Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi akimkabidhi kiongozi wa vijana wanaokwenda kutembea kwa miguu katika mikoa 16 nchini kuunga mkono kazi za Rais Samia Suluhu Hassan na kuhimiza vijana kuchapa kazi, Abiudi Maugo, bendera ya taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi (katikati) akiwa na vijana wanaokwenda kutembea kwa miguu katika mikoa 16 nchini. Kulia kwa DC ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke na kushoto kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika.
Na Khadija Kalili Michuzi Tv
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Mobhare Matinyi, amewaagiza vijana saba wazalendo ambao wameondoka Dar es Salaam leo asubuhi kuanza matembezi ya Mikoa 16 ambapo watazitangaza kazi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
DC Matinyi anewakabidhi bendera ya taifa kwenye hafla fupi iliyofanyika ofisini kwake leo asubuhi Agosti 15 2023 , amezitaja baadhi ya kazi zilizofanywa Wilayani Temeke mwaka 2022/23 na thamani ya fedha zilizotolewa na Rais Samia kuwa ni pamoja na miradi ya afya sh. bilioni6.1, elimu ya msingi sh. bilioni 7.6, elimu ya sekondari sh. bilioni 10, maji sh. bilioni 15.5, umeme sh. bilioni 61.6 na barabara sh. bilioni 43.7.
Amesema kwa ujumla Wilaya ya Temeke imepatiwa na Rais Samia zaidi sh. bilioni 152 katika kipindi hicho kutokana na wingi wa wakaazi wake ambao wanafikia milioni 1.35 na nia yake ya kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Aidha amewaaambia vijana hao kuwa katika kilomita 3,624 wanazotarajia kutembea kwa miguu watakutana na ushahidi lukuki wa kazi za Rais Dkt. Samia.
Vijana hao saba wanaoongozwa na Abihudi Maugo wanatarajiwa kuhitimisha matembezi yao Mkoani Manyara wakati wa sherehe za kuuzima mwenge hapo Oktoba 14, 2023.
Vijana wengine ni Sophia Kooni, Beatrice Masanja, Shabani Juma, Jesca Giribert, Flora Ernest na Paul Mkinga.
Hii ni mara ya nane kwa vijana wa Temeke kufanya matembezi nchini kuunga mkono matukio au dhima tofauti.
No comments:
Post a Comment