Wadau waipongeza serikali kwa kuwa na bajeti yenye mtazamo chanya - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 19, 2023

Wadau waipongeza serikali kwa kuwa na bajeti yenye mtazamo chanya

WADAU wameipongeza serikali kwa kuwa na bajeti yenye mtazamo chanya katika kuongeza walipakodi na kuvutia zaidi uwekezaji.

Wakizungumza wakati wa uchambuzi wa bajeti ya serikali kwa mwaka  2023/24 ulioandaliwa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya EY hapa nchini na kuwashirikisha wataalamu kadhaa wa masuala ya uchumi na fedha, uliofanyika Juni 19, 2023 katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, wamesema kuwa ukusanyaji wa kodi ukifanyika ipasavyo, utasaidia kutengeneza upya uchumi wa Tanzania.

Mshauri wa Masuala ya Kodi kutoka Kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya EY, Beatrice Melkiory amesema kuwa  kitendo cha kupunguza kodi kwa wawekezaji, serikali imelenga kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje  lengo likiwa ni kukuza uchumi.
Amesema kuwa serikali inategemea kodi kwa ajili ya kupata mapato yake na imeongeza wigo kwa walipakodi ili waweze kuingia kwenye eneo la kulipa kodi na kuongeza mapato.

"Kuna baadhi ya sekta ambazo serikali imetoa kipaumbele ikiwemo utalii ambako wanataka kutoa masamaha wa kodi ya ongezeko la thamani( VAT) hivyo wanategemea eneo kama hilo kutakuwa na mabadiliko kwa sekta hiyo kufanya vizuri na kuongeza idadi ya watalii nchini," amesema Melkiory.

Pia ameeleza serikali inataka kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya walipakodi ili walipe bila kupata bugudha zozote na hii itasaidia watu kulipa kodi kwa wakati.
Kwa upande wa walipakodi wadogo ambao wataingizwa kwenye mfumo na kutakiwa kulipa kodi ya asilimia mbili,  itakuwa kodi ya ziada na itasaidia serikali kupata mapato yake.

Kuhusu kuongezwa kwa kodi ya mafuta na saruji, Melkiory alisema kodi hizo zitaleta changamoto kwa sababu zitaongeza gharama za maisha kwa watu.

"Kuna mapendekezo ambayo tuliyapeleka na serikali imeyafanyia kazi naamini kutakuwa na mabadiliko zaidi katika bajeti yetu,"
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi kutoka ESRF, Vivian Kazi amesema kuwa bajeti imejali makundi na rika zote hususan vijana katika kuongeza ajira.

Amesema kati ya sekta ambazo zinaongeza ajira ni pamoja na kilimo, hivyo wanaamini kupitia Mradi wa BBT, vijana wataleta mabadiliko kwa kuzalisha chakula kwa wingi na kuuza nje ya nchi.

Amesema wawekezaji katika kilimo na viwanda wamepewa ahueni kubwa katika masuala ya kodi na kwamba itasaidia kutengeneza ajira kwa wingi na kuuza zaidi bidhaa kuliko kuagiza.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad