MWEKEZAJI: HAUWEZI KUNUNUA BANDARI, TUTAKUWA WAJINGA KUKATAA UWEKEZAJI HUU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 4, 2023

MWEKEZAJI: HAUWEZI KUNUNUA BANDARI, TUTAKUWA WAJINGA KUKATAA UWEKEZAJI HUU


Nazir Karamagi, mmoja wa watu ambaye ametajwa muda mrefu kuwa mmiliki wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Bandarini (TICTS), iliyokuwa ikifanya kazi ya kupakia na kupakua makontena ya mizigo katika Bandari ya Dar Es Salaam, amekiri kuwa uwezo wa TICTS kuhudumia bandari hiyo hauwezi kumudu mahitaji ya sasa, huku akionesha umuhimu wa Tanzania kuchangamkia fursa ya mwekezaji mwingine, atayakeboresha utendaji kazi na ufanisi wa bandari hiyo na kuitumia kimkakati kuongeza mapato ya nchi.

Akizungumzia kwa mlengo wa falsafa ya biashara na uwekezaji wenye manufaa, ambao utasaidia nchi kuitumia bandari kimkakati kuwa mojawapo ya vyanzo vitakavyoongeza mapato, ambayo hatimae yatasaidia Serikali kuacha kutoza kodi nyingi wananchi wake, Mzee Karamagi amesisitiza kuwa uwekezaji wa bandari ni tofauti na maeneo mengine, ambapo bandarini kinachowekezwa ni uendeshaji, huku miundombinu ikiendelea kubakia mikononi mwa Serikali.

“Sisi tulikaa pale (Bandari ya Dar Es Salaam) kwa miaka 22, tulinunua bandari? Si mkataba umekwisha, tunamwachia mwenye bandari, anatafuta wengine. Tulipokuwa pale tunaweza kusema bandari ni ya kwetu? Miundombinu ya bandari inabaki mikononi mwa Serikali. Kwa hiyo, hilo mtu asipolijua atachanganya uwekezaji, auchanganye na ununuaji kama ilivyokuwa katika mashirika mengine.

"Mimi ni Karamagi ambaye ni mwasisi wa Kampuni ya TICTS. Wameizungumzia saaana. Ukiangalia, inaonesha kwamba Serikali zetu zote hazijafanya makosa katika uwekezaji ili taifa letu linufaike. TICTS imefanya kazi vizuri, ingawa kwa sasa tulipofikia Serikali imesema basi hebu tujaribu na wengine, ambalo si baya. TICTS wakati inaingia, bandari yetu ilikuwa makontena elfu sabini (70,000) kwa mwaka. Sasa hivi ni laki saba (700,000) kwa mwaka. Lakini tulipofika, mkataba wetu ukafika pale mwisho. Sisi hatuna matatizo na hilo, nchi kwanza. Kwa sbaabu kuna mkakati mkubwa, ambao ni uchumi,” amesema Karamagi na kuongeza;

"Kabla sijakupa maiki (Mhe. Katibu Mkuu Chongolo) naomba nikwambie kwanini mimi naunga mkono DP World, mimi sio mwanasheria, sitazungumzia vifungu vya sheria, nitazungumzia falsafa ya biashara. Naungana kwa hilo na Profesa Kitila. Serikali imewekeza zaidi ya trilion 1 kwenye uboreshaji wa bandari gati 0 mpaka namba 7. Mpaka leo hii eneo hili linachangia kwa makontena asilimia 15% tu ya makontena yote yanayotoka Bandari ya Dar es Salaam.”

Kampuni hiyo ya TICTS imekuwa ikifanya kazi ya kupakia na kupakua makotena katika Bandari ya Dar Es Salaam, kwenye magati ya makontena, tangu mwaka 2000, kwa mkataba uliodumu kwa miaka 22, hadi ulipofikia tamati mwishoni mwa mwaka jana na Serikali, kupitia Bodi ya Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA), kufikia uamuzi wa kutoiongezea muda mwingine na kuamua kutafuta wawekezaji wengine watakaoboresha utendaji kazi na ufanisi wa Bandari ya Dar Es Salaam.

Kwa mujibu wa Makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai yanayoweka msingi wa kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uboreshaji wa uendeshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam, mwekezaji atawekeza katika magati namba 0 hadi 7, pekee katika bandari hiyo, tofauti na upotoshaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaopinga uwekezaji huo, wakipotosha kuwa atapewa maeneo yote ya bandari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad