HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 24, 2023

Benki ya CRDB yaidhinishwa na CMSA kutoa hatifungani ya kijani

Dar es Salaam, 24 Agosti 2023: Katika juhudi za kuongeza uwezo wake wa kufanya uwezeshaji wa miradi rafiki kwa mazingira, Benki ya CRDB imepata idhini kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuuza Hatifungani ya Kijani (Green Bond) yenye thamani ya dola 300 milioni za Marekani (takriban Shilingi bilioni 780). Benki ya CRDB inaweka historia ya kuwa taasisi ya kwanza kutoa hatifungani ya kijani hapa nchini inayoweka mkazo katika masuala ya mazingira na kubwa zaidi kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumza wakati wa kupokea idhini ya kuuzwa kwa hatifungani hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema ni furaha kubwa kupata idhini kutoka CMSA kuiuza hatifungani hiyo ambayo lengo lake si tu kupata rasilimali fedha bali kufanikisha utekelezaji wa miradi yenye mrengo wa kuhifadhi mazingira hivyo kushiriki ipasavyo katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Pamoja na kuwa Benki ya CRDB inaweka rekodi ya kuwa taasisi kubwa zaidi ya fedha nchini kupata idhini ya kuuza hatifungani ya kijani, lakini Benki yetu sio ngeni katika uwezeshaji wa miradi yenye mrengo wa utunzaji mazingira kwani Novemba 2019 ilitambuliwa na kuingia makubaliano na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (GCF) kufanikisha miradi ya kulinda mazingira. Hii pia ilikuwa ni mara ya kwanza benki ya biashara kusini mwa Jangwa la Sahara kutunukiwa sifa hiyo na tangu hapo, tumeshiriki kwa kiasi kikubwa kuwezesha miradi inayokusudia kulinda mazingira,” amesema Nsekela.

Kuhusu uwezeshaji wa miradi ya mazingira, Nsekela amesema kwa mwaka jana pekee, Benki ya CRDB ilikopesha jumla ya shilingi trilioni 6.978 ambazo ni sawa na asilimia 26 ya mikopo yote iliyotolewa na taasisi za fedha nchini. Katika fedha hizo, amesema shilingi bilioni 1.44 zilikopeshwa katika sekta ya misitu, kiasi hicho ni sawa na asilimia 55 ya mikopo yote iliyotolewa kwenye sekta ya misitu.  
Kwenye kilimo, sekta muhimu kwenye uhifadhi wa mazingira na inayotoa ajira nyingi zaidi nchini na kulipa Taifa fedha nyingi za kigeni, amesema benki hiyo ilikopesha takriban shilingi trilioni moja ambazo ni sawa na asilimia 43 ya mikopo yote iliyotolewa kwenye eneo hilo na ikapeleka shilingi bilioni 55.88 kwenye sekta ya nishati mbadala.

Licha ya jitihada hizo, mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya fedha kuliko uwezo walionao hivyo kutafuta namna rafiki ya kufanikisha suala hilo.

“Kwa kutambua mahitaji yaliyopo, Benki ya CRDB imeona ni muhimu kutafuta vyanzo vipya vya fedha kuwezesha miradi hii. Leo nina furaha kuona jitihada zetu zimezaa matunda kwa CMSA kutupa idhini ya kuuza hatifungani yetu ya kijani (green bond) ambayo itauzwa kwa awamu tano ambapo katika awamu hii ya kwanza tunatarajia kupata shilingi bilioni 55,” amesema Nsekela.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama ameipongeza Benki ya CRDB kwa kufanikiwa kuwa Benki ya kwanza nchini kupata idhini ya kutoa hatifungani itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na matokeo chanya kwa jamii yaani green, social and sustainability bond. 

Idhini imetolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; Miongozo ya Utoaji wa Hatifungani yaani “Capital Markets and Securities (Guidelines for issuance of Corporate Bonds”; uwepo wa Muundo wa Hatifungani yaani Green, Social and Sustainability Bond Framework; Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji yaani International Capital Markets Association (ICMA); na kupata ithibati kutoka kwa taasisi zenye utaalam kuhusu miradi ya kuhifadhi mazingira na matokeo chanya kwa jamii. 

Amesema Benki ya CRDB imekidhi matakwa haya na kupata ithibati kutoka Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika, FSD Africa na Taasisi ya Sustainalytics ya Uingereza. Hatifungani hii inaweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza yenye lrngo la kuhifadhi mazingira na matokeo chanya kwa Jamii kutolewa nchini Tanzania na katika Ukanda kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mkama amefafanua kuwa, utoaji wa hatifungani hii ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi hapa nchini, kwani utachangia katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha yaani National Financial Sector Development Master Plan 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya miradi katika sekta ya umma na binasi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Mkama amesema kuwa CMSA imeidhinisha utoaji wa hatifungani hii itakayotoa mikopo kwa shilingi na fedha za kigeni (multicurrencies) kutokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria na kiutendaji ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi madhubuti wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mkama amehitimisha kwa kutoa rai kwa wadau wote wa sekta ya fedha kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) katika kutekeleza mikakati ya upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo kwa kutoa bidhaa mpya na bunifu zenye lengo la kuhifadhi mazingira, na zenye mguso na matokeo chanya kwa jamii hivyo kuchangia katika kuchochea maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi nchini. 
Akiishukuru CMSA na wadau wengine walioshiriki mchakato mzima mpaka kupatikana kwa kibali hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay amesema wawekezaji wa ndani na watokao nje wanayo fursa ya kunufaika na hatifungani hii kwani mikopo itapatikana kwa shilingi au dola ya Marekani. 

“Mara nyingi, Benki ya CRDB imekuwa ya kwanza. Leo hii ni fursa nyingine kwa benki hii kuorodhesha hatifungani kubwa zaidi, sio nchini pekee bali kwa nchi zote za kusini mwa Jangwa la Sahara. Nawashukuru CMSA na Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na wadau wengine waliotusaidia kufanikisha hili. Nawaomba Watanzania wenzangu kujitokeza kununua hatifungani hii pindi itakapoanza kuuzwa muda si mrefu kutoka leo. Tusiiache fursa hii itupite,” amesema Dkt Laay.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama akikabidhi kibali cha kutoa hatifungani ya kijani "green bond" yenye ya thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na Shilingi bilioni 780 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam. Hatifungani hiyo ni ya kwanza kutolewa Tanzania na ya kwanza kwa ukubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Picha zote na Othman Michuzi.
Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru akizungumza katika hafla kukabidhi kibali cha kutoa hatifungani ya kijani "green bond" yenye ya thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na Shilingi bilioni 780 kwa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika hafla kukabidhi kibali cha kutoa hatifungani ya kijani "green bond" yenye ya thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na Shilingi bilioni 780 kwa Benki ya CRDB, iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam leo.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad