HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 29, 2023

MWANAMITINDO FLAVIANA MATATA AKABIDHI TAULO ZA KIKE KWA WANAFUNZI NJOMBE,AGUSWA NA CHANGAMOTO YA MIUNDOMBINU YA VYOO

 


Njombe
TAASISI ya Flaviana Matata foundation imeendeleza maadhimisho ya siku ya hedhi Duniani kwa kuendesha mafunzo kuhusu hedhi salama na elimu ya afya ya uzazi pamoja na ugawaji wa taulo za kike kwa wasichana 800 katika shule ya sekondari ya wasichana ya Manyunyu iliyopo Matembwe katika halmashauri ya wilaya ya Njombe.

Katika mafunzo hayo yaliyohusisha mijadala ya wazi kuhusu hedhi na njia sahihi za matumizi ya taulo za kike,walimu pia wamejengewa uelewa na utamaduni sahihi wa kukabiliana na hedhi kwa uwazi na kujiamini,kuondosha utamaduni na imani potofu zinazojenga hofu,usiri na uoga hali ambayo imekuwa ikiwaondolea watoto wa kike uhuru,kujiamini na wakati mwingine kulazimika kusitisha masomo yao wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi.

Licha ya hayo,mwanamitindo Flaviana Matata ameonyesha kuguswa na changamoto ya miundombinu ya vyoo pamoja na maji mashuleni ambapo ameahidi kwenda kutatua changamoto hiyo.

"Ukiacha upatikanaji wa PEDI tunajua miundombinu ndio moja ya jambo ambalo tunakwenda kutatua hapa shuleni ikiwemo kwenye vyoo,maji ili kuhakikisha msichana anapokuwa kwenye siku zake za hedhi isiwe kikwazo"Alisema Flaviana Matata

Afisa miradi wa taasisi ya Flaviana Matata Suzan Cleopas amesema zoezi hilo limeambatana na elimu ya hedhi salama.

"Tumewapatia taulo za kike watoto takribani 800 lakini pia tumewaelemisha kuhusiana na maswala ya hedhi salama na tumeweza kujua changamoto mbalimbali ambazo wanakabiliana nazo hapa shuleni pamoja na kufanya michezo"amesema Suzan

Kwa upande wake afisa elimu sekondari halmashauri ya wilaya ya Njombe Charles Meshack pamoja na Twumwimbile Lufunyo Ndelwa ambaye ni afisa elimu ya watu wazima idara ya sekondari wamesema Pedi na elimu waliyoipata wanaamini itawasaidia kujitambua pamoja na kuongeza ufaulu na kujiamini.

Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo taasisi hiyo imeainisha kutekeleza miradi endelevu katika kipindi cha mwaka 2023 - 2027 ili kuhakikisha wasichana wanapata usaidizi wa msingi ili waweze kuzifikia fursa za elimu,uwezo wa kujikimu kiuchumi,kusomesha watoto wa kike wanaotoka kwenye mazingira magumu,kuongeza upatikanaji wa miundombinu ya WASH mashuleni pamoja na kusaidia mabinti waliokatishwa masomo kwasababu mbali mbali kurejea mashuleni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad