Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza katika kikao cha Mawaziri kuhusu Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika AGRF kilichofanyika ukumbi wa Maunt Meru Kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kabla ya wakuu wa nchi za Afrika kushiriki katika jukwa hilo Septemba 7,2023 ambapo amewasilisha mada kuhusu mambo mbalimbali ya kilimo na uwekezaji katika sekta kilimo nchini Tanzania.
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akizungumza katika kikao cha Mawaziri kuhusu Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika AGRF kilichofanyika ukumbi wa Maunt Meru Kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam.
Mawaziri na Viongozi mbalimbali wakishiriki katika mkutano huo.
Faraji Asas kutoka Kampuni ya ASAS Group pamoja na washiriki wengine wakishiriki mkutano huo.
Picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
ILI Mkulima aweze kuzalisha kwa tija anahitaji mbegu bora, kuwa na uhakika wa mbolea kwa wakati na kwa gharama nafuu lakini pia miundombinu ya maji ili aweze kuzalisha mara mbili mpaka tatu kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha mawaziri wa kilimo na uvuvi kutoka bara na visiwani pamoja na wadau wa sekta kwenye kikao cha Mawaziri kuhusu Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam leo Septemba 05, 2023. amesema nchi imeweka mazingira mazuri kwa ajili ya uwekazaji.
Amesema changamoto kubwa ni mitaji lakini pia uhakika wa mkulima kwenye kile anachokilima kwa wakulima wadogo hivyo wawekezaji wanapaswa kuweka mitaji yao ili kusaidia sekta hiyo kwani serikali imetenga ardhi ya kutosha kwa kituo cha uwekezaji (TIC) kwa ajili ya uwekezaji.
Amewataka wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwa ajili ya kumsaidia mkulima mdogo ili kufanya kilimo chenye tija na kulifanya bara la Afrika kujitegemea kwenye chakula hata yanapotokea majanga Duniani.
“Tumekutana hapa mawaziri wa kilimo ili kuwaonyesha wawekezaji maeneo ya kuwekeza ili kuboresha sekta hii kwani sasa hivi kilimo kimeshakua biashara na ndio maana tumefungua milango kwa mkulima kuuza mazao yake popote”amesema Bashe
Ameongeza kuwa kupitia mkutano huo wa AGRF wataonyesha dunia fursa zilizopo nchini katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha nchi inalima kwa tija lakini pia inaacha utegemezi wa chakula na badala yake inauza kwenye mataifa mengine,
Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kujikita kwenye sekta ya kilimo kutasaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana lakini pia kupunguza kutumia pesa nyingi kuagiza chakula kutoka nje.
Amesema kilimo sasa imekuwa sekta ya biashara hivyo inapaswa kutumiwa ili kubadilisha maisha ya vijana kwani nchi inaenda kujitegemea katika chakula lakini pia kuzalisha ajira nyingi hali itakayopelekea kuzalisha walipakodi wengi.
“Idadi ya watu wanaohitaji ajira ni kubwa hivyo juhudi za serikali ni kuingiza vijana wengi na wanawake kwenye sekta ya kilimo kwani sasa hivi kilimo kimekuwa biashara hivyo mapato ya serikali yataongezeka ikiwa sekta hii itakua na kuwekezwa ili izalishe kisasa”amesema Mwigulu
Akizungumzia kuhusu nini kifanyike ili kuboresha sekta ya kilimo na uvuvi, Waziri wa Uvuvi na Mifungo Abdalla Ulega amesema ili kuboresha sekta ya kilimo,uvuvi na mifugo teknolojia, masoko na mitaji inahitajika hivyo wawekezaji wanapaswa kuwekeza ili kukuza sekta hiyo ili kuzalisha kwa tija na kuuza nje.
Mkutano wa mifumo ya chakula Afrika AGRF unafanyika jijini Dar es salaam ambapo unahudhuriwa na watu zaidi ya 3000 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kuanzia leo Septemba 05, 2023.
No comments:
Post a Comment