HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 13, 2023

SERIKALI HAIJASHINDWA KULIPA MIKOPO



Na Farida Ramadhani WFM -Dodoma.

Serikali imeeleza kuwa hakuna mikopo ambayo imeshindwa kulipa katika kipindi cha Awamu zote sita za uongozi.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bunda, Mhe. Boniphace Mwita Getere aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kupata mkopo wa fedha nyingi wa muda mrefu kwa masharti nafuu ili kulipia madeni sumbufu katika Awamu zote sita (6).

Mhe. Chande alisema katika kipindi cha Awamu zote sita (6) Serikali imeendelea kukopa na kulipa mikopo kulingana na mtiririko wa malipo kwa kila mkopo na hakuna mikopo ambayo Serikali imeshindwa kulipa.

“Malipo ya madeni yote ikiwemo madeni sumbufu yanaendelea kulipwa kupitia mpango na bajeti za Serikali za kila mwaka”, alifafanua Mhe. Chande.

Alisema Serikali inaendelea kusimamia deni la Serikali kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, SURA 134 inayobainisha vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta fedha za mikopo kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli za Serikali, hususani miradi ya maendeleo.

Alibainisha kuwa Sheria hiyo pia inatumika kama nyenzo ya kudhibiti ongezeko la deni la Serikali kwa kulipa mikopo iliyoiva na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu swali bungeni, jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad