HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 14, 2023

WAZIRI MKUU: JUKUMU LA USALAMA BARABARANI NI LA KILA MTU



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa jukumu la usalama barabarani ni la kila mtu na si la Serikali pekee na amewataka wananchi wote watoe ushirikiano kuzuia ajali za barabarani.

 

“Jukumu la usalama barabarani ni la kila mmoja wetu na si la Serikali pekee. Hivyo basi, tushirikiane kupambana na kuzuia ajali za barabarani kwa kumuonya kila mmoja wetu anapovunja sheria na kanuni za usalama barabarani. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kupunguza ajali za barabarani na kuokoa maisha”.

 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 14, 2023) wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani Kitaifa uliofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza. 

 

Akiainisha makundi yanayochangia kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani, Waziri Mkuu amesema uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa mabasi yanayofanya safari ndefu ndiyo wahusika wakubwa wa ajali za barabarani.

 

“Ajali hizo kwa kiwango kikubwa husababishwa na uzembe wa madereva. Ni kwa nini basi tusifuate sheria zilizowekwa kama vile kuhakikisha kuwa kwenye mabasi hayo kuna madereva wawili watakaokuwa wanapokezana? Naliagiza Jeshi la Polisi wasimamie hili na wenye mabasi wahakikishe kuwa wanaajiri madereva zaidi,” amesema.

 

Amesema kuwa madereva wa magari na pikipiki nao wamekuwa ni sehemu kubwa ya vyanzo vya ajali za barabarani na kuchangia kuongezeka kwa ajali kwa kuendesha kwa mwendo kasi, kuyapita magari ya mbele bila ya kuchukua tahadhari, kuendesha magari mabovu ama kutoheshimu alama na michoro ya barabarani.

 

Katika kuhakikisha ushirikiano miongoni mwa wadau unakuzwa na mapambano dhidi ya ajali za barabarani yanaimarishwa, Waziri Mkuu ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani liharakishe mchakato wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwe na sheria bora isiyoacha mwanya kwa watumiaji wa barabara na waendesha vyombo vya moto.

 

Pia amelitaka Baraza hilo lifuatilie kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za udereva (points system) ili kuwaondoa madereva wanaokithiri kwa kukiuka sheria na kuwafungia kuendesha vyombo vya usafiri wale watakaoonesha usugu.

 

Kuhusu maagizo yaliyotolewa kwenye sherehe za mwaka jana mkoani Arusha, Waziri Mkuu amesema: “Harakisheni kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu kuimarisha ukaguzi wa magari kwa kuishirikisha sekta binafsi badala ya utaratibu mnaoendelea nao sasa.”

 

Mapema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jumanne Sagini alisema makosa ya kibinadamu ndiyo yanaongoza kwa kuchangia ajali nyingi za barabarani, na kwamba Baraza linaandaa mkakati ambao ni shirikishi na unaolenga kuwadhibiti madereva walevi na wanaoendesha kwa uzembe.

 

“Mkakati huo pia unalenga kudhibiti uendeshaji magari bila sifa au leseni za udereva na kutokuwa na bima, kudhibiti usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo yenye muundo wa tairi moja nyuma kama vile Noah na Probox na tutaupitia baada ya miezi sita ili kupima matokeo,” alisema.

 

Naye, Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura alisema maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani yatumike kama chachu ya kuwakumbusha Watanzania kwamba kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari awapo barabarani. ”Maadhimisho haya yanatukumbusha kuwa sote ni wahanga wa barabara, kwa hiyo tunahitaji kuchukua tahadhari za usalama tuwapo barabarani.”

 

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu kote nchini kwa sababu wanaamini kwamba kupitia elimu hiyo, wataweza kuongeza kinga ya ajali za barabarani.

 

Mbali na kutoa elimu, alisema hivi sasa jeshi hilo linafanya uhakiki wa leseni na vyeti vya madereva waliohitimu mafunzo. ”Makamanda wa Vikosi vya Usalama Barabarani wa Mikoa wameagizwa wafanye ukaguzi kwenye vyuo vyote vya udereva vinavyotoa mafunzo

ili kubaini kama bado wanastahili kuendelea kutoa elimu hiyo.”

 

Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani yalianza jana Machi 13 na yanatarajiwa kuhitimishwa Machi 19, mwaka huu. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Tanzania bila ajali za barabarani inawezekana, timiza wajibu wako.”

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad