HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 1, 2023

ZANZIBAR WAZINDUA KAMATI YA KUZUIA UDHALILISHAJI KIJINSIA

 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (wa pili kulia) akifungua pazia na Mkurugenzi Mastaka Zanzibar Mhe.Mgeni Jailani Jecha (wa tatu kushoto) ikiwa ni isahara ya Uzinduzi rasmi wa  Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar  leo  katika  Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil  Kikwajuni Jijini Zanzibar (kulia) Mke wa Rais Mama Mariam Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman (kushoto)  na Mwenyekiti wa Kamati Hiyo Bi.Mwanamkaa A.Mahmoud.
[Picha na Ikulu] 01/06/2023.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar, iangalie suala la matumizi na athari za mitandao kwa vijana ili serikali ijipange vyema na kwenye mwelekeo wa uhuru wa matumizi hayo kwa Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye hafla ya uzinduzi wa kamati ya kuzuia udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar huko ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakili, Kikwajuni Wilaya ya mjini.

Alisema, mitandao inapotumiwa vibaya ni kishawishi kimojawapo cha mmong’onyoko wa maadili na vitendo vya udhalilishaji.

“Naiagiza Kamati hii ifanye kazi ya kuchunguza athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la kesi za udhalilishaji, baada ya kufanya kazi hiyo, itoe ushauri na mapendekezo Serikalini ili tuwe na muelekeo bora zaidi juu ya uhuru na matumizi ya mitandao hapa Zanzibar”. Aliagiza Dk. Mwinyi.

Alieleza furaha yake kuona Kamati hio imeundwa ikiwa na lengo la kuzuia matukio ya udhalilishaji kabla ya kutokea, badala ya kupambana nayo yakiwa yameshaathiri jamii.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Kamati hiyo iangalie mapungufu ya Kisera, Sheria na Kanuni yaliopo ili watoe mapendekezo sambamba na kuweka malengo ya kimkakati yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kasi na haraka zaidi.

“Kwa vile ndani ya Kamati hii, wamo viongozi na wajumbe kutoka taasisi za elimu ya sekula na elimu ya dini, ninayo matumaini kwamba kamati hii itakuja na mapendekezo yatakayohusisha mitaala pamoja na uendeshaji na usimamizi mzuri wa skuli, madrasa na maeneo mengine yanayotoa mafunzo ya dini” alitanabahisha Dk. Mwinyi.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafarijika kuona jamii imesimama pamoja kuungamkono juhudi za Serikali kivitendo.

“Sote tunasimama pamoja kupiga vita janga la udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia. Hii ni ishara kwamba sote tunaguswa na uzito wa janga hili kwa kuzingatia madhara yake. Endapo vitendo hivi tutashindwa kuwa na mbinu mwafaka za kuvikabili, jamii yetu itakuwa na idadi kubwa ya washtakiwa wa makosa ya udhalilishaji”. Alitanabahisha Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwepo kwa tatizo la idadi kubwa ya watu wanaofungwa kwa kesi za udhalilishaji inaifanya jamii yetu kuwa na familia zinazokosa matunzo, hali aliyoieleza kusababisha mifarakano na kusalia kuwepo kwa kundi kubwa la watoto wanaokosa usimamizi wa familia zilizo madhubuti.

Hivyo, aliwataka wazazi na walezi wajitahidi kusimamia vyema maadili, hulka na silka za vijana wao na kuhakikisha wanawalinda na kuwawekea mipaka sahihi kwa kutowapa uhuru sana pamoja na kufuatilia mabadiliko ya tabia na mienendo yao ya kila siku kwani kesi nyingi za udhalilishaji wa kijinsia zilizopo kwenye vyombo vya sheria zinawahusisha vijana.

Alisema watoto na vijana wanaofanyiwa udhalilishaji huathirika kiafya na kisaikolojia, hali aliyoieleza kuchangia kuharibu mipango na muelekeo wao wa maisha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mwl. Haroun Ali Suleiman alisema kazi ilio mbele yao kamati aliyoizundua Rais Dk. Mwinyi ni utekelezaji wa vitendo katika juhudi za kumuungamono Rais katika mapambano dhidi ya udhalilishaji Zanzibar.

Naye, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, (DPP) Mgeni Jailani Jecha alisema vitendo vya udhalilishaji wa kijinsini vinazidi kuongezeka nchini badala ya kupungua.

Alieleza kwamba vinaweza kuimaliza jamii, jambo ambalo linazidi kuleta hofu na kutia dosari taifa
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hutuba yake ya  Uzinduzi wa Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar uliofanyika leo katika Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil  Kikwajuni Jijini Zanzibar,ambapo Viongozi na wadau wa Sekta mbali mbali walihudhuria.
Baadhi ya Wakuu wa vyombo vya Usalama na Viongozi wengine wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar uliofanyika leo Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar,mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Viongozi wa Taasisi mbali mbali na waalikwa wakiwa katika hafla ya Uzinduzi wa Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar uliofanyika leo Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar,mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Mke wa Rais Mama Mariam Mwinyi (katikati) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman (kulia) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (kushoto) wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Uzinduzi wa Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar uliofanyika leo katika Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar,mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Mkurugenzi Mastaka Zanzibar Mhe.Mgeni Jailani Jecha akisoma risala yake  katika  hafla ya   Uzinduzi wa Kamati ya Udhalilishaji wa Kijinsia Zanzibar uliofanyika leo katika Ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil  Kikwajuni Jijini Zanzibar,mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.
[Picha na Ikulu] 01/06/2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad