ORYX GAS YATOA MITUNGI 500 NA MAJIKO YAKE KWA MAMA LISHE JIMBONI KWA WAZIRI MABULA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 30, 2023

ORYX GAS YATOA MITUNGI 500 NA MAJIKO YAKE KWA MAMA LISHE JIMBONI KWA WAZIRI MABULA

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WANAWAKE wajasiriamali ambao wanajishughulisha na shughuli za Mama Lishe katika wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wamepatiwa mitungi 500 ya Oryx Gas pamoja na majiko yake bure, lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Wilaya ya Ilemela wakiongozwa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk.Angelina Mabula,Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Araman Benoite alisema wameendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda na kutunza mazingira kwa kuhamasisha nishati safi ya kupikia.

“Katika muendelezo huo wa kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama kwa kupikia ambapo Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited imekuwa mstari wa mbele kufikia azma hiyo, leo kampuni yetu imetoa macho kwa vikundi vya wafanyabiashara wa vyakula (Mama Lishe) Wilaya ya Ilemela kwa kuwakabidhi mitungi  500 ikiwa na gesi yake bure,alisema Benoite.

“Utoaji huu wa mitungi ya Oryx umefanikiwa kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.Malengo ya kampuni ni dhahiri kuona mabadiliko katika matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia kwa jamii zote za Watanzania,”alisema.

Aliongeza na hiyo inaendana na mpango wa Serikali wa miaka 10 wa matumizi salama ya nishati safi ya kupikia huku akifafanua wanafahamu kundi la Mama Lishe kila siku wanahudumia chakula cha Watanzania wengi, wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.

“Hivyo Oryx Gas kwa kushirikiana na Dk.Mabula, wameamua kuunga mkono jumuiya hii kama motisha kwa wengine kwa ajili ya mabadiliko.

“Mwanza na mikoa ya kanda ya ziwa imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya chakula hivyo juhudi kubwa inahitajika kulinda afya na kuokoa mazingira ya ukanda huu na maeneo mengine nchini,”alisema.

Aliongeza Oryx Gas inawekeza katika siku zijazo kwa kutekeleza mipango ya kukabiliana na kaboni kupitia elimu ya upishi safi, uchangiaji wa vifaa vya kuanzisha LPG bila malipo kwa baadhi ya mikoa, uhamasishaji wa matumizi ya LPG kupitia uuzaji mkubwa wa mitungi ya gesi kwa bei nafuu.

“Juhudi hizo zinazolenga kuhakikisha Watanzania walio wengi wanatumia nishati safi ya kupikia.Rais Samia Suluhu ameweka lengo la Watanzania kutumia nishati safi kwa asilimia 80 ya watu wote ifikapo mwaka 2032.Kampuni ya Oryx Gas Tanzania inajivunia kuunga mkono maono yake katika kutoa nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wengi,”alisisitiza Benoite.

Kwa upande wake Dk.Mabula alisema kuwa mitungi hiyo ya gesi imetolewa katika kata zote 19 katika wilaya ya Ilemela na wameigawa kulingana na shughuli ambazo zinafanywa na Mama Lishe ambalo ni kundi muhimu katika jamii.

“Tunaona namna ambavyo akina mama  wanapata shida katika kufanya shughuli zao kwa haraka lakini katika mazingira mazuri, lakini tunahitaji kutunza mazingira yetu. Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amedhamiria  kuhakikisha huduma zote anazotoa kaanzia kwenye huduma za uchumi, kaja kwenye elimu lakini uwekezaji ameupa kipaumbele

“Ukija kwenye huduma za jamii akina mama wengi wamekuwa wakihanagika kutafuta kuni na mkaa , wanakwenda kufyeka misitu.Tumetajiwa mpaka kiwango cha uharibifu ambacho kimefanyika.Sasa tunapopata kampuni kama hizi ambazo ziko tayari kuwekeza katika afya na utunzaji bora wa mazingira yetu, lazima tuwashukuru,”alisema Dk.Mabula.

Alifafanua mitungi hiyo imetolewa bure ikiwa na gesi lakini anaamini wakishaona faida yake wataendelea kutumia kwani inakupunguzia muda ukilinganisha na matumizi ya mkaa na kuni huku akifafanua mtungi huo ukitumika vizuri unatumika kati ya wiki tatu mpaka nne na gharama ua kujaza gesi ni Sh.24000.

“Gunia moja la mkaa linauzwa kati ya Sh. 70,000 mpaka 70,000 na ukilitumia kwa kubana hauzidi wiki tatu au mwezi mmoja,sasa niambie ni mitungi ya gesi mingapi katika hilo gunia moja unalolipata?Ni mitungi mitatu ambayo itakulepeka mpaka miezi mitatu.

“Katika hili naipongeza Oryx , lakini nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria mpaka kufikia mwaka 2032 tutakuwa tumesahau kabisa haya masuala ya kutumia kuni na mkaa.

“Ukiangalia hata kwenye Ilani yetu Ibara ya 62 inayozungumzia masuala ya nishati ,utaona masuala ya gesi yametajwa na tayari tuna gesi asilia inayotokana na mazao yetu sisi wenyewe kwa maana ya kwamba inazalishwa hapa nchini na sasa tunaendelea kupata gesi kama hii ya Oryx.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite akizungumza wakati wa tukio la ugawaji mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Mama Lishe waliopo katika Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Araman Benoite.

 Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akitoa elimu ya matumizi salama ya mtungi wa gesi ya Oryx kabla ya mitungi hiyo kukabidhiwa kwa wanawake wajasiriamali wilayani Ilemela mkoani Mwanza


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad