkubwa wa kutoa
ishara ya ubora wa maji katika eneo na ndio maana pamoja na watafiti wengine
huchukua sampuli za maji na kuzipima, lakini mbinu ya kuangalia viumbe ndio
muhimu zaidi kwa kuwa ndio wanakaa kwa muda mrefu kwenye eneo hilo kuliko
kupima maji maana unaweza kwenda kuchota maji ukakuta wakati huo ni bora kwa
muda huo tu, ila viumbe waishio kwenye maji hawapiti wapo muda wote” alifafanua
Mkama.

Mtafiti huyo amezitaka mamlaka zinazosimamia maji kuhakikisha kunakuwepo na
usimamizi mzuri hasa kwenye maeneo wanayochota maji mengi kwenye skimu ya
Umwagiliaji ya Igomelo ambayo wanatumia viuatilifu na mwisho sehemu ya maji hayo
yanarudi mtoni yakiwa na viambata sumu kama hawatazingatia matumizi salama ya
viuatilifu, mwisho yaweza pelekea kuua viumbe walio mtoni na kuathiri pia jamii
inayotegemea maji ya mto huo kwa matumizi ya nyumbani.

Naye Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya
maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI)
amesema mimea hiyo ni muhimu kwa kuwa ndiyo inayosaidia kuwepo kwa uhai wa
mto kwa kutunza maji, kufyonza mbolea na kuyafanya yatiririke kidogokidogo badala
ya kasi pamoja na kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito.

“Tunapoangalia hali ya Uoto kwenye mito na afya ya mto huwa tunatumia madaraja A
mpaka F, hivyo tunaposema hali ya ukanda fulani ni A maana yake hakuna uharibufu
katika eneo hilo, lakini ikiwa daraja B ina maana eneo limeanza kupata athari za
awali lakini hazijaanza kuleta madhara, na ikishuka kufikia daraja D ina maana athari
ni kubwa sana na ikifikia daraja F ina maana eneo hilo limeharibika sana, athari ni
kubwa sana na madhara yake ni makubwa sana ambapo si rahisi kurekebishika katika
hali ya kawaida. Tathmini yetu imeonesha kuwa yapo mabadiliko kadhaa ambayo
yametokana na shughuli za kilimo na ufugaji lakini kimsingi uharibifu wake kwenye
uoto wa kandokando za mto sio mkubwa sana na kupelekea kupata daraja B, hata
hivyo ni lazima jitihada zifanyike kusitisha changamoto hii kuendelea” alieleza Dkt.
Immanuel.

Amesema kuwa wamekuta mimea kama vile Msandali ambayo ni mimea yenye
matumizi mengi kama utengenezaji wa Manukato pamoja na mimea mingine rafiki wa

maji lakini inawezekana kutoweka kwa kuwa jamii zinafanya shughuli mbalimbali
kandokando ya mto huo na kuiathiri, hivyo jitihada za makusudi zichukuliwe na
mamlaka za usimamizi wa mito kunusuru mto kuachwa wazi.

Mradi huu wa Utafiti unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa
kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na
kutekelezwa katika Bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa ushirikiano
na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa Huduma za Misitu
(TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa ufadhili wa program ya

Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, kupitia michango ya nchi kumi wanachama wa
Azimio la Nairobi ambapo kwa Tanzania ni kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira,
katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Kivitendo wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi
chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.
Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama akizungumzia matokeo hayo mbee ya Waandishi wa habari nje ya mkutano huo.
Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akizungumzia eneo la utafiti wake.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili kutoka SUA akiwasilisha matokeo ya mradi huo wa utafiti wa miaka miwili mbele ya wadau.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad