Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis- Bima za Mali na Ajali, Jabir Kigoda akizungumza wakati wa uzinduzi huo Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
BIMA mpya ya Kilimo ya Mtetezi iliyozinduliwa na kampuni ya Bima ya Strategis sasa inatarajiwa kumpa mkulima uhakika zaidi wa uwekezaji wake katika kilimo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Strategis- Bima za Mali na Ajali, Jabir Kigoda amesema bima hiyo mpya imezinduliwa ili kuhakikisha wakulima hawapati hasara endapo uzalishaji wao utakumbwa na majanga mbalimbali.
“Hapo awali wakulima hawakuwa na uhakika wa kupata mavuno kutokana na majanga mbalimbali ambayo huathiri mazao na kuwasababishia hasara kubwa mwisho wa siku.
"Tunaona juhudi na msukumo unaowekwa na Serikali yetu katika kusukuma kilimo, na watu wengi sasa wanawekeza katika kilimo. Uwekezaji huu inabidi ulindwe, na tunaamini Mtetezi ni suluhisho sahihi katika kulinda uwekezaji huu kwa wakulima” amesema Kigoda.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu huyo, bima hiyo mpya imeanzishwa ili kumkinga mkulima na majanga yanayo athiri mavuno kama vile hali hewa, wadudu, magonjwa na majanga mengine.
Ametoa wito kwa wakulima kote nchini waichangamkie bima hii mpya kwani itawapa Imani zaidi na nguvu ya kuwekeza zaidi kwa kuwa wataweza kuepuka hasara endapo majanga hayo yatatokea.
Kuhusu malipo ya madai, alisema kampuni ya Bima ya Strategis imekuwa ni mfano bora katika soko linapokuja suala la kulipa madai. Na ameahidi kuendelea kuilinda sifa yao hiyo pamoja na kuzingatia maagizo ya Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dk. Baghayo Saqware aliyetoa wito kwa Strategis kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati ili huduma hii ya bima ifanye vizuri sokoni.
Pia ametoa wito kwa wakulima wahakikishe wanajiunga katika makundi ili wapate bima hiyo kiurahisi. “Ni rahisi kuwahudumia wakiwa katika makundi kuliko mkulima mmoja mmoja,” alisema na kuongeza kuwa Strategis itakuwa karibu na wakulima kuwasaidia hatua kwa hatua ili bima hii iwanufaishe wengi.
Amesema timu ya watu mbalimbali kutoka kampuni ya bima ya Strategis tayari zimesambaa katika maeneo mbalimbali mikoani kutoa elimu zaidi kwa wakulima kuhusu bima hii ya Mtetezi.
No comments:
Post a Comment