Na Mwandishi Wetu , Mwanza.
KITUO cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimefanya uzinduzi wa Jukwaa la Majadiliano ngazi ya wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza ambalo litaviwezesha vyama vya siasa kujadili tofauti zao.
Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Julai 21, 2023, wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini wamemchagua Salum Mkumbukwa (CUF) kuwa Mwenyekiti na Geoffrey Kavenga (CCM) kuwa Katibu wa TCD wa wilaya hiyo.
Mjumbe wa TCD Taifa, Victory Mnyaga amesema jukwaa hilo litatumika kubainisha changamoto za kisiasa zinazoibuka na kuzijadili kisha kuzitafutia mwarobaini wake.
"Jukwaa hili litafanya vikao na kujadili changamoto za kisiasa na kutafuta mwafaka wake. Kama kuna migogoro baina ya vyama vya siasa ambayo inaweza kutatuliwa katika ngazi hii itapatiwa ufumbuzi," amesema Mnyaga
Mwenyekiti wa TCD wilaya ya Nyamagana, Salum Mkumbukwa ameishukuru TCD kwa hatua hiyo huku akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza jukwaa hilo.
"Tumekuwa tukipitia changamoto na migogoro mbalimbali ya kisiasa katika maeneo yetu. Pamoja na kwamba bado Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea na maridhiano lakini jukwaa hili litatusaidia kuwa sehemu ya kutatua changamoto zetu," amesema Mkumbukwa.
Kikao cha jukwaa hilo kimehudhuriwa na watu zaidi ya 25 wakijumuisha wenyeviti, makatibu na wajumbe wa kamati tendaji za vyama vya siasa ikiwemo CCM, Chadema, CUF, ACT Wazalendo na mwakilishi kutoka Asasi za Kiraia (Azaki).
No comments:
Post a Comment