HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 24, 2023

VULI 2023: MVUA ZA JUU YA WASTANI HADI WASTANI ZINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI

 


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2023 na kusema kuwa mvua hizo zitakuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani

"Mvua hizo zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023.

Aidha, maeneo ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani pia.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislous Chang'a amesema hayo leo Agosti 24, 2023 wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), katika ukumbi wa Ubungo Plaza,Dar es Salaam.

Dkt. Chang'a amefafanua kuwa kutokana na uwepo wa El-Niño, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini.

Amesema, mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi. “Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023. Kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023”. Amesema Dkt. Chang’a.

Kufuatia utabiri huo, Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba,kupanda na kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati kutokana na kutokana na magonjwa kama vile ukungu kuathiri mazao,pia kwa wafugaji tunawashauri kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadae,"amesema.

Kuhusu usafiri na usafirishaji,Dk Chang'a amesema kutokana na utabiri huo miundombinu ya usafiri inaweza kuathirika kutokana na na hali ya hewa hivyo wadau wa sekta hiyo wanatakiwa kuchukua hatua stahiki na kukagua mara kwa mara miundombinu hiyo.

Eneo afya, Dk Chang'a amesema kutakuwepo na uwezekano wa kutatokea magonjwa ya mlipuko kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji taka unaosababishwa na maji kutuama na kutiririka hivyo wananchi wanapaswa kutibu maji ya kuyatumia.

Aidha, Dkt. Chang'a ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa saa24, na tahadhari zinazotolewa na TMA ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.

Dkt. Chang’a alisema, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.

Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad