UKUSANYAJI WA MAPATO BADO NI CHANGAMOTO KUTOKANA NA UKUBWA WA SEKTA ISIYO RASMI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 30, 2023

UKUSANYAJI WA MAPATO BADO NI CHANGAMOTO KUTOKANA NA UKUBWA WA SEKTA ISIYO RASMI

 


Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea katika nchi za Afrika, bado kuna changamoto ya ukusanyaji wa mapato kutokana na ukubwa wa sekta isiyo rasmi.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, utafiti unapaswa kufanyika kwa kushirikisha taasisi mbalimbali, kuwa na mifumo ya kisasa itakayogusa maeneo mengi yanayoweza kuipatia serikali mapato.

Aidha, ameagiza mamlaka za mapato kutunga sera nzuri zitakazovutia ulipaji kodi wa hiari na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliyasema hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais, alipokuwa akifungua mkutano wa nane wa Jukwaa la Kodi Afrika (ATAF).

Amesema kuwa takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kwamba mchango wa kodi kwenye pato la taifa ni asilimia 14.55 hivyo, alielekeza uwepo ushirikiano baina ya watafiti, watunga sera na watendaji kwenye mamlaka za kodi ili kuunganisha nguvu kuiwesesha serikali kupata mapato ya kutosha.

"Mapato haya yatatusaidia katika kuwekeza kwenye sekta muhimu za afya, elimu na miundombinu na kuweka mifumo rahisi inayotekelezeka,” alisema Dk Mpango.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alisema wizara yake iko tayari kuongeza nguvu kwenye eneo la utafiti ili kutunga sera nzuri za kikodi zinazoendana na mazingira yaliyopo.

Amesema Afrika ni bara lenye uchumi unaokua kwa kasi unaoongeza watu wenye mapato makubwa hivyo ni muda muafaka kuwa na kuwa na njia nzuri ya kuwatoza kodi.

"Afrika imebarikiwa kuwa na maliasili nyingi ambazo zinaweza kutatua changamoto za kiuchumi na kujiletea maendeleo. Kuongeza matumizi ya teknolojia ni eneo lingine ambalo linapaswa kuangaliwa ili biashara na uwekezaji wa kiteknolojia viweze kuziingizia nchi mapato," amefafanua Dk Nchemba.

Naye, Katibu Mtendaji wa ATAF, Logan Wort, alisema lengo la jukwaa hilo ni kutafiti na kutoa njia bora za kuongeza wigo wa makusanyo ya serikali.

Amesema takwimu zinaonesha kwamba Bara la Afrika linapoteza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 88 kutokana na kushindwa kukusanya kodi.

Amesisitiza kuwa mkutano huo umewakutanisha wataalamu zaidi ya 300 kutoka nchi 43 barani Afrika, ukiwa na kauli mbiu ya ‘Masuala ya kikodi yanayojiri.’

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili tafiti 43 za kikodi kati ya 150 zilizowasilishwa na kwamba lengo ni kutoa mapendekezo ya maeneo mapya ya kikodi zikiwamo sekta za gesi, mafuta, madini, mazingira na biashara za kiteknolojia.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Gaudence Kayombo, alisema jukwaa hilo limezikutanisha taasisi za mamlaka ya mapato barani Afrika, watafiti na wadau wengine kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kwa kuangalia vyanzo vipya vya mapato.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda akifungua mkutano mkuu wa 8 wa Jukwaa la kodi (ATAF)wa mwaka kwa niaba ya Mkamu wa Rais Dk Philip Mpango jijini Dar es Salaam.  Katika mkutano hao wamejadili masuala mbalimbali ya Kodi Barani Afrika.
Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa 8 wa mwaka wa Jukwaa la kodi,  wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda aliyefungua mkutano huo kwa niaba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kujadili masuala mbalimbali ya Kodi Barani Afrika.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad