HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 3, 2023

SHAMBA LA MITI RUBARE WAIMARISHA USHIRIKIANO KATI YAO NA WANANCHI





Na Mwandishi Wetu, Kagera

*Wazungumzia vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya shamba hilo, nyumba ya kulala wageni ya kisasa

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Rubare mkoani Kagera umesema umekuwa na ushirikiano mzuri kati yao na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo hali inayofanya shamba hilo kuendelea na shughuli zake za uhifadhi pamoja na utalii Ikolojia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Miti Rubare ambaye pia ni Mhifadhi Misitu Daraja la Kwanza Jovanes Mtashaga amesema pia kupitia shamba hilo wananchi wamekuwa wakipata ajira za muda pamoja na kupatiwa miche ya miti bure kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao.

"Tunashirikiana vizuri na wananchi hasa wanaozunguka shamba la miti la Rubare , lakini wamekuwa wakiwapatia ajira za muda kama kufyeka samba , kuhudumia bustani, pia tumekuwa na mgao wa miti kila mwaka ambayo inatolewa kwa wananchi ili wapande kwenye maeneo yao.

"Jamii ya watu inayozunguka shamba hili wanayo maeneo yao ambayo wanapanda miche ya miti , hivyo tunashirikiana vizuri na wananchi katika kutunza shamba hili, pia tumekuwa tukitoa huduma saidizi kwa mfano ikitokea mgonjwa wa dharura wananchi wanapata usafiri, ikitokea ujenzi wa taasisi wakija kutuaomba tumekuwa tukiwasaidia, kwa tunashirikiana vizuri."

Akizungumzia Shamba la Miti Rubare, Kaimu huyo Mhifadhi amesema shamba hilo ni miongoni mwa mashamba 26 ya Serikali ambayo ni ya miti ya kupanda na iko chini ya TFS na shamba hilo lina ukubwa wa hekta 6734 na lina safu mbili ya Maruku na Kajungu.

" Shamba letu liko ndani ya wilaya tatu Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini na Misenyi , ndani ya shamba la Rubare tunayo hifadhi ya misitu ya asili ambayo ni maeneo oevu kwa ajili ya vyanzo vya maji, lakini pia kuna miti ya kupanda, "amesema.

Ameongeza pamoja na shughuli za upandaji miti wanazo shughuli za utaii Ikolojia kwani ndani ya shamba kuna maporomoko ya maji pamoja na pango la kihistoria ambalo linasemekana wakati wa vita ya Kagera pango hilo lilitumika katika harakati za ukombozi

"Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na vikosi vyake vya ulinzi na usalama walijihifadhi kwenye hilo pango kwa ajili ya kufanya mawasiliano na vikao kwa ajili ya mshambulia nduli Idd Amini.Hivyo tumekuwa tukipokea watalii wanaokuja kuangalia vivutio vinavyotokana na utalii Ikolojia tulionao ndani ya shamba la miti Rubare."

Kuhusu maeneo ya kupumzika ,Mtashaga amesema pamoja na shughuli nyingine wanayo Rest House Shamba la Miti Rubare ambayo ni maalum kwa ajili ya watalii ambao watapumzika na kulala na gharama zake ziko chini licha ya kuwa ya kisasa na inayovutia kutokana na mazingira yaliyopo.

"Nyumba hiyo iko kwa ajili ya wageni wanaotembelea shamba hili kwa shughuli za utalii , wakifika hapa wanapata sehemu nzuri ya kupumzika pamoja na kulala.Pia Serikali kupitia TFS iliamua kujenga Rest house hii ili wageni wanapofika ndani ya shamba waweze kujionea shughuli nzima ya uhifadhi wa mazingira yanavyofanyika ndani ya shamba la miti la Rubare

Akizungumzia maboresho , amesema wameendelea kuboresha kwa kuweka maeneo ya kupumzika na ndani ya msitu kuna ufukwe wa Kalubela ambao una mandhari nzuri na ya kuvutia.

"Upande wa Kusini shamba hili limepakana na Ziwa Victoria , kwa hiyo sehemu ya Kalubela tunaiandaa kwa ajili ya shughuli za utalii Ikolojia, tutaandaa utalii wa kasia na michezo ya ufukweni ili mtalii akitoka kutembelea kwenye maporomoko A na pango la kihistoria basi akapumzike pale ufukweni.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 ya kila mwaka Mtashaga amesema wanaendelea kuwahamasisha wananchi waendelee kuhifadhi mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji na kutokomeza taka zote za plastiki kwenye maeneo yao.

“Sisi kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kupitia shamba la miti Rubare tunaunga mkono jitihada za viongozi wetu katika kutunza mazingira kwa kutokomeza taka za plastiki , katika shamba letu la miti Rubare tunayo maeneo ya kuhifadhia taka ambazo huwa tunazitokomeza, "amesema.

Aidha ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo kutochoma moto, kwani changamoto kubwa imekuwa uchomaji moto hovyo , hivyo amewaomba wananchi kuelewa mazingira ni rafiki wa kila mwananchi

Kwa upande wao wananchi wanaozunguka shamba hilo wameipongeza TFS kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na kubwa zaidi kujenga uhusiano na ujirani mwema.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi , Sylivester Paul amesema kupitia shamba la miti Rubare wameweza kupata ajira kutokana na shughuli za uhifadhi pamoja na utalii Ikolojia lakini hata wanapohitaji msaada wamekuwa wakisaidiwa.

" Tumekuwa na ushirikiano mzuri sana kati yetu wananchi na Shamba la Miti Rubare, tunashirikiana katika kutunza shamba hili na tumekuwa tukipewa miche ya miti bure ili tukapande katika maeneo yetu.Lakini hata inapotokea changamoto tunasaidiana, "amesema Paul.


Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Rubare mkoani Kagera akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS).Nyuma yake ni nyumba ya kisasa ya kulala wageni ya Rest House Shamba la Miti Rubare ambayo imejengwa ndani ya shamba hilo kwa ajili ya watalii wanaokwenda kuangalia utalii Ikolojia iwapo watahitaji kulala hapo.











Moja ya maporomoko ya maji yaliyoko ndani ya shamba hilo ambayo yamekuwa miongoni mwa utalii Ikolojia unaopatikana katika Shamba la Miti Rubare





Mlango wa pango la kihistoria linalofahamika kwa Kyamunene ambalo linaelezwa kuwa lilitumiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalim Julius Nyerere wakati wa vita dhidi ya Nduli Idd Amini aliyekuwa Rais wa Uganda.Pango hilo lilitumika kama eneo la kufanya mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad