HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 12, 2023

MFAHAMU MZEE ALIYEMFICHA NYERERE KWA SAA KUMI KWENYE KIHENGE NAMTUMBO

 

Na Albano Midelo,Namtumbo.

TAMASHA kubwa la kutangaza fursa mbalimbali zilizopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma linatarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 22 hadi 23 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya anazitaja baadhi ya fursa katika tamasha hilo ambalo limepewa jina la Namtumbo Kihenge ni kutangaza fursa za uwekezaji kwenye sekta ya utalii kwa kuwa wilaya hiyo pia imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii wa kiikolojia,kihistoria
na kiutamaduni.

“Sisi Wilaya ya Namtumbo ni miongoni mwa Wilaya nchini ambazo zimebeba historia kubwa katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika ambao ulipatikana mwaka 1961’’,alisema.

Analitaja eneo la kitongoji cha Mikulumo kata ya Luegu wilayani Namtumbo kuwa lina historia iliyotukuta hapa nchini kwa kuwa ni eneo ambalo alijificha baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere wakati anatafutwa na askari wa wakoloni katika harakati za kudai Uhuru kuanzia Novemba 24 hadi 25,1955.

Anasema ili kulinda urithi wa eneo hilo serikali imeboresha mnara wa kumbukumbu ya Mwl.Nyerere na kwamba kati ya walinzi wanne waliomlinda Baba wa Taifa alipojificha katika eneo hilo mwaka 1955,walinzi watatu wamefariki lakini,mlinzi mmoja mzee Maulid Hassan mwenye umri
wa miaka 90 bado yupo hai na anaishi jirani na mnara huo.

Akizungumza namna alivyomficha Baba wa Taifa na kumuokoa kutoka kwa
askari wa wakoloni waliokuwa wanamsaka Baba wa Taifa mwaka
1955,Mzee Maulid anasema kipindi hicho akiwa kijana wa umri wa miaka
20 aliambiwa na baba yake mzee Hassan kumficha Nyerere ili asikamatwe
na wakoloni .

Anasema wazungu walipofika walimuulizia baba yake na yeye akajibu yupo
mjini kwenye mkutano na kwamba kwa siku tatu alikuwa hajarudi
nyumbani.

Mzee Maulid Hassan anabainisha kuwa baba wa Taifa alimficha kwenye
vihenge vya baba yake vya kuhifadhia chakula ambavyo vilikuwa nyuma
ya nyumba yao.

“Nilimficha Nyerere hapa kwenye vihenge wakati huo msitu ulikuwa mnene
sana,tangu asubuhi alishinda kutwa nzima kwenye vihenge,mama
alimpikia ugali wa ulezi na nyama ya kuku aliupenda sana nilikula naye na
kushinda naye kutwa nzima kwenye vihenge,niliamua kwa ujasiri lolote na
liwe, kama wazungu wakigundua bora mimi waniue na wamuache
Nyerere’’,alisisitiza Mzee Maulid.

Hata hivyo alisema muda wote aliokaa na Nyerere alikuwa anazungumzia
Tanganyika kupata Uhuru kutoka kwa wakoloni na kwamba katika kipindi
hicho yeye ndiye alikuwa mtu wa karibu wa Baba wa Taifa hadi
alipochukuliwa jioni na kuondoka akiwa salama kabisa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Luegu Ditha Kayombo
amelitaja eneo hilo kuwa lina utajiri wa historia ya Tanganyika kwa kuwa
hadi sasa mzee aliyemficha Baba wa Taifa akiwa wilayani Namtumbo
katika harakati za kudai Uhuru mwaka 1955 mzee Hassan bado yupo hai
na serikali imejenga mnara wa kumbukumbu katika eneo hilo.

Anatoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha eneo hilo kwa
kuongeza majengo na wananchi waliopo jirani na eneo hilo wasogezwe
pembeni ili eneo hilo libaki kuwa kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Mwl.Julius Nyerere.

Ameishauri Serikali kuhakikisha Mzee Maulid Hassan aliyemficha baba wa
Taifa ili kumuokoa na askari wa kikoloni mwaka 1955 anapatiwa huduma
za msingi kama vile maji,umeme,huduma ya afya na kujengewa makazi ya
kisasa.

Serikali wilayani Namtumbo imeamua kwa vitendo kumuunga mkono Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa
kuanzisha tamasha la Namtumbo Kihenge lililosheheni fursa lukuki za
uwekezaji na uchumi.
Kushoto ni Mzee Maulid Hassan mwenye umri wa miaka 90 ambaye alikuwa miongoni mwa walinzi wanne waliomficha  Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere kwenye kihenge katika kijiji cha Luegu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma katika harakati za kudai Uhuru mwaka 1955.Baba wa wa Taifa alikuwa anatafutwa na Askari wa kikoloni ambapo mzee huyo alimficha kwa saa kumi na baba wa Taifa kutoa salama.

Eneo lililokuwa na vihenge vya kuhifadhia chakula katika kijiji cha Luegu wilayani Namtumbo ambako baba wa Taifa alifichwa kwa saa kumi kwenye vihenge hivyo na kutolewa salama na kuendelea na safari ya kudai Uhuru.

Mnara wa kumbukumbu katika eneo la kijiji cha Luegu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma ambako Baba wa Taifa alijificha ili asikamtwe na askari wa wakoloni mwaka 1955 katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika.
Mzee Maulid Hassan mwenye umri wa miaka 90 Askari pekee alibakia hai kati ya Askari wanne waliomlinda na kumficha baba wa Taifa katika kijiji cha Luegu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika mwaka 1955.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya akiwa ofisini kwake mjini Namtumbo akizungumza kufanyika tamasha kubwa la kutangaza fursa mbalimballi zilizopo wilayani humo,tamasha hilo linatarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 22 hadi 23 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad