TCAA YATOA UFAFANUZI KUHUSU ZOEZI LA UTAFUTAJI NA UOKOAJI WA NDEGE MKURANGA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 27, 2023

TCAA YATOA UFAFANUZI KUHUSU ZOEZI LA UTAFUTAJI NA UOKOAJI WA NDEGE MKURANGA

 


Kutokana na utafutaji na uokoaji wa ndege ya abiria iliyoanguka katika kijiji cha Msufini Kidete, Kata ya Mbezi, tarafa ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani ikiwa inatoka katika uwanja wa Kilwa Masoko na kuelekea uwanja Tanga Ndege hiyo aina ya Embraer 120 (E120) ilikuwa imebeba abiria 25 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetoa taarifa kwa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege, Flora Alphonce amesema tukio hilo lilikuwa ni zoezi ambalo lengo lake ni kupima uwezo na utayari wetu kama nchi wa kukabiliana na matukio ya utafutaji na uokoaji pindi ndege zinazopata ajali kwenye nchi kavu au majini na pia nyombo vya majini.

Amesema zoezi hili limeandaliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo inajukumu la kuratibu na kusimamia huduma ya utafutaji na uokoaji wa ndege zinazopata ajali kwenye anga la Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi za udhibiti wa usafiri wa majini ambazo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa Tanzania bara na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini (ZMA) kwa upande wa Zanzibar.

Bi. Flora amesema zoezi hilo lilihushisha taasisi za utafutaji na uokoaji za umma na binafsi zikiwemo Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mashirika ya ndege, Mashirika ya vyombo vya majini, Mamlaka ya viwanja vya ndege (TAA), Mamlaka ya hali ya hewa (TMA), Hospitali, Shirika la msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross), Wavuvi, pamoja wadau wengine mtambuka wa utafutaji na uokoaji ambapo kauli mbiu ya zoezi la mwaka huu 2023 ni “Okoa Maisha” (Save life).

"Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Utafutaji na Uokoaji Majini wa mwaka 1979 (International Convention on Maritime Search and Rescue, (SAR Convetion,1979) unazungumzia kuhusu masuala ya utafutaji na uokoaji katika usafiri wa majini." alisema Flora

Pia amesema mikataba hiyo yote inayosimamiwa na ICAO na IMO inazitaka nchi wanachama kutoa huduma za utafutaji na uokoaji katika usafiri wa anga na majini wakati ajali na matukio ya dharura ya vyombo vya usafiri wa anga na majini ndani ya eneo la nchi mwanachama na wa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, eneo la nchi la utafutaji na uokoaji ni mipaka ya kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na eneo la Bahari ya Hindi kuanzia pwani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Mashariki hadi Longitudi nyuzi 44 (440E) pamoja na maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Amesisitiza kuwa katika utekelezaji wa maelekezo yaliyo katika Mwongozo huo, Tanzania imeimarisha na kuboresha vituo vya kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji katika usafiri wa anga na majini ambavyo Vituo hivyo vinavyojulikana kama Aeronautical Rescue Coordination Centre (ARCC) ambacho kipo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Maritime Rescue Coordination Centre (MRCC) ambacho kipo eneo la Magogoni, Dar es Salaam. Kituo cha ARCC kinasimamiwa na TCAA na kituo cha MRCC kinasimamiwa na TASAC.

Amesema mwongozo huo wa ICAO na IMO unazitaka nchi wanachama kufanya majaribio au mazoezi ili kupima uwezo na utayari wa taasisi zote zinazohusika katika kutoa huduma hii muhimu ya utafutaji na uokoaji hivyo kufanya mazoezi haya ni kutekeleza matakwa ya sheria na mikataba ya kimataifa ili kuboresha mifumo, taratibu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Meneja Uhusiano na Mawasiliano TCAA Bw. Yessaya Mwakifulefule amesem zoezi hili limehusisha waangalizi wa ndani na nje ya nchi ili kutathmini maeneo yanahitaji kuboreshwa ili huduma hii itolewe kwa ufanisi mkubwa. Waangalizi hao ni kutoka Shirika la kimataifa la usafiri wa anga duniani (ICAO), Mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Mashirika ya vyombo vya majini. Waangalizi hawa watatoa ripoti ambazo zitafanyiwa kazi ya kamati ya kitaifa ya utafutaji na uokoaji wa ajali za ndege na vyombo vya majini.
Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege, Flora Alphonce (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utafutaji na uokoaji wa ndege ya abiria iliyoanguka katika kijiji cha Msufini Kidete, Kata ya Mbezi, tarafa ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani wakati wa zoezi la uhokoaji lenye lengo la kupima ufanisi katika taasisi mbalimbali zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya Usafiri wa anga. Kulia ni Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw Yessaya Mwakifulefule
Meneja Mahusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw Yessaya Mwakifulefule akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa taarifa kamili utafutaji na uokoaji wa ndege ya abiria iliyoanguka katika kijiji cha Msufini Kidete, Kata ya Mbezi, tarafa ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani.
Viongozi wa kitengo cha Utafutaji na Uokoaji wa Ndege wakifuatilia mkutano huo
Viongozi waandamizi wa Idara ya Uongozaji ndege wakifuatilia mkutano huo

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad