HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 16, 2023

MAKAMBA AYATAKA MAKAMPUNI YA BIMA NCHINI KUTUMIA FURSA KATIKA SEKTA YA NISHATI

Makampuni ya Bima nchini, yametakiwa kuhakikisha kwamba yanazitumia fursa zilizopo katika Sekta ya Nishati, kuzitambua na kufahamu kuwa wana nafasi ya kuzifikia na kuzipata.

Wito huo umetolewa tarehe 15 Julai, 2023 na Waziri wa Nishati, January Makamba wakati wa ufunguzi wa Semina ya kujadili ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati.

Waziri Makamba ametoa wito kwa wadau, wahusika makampuni ya Bima na wadau wengine, kufahamu kuwa, kwa upande wa Wizara ya Nishati, mlango uko wazi kuendelea kushirikiana nao, na kuwasiliana kwa karibu lakini pia kuna uwekezaji kwa upande wao wa ujuzi, maarifa ya mahitaji mahsusi ya Sekta ya Nishati ikiwemo upanuzi wa mtaji kutokana na ukubwa wa uwekezaji katika Sekta ya Nishati.

Akizungumzia kuhusu madhumuni ya mkutano huo, Waziri Makamba ameeleza kuwa, umelenga kujadiliana kati ya makampuni ya Bima ambayo yametengeneza umoja wao ambao unataka kujishughulisha na fursa zilizoko katika Sekta ya Nishati hasa Miradi ya Gesi na Mafuta, Miradi ya Umeme na miradi mingineyo katika Sekta ya Nishati.

“Kama mnavyofahamu, tunaelekea katika utekelezaji wa miradi mikubwa sana ya kimkakati ya Nishati ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani Tanga, Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia kule Lindi. Moja ya fursa zilizopo katika Miradi hiyo mikubwa ya kimkakati ya Nishati ni Bima.” Alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba alifafanua zaidi kuwa, Bima ni sehemu ya huduma ya fedha, ni Biashara kubwa na kuwa yapo makampuni 22 ambayo yametengeneza umoja wao hapa nchini na yameialika Wizara ya Nishati ili kufanya mazungumzo nao kueleza ni fursa zipi zilizopo za Bima katika Miradi ya Nishati na wanaweza kuzifikia vipi fursa hizo, ushirikiano ambao unaweza kuwepo kati ya Serikali, kati ya Wizara ya Nishati na Taasisi na kampuni hizi.

Amesema, mazungumzo ya kutengeneza Mradi wa Kusindika na Kuchakata Gesi kule Lindi Mradi yamemalizika na kulikuwa na mazungumzo na vipengele vinavyohusu Bima.
 

Waziri huyo wa Nishati ameeleza kuwa, Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Lindi ni fursa kubwa, thamani yake ni takribani shilingi trillioni 97 ambapo inabidi ukatiwe Bima. na Bima yake ni kubwa hivyo, makampuni hayo 22 yamejenga umoja ili kuhakikisha kwamba fursa hiyo wanaitumia na wanaifikia.

Makamba amesema, hapa nchini, ni Watanzania wachache wanaotumia Bima na mtawanyiko na matumizi ya Bima nchini bado ni madogo hivyo, ni matumaini kuwa mkutano huu ulioandaliwa na TIRA pamoja na makampuni mengine ya Bima itakuwa chachu katika kukuza Tasnia ya Bima hapa nchini.

Ameyapongeza Makampuni ya Bima nchini kwa kuchukua uamuzi huo wa kuanzisha umoja huo na kuipongeza sana TIRA kwa kuwaratibu na kuwakutanisha na Wizara ya Nishati.

Akijibu swali wakati wa mahojiano na Waandishi wa Habari, tofauti ya mahitaji ya Bima miradi ya Mafuta ikilinganishwa na miradi mingine, Waziri Makamba amesema, miradi ya kutafuta Mafuta na Gesi na Miradi ya uchakataji wa Mafuta na Gesi, ni miradi ambayo kwanza ni mikubwa, ya gharama kubwa, Teknolojia kubwa, ina mahitaji mahsusi na riski yake ni kubwa.

“mfano, unaweza ukachimba kisima cha bilioni 100 ukitegemea kupata mafuta au gesi na usipate. Unaweza ukichimba visima 100, ni visima 36 tu ndio unaweza kupata Gesi na Mafuta na mwekezaji yeyote anayetaka kuanza kuchimba mafuta au gesi anakata Bima ili asipopata ule uwekezaji urudishiwe.” Alisema Makamba.

Hivyo, Tasnia ya Gesi na Mafuta ni Tasnia Mahsusi, yenye mahitaji ya Bima mahsusi, kutokana na teknolojia yake, ukubwa wake na mahitaji yake. Hivyo, ni muhimu semina kama hizi kufanyika ili kupata uelewa wa pamoja kati ya Makampuni ya Bima lakini pia na Wataalam wa Tasnia ya Mafuta na Gesi.

Amesema, Wizara ya Nishati itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo haswa kwa upande wa Sekta ya Nishati kuhakikisha kwamba, makampuni ya ndani ya Bima yanazifikia hizo fursa, na kwamba zipo sheria ambazo zinaelekeza kuhakikisha kwamba kwa kadri inavyowezekana makampuni ya ndani, wajasiria mali wa ndani, wanufaike na uwekezaji huu unaokuja.

Lakini vilevile ili kunufaika na fursa hizi kuna mahitaji ya ukuaji, utaalam zaidi, uelewa zaidi wa Sekta ya Nishati kwa sababu, mtaji unaotumika ni mkubwa, teknolijia kubwa hivyo kuna mahitaji pia ya makampuni ya Bima kuelewa kuhusu mahitaji mahsusi kuhusu Sekta ya Nishati.

Amesema, kwa kadri makampuni ya ndani yanavyonufaika, yawe ni Bima, yawe ni ya ulinzi, usafirishaji, mabenki, ndivyo ambavyo uchumi wa nchi unapata manufaa zaidi, ajira zinaongezeka zaidi, kodi zinapatikana zaidi, kwa hiyo kuna manufaa mapana kwa nchi yetu pale wajasiria mali wa ndani wanapoweza kushiriki katika fursa hizi.

Akifafanua kuhusu ushiriki wa wazawa upande wa Bima kwenye miradi ya Nishati wakati wa Semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka ameeleza kuwa, ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa Makampuni ya Bima ya hapa nchini yanashiriki kikamilifu kwenye miradi ya Nishati.

Awali, Akizungumza wakati wa hotuba fupi ya kumkaribisha mgeni rasmi, kwenye Semina ya konsotia ya Mafuta na Gesi, Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware alisema, lengo la kuunda Konsotia (Ushirika wa Makampuni yanayoweka mitaji yao pamoja) ni kutokana na ukweli kuwa, miradi ya Nishati inahitaji mitaji mikubwa na pia ni miradi ambayo vihatarishi vyake au majanga viko juu sana ambapo kampuni moja moja inaweza kupata changamoto kwenye kumudu kukinga majanga yanayoweza kutokea kwenye miradi hivyo, na hivyo kupelekea muungano huo.

Amesema, ili kuweza kukinga miradi ya Nishati ni muhimu makampuni kuungana na kuweka mitaji pamoja ambapo jumla ya Makampuni 22 ya Bima yaliyosajiliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) yameshaweka mitaji yake pamoja yenye thamani ya dola milioni sita ili kukinga majanga kwenye miradi ya Nishati

Dkt. Baghayo Saqware, ameeleza kuwa, Kampuni Kiongozi ni Phoenix Insurance Company ambayo imeweka share kubwa katika Konsotia hiyo, ambapo itahusika na utafutaji wa masoko na kupokea sehemu ya majanga ambayo Konsotia haitaweza kuyamudu.

Ameeleza zaidi kuwa, Shirika la Bima la TANRE litashughulikia ulipaji wa madai ya majanga yaliyotokea na uwekezaji mitaji kwenye Konsotia.

Amesema, lengo la semina ni kutoa uelewa kwa Wizara ya Nishati pamoja na Wataalamu wa Timu ya Majadiliano ya Kitaifa ya Miradi ya Nishati kuhusiana na Konsotia, majukumu, manufaa na uendeshaji wa Konsotia pamoja na jinsi Konsotia inavyoweza kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya Nishati pamoja na maeneo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima kwa ajili ya uratibu wa Miradi mbalimbali ya Nishati.

Dkt. Saqware amesema, Konsotia hiyo ilizinduliwa tarehe 16 Novemba 2022 na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande.

Semina hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Luka Kitandula, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Iddi Kassim Idd, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo, Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Mhe. Dkt. Charles Kimei, Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Mhe. Zaituni Swai, Mkurugenzi Mtendaji PURA, Mha. Charles Sangweni, Naibu Kamishna wa Bima, Bi. Khadja Issa Said, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati na PURA.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.

Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka akizungumza wakati wa kufunga Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Luka Kitandula akizungumza wakati wa majadiliano kwenye Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mha. Charles Sangweni, akizungumza wakati wa majadiliano kwenye Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha. Kushoto kwake, wakimsikiliza Mha. Sangweni, ni Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Luka Kitandula

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo, akichangia jambo wakati wa majadiliano kwenye Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Luka Kitandula.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware wakati wa Semina ya kujadili ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu PURA Mha. Charles Sangweni na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, akifuatilia maoni yaliyokuwa yakitolewa na washiriki wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo na kushoto ni Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania, Bi. Khadja Issa Said.

Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware akifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Nishati, January Makamba, wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Dunstan Luka Kitandula.

Kamishna Msaidizi Sehemu ya Maendeleo ya Petroli wa Wizara ya Nishati, Marwa Petro, akifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Nishati, January Makamba wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha.


Washiriki wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati iliyofanyika tarehe 15 Julai, 2023 jijini Arusha, wakifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Waziri wa Nishati, January Makamba, wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujadili Ushiriki wa Kampuni za Bima nchini kwenye miradi ya Nishati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad