HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, March 12, 2023

WAZIRI MKUU AWATAKA VIJANA NA WANAWAKE KUCHANGAMKIA PROGRAMU YA IMBEJU YA BENKI YA CRDB

Dar es Salaam 12 Machi 2023 – Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ametoa rai kwa vijana na wanawake kote nchini kuchangamkia programu ya uwezeshaji kiuchumi iliyozinduliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA (ICTC), na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuboresha bunifu zao za kibiashara.

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo wakati wa Semina ya Uwekezaji na Fedha ya Benki ya CRDB maarufu kama “CRDB Bank Uwekezaji Day” iliyoenda sambamba na uzinduzi wa taasisi ya hisani ya CRDB Bank Foundation, pamoja na programu hiyo ya iMBEJU ambayo inalenga kutoa mafunzo, ushauri, na mitaji wezeshi kwa vijana na wanawake.
 
Waziri Mkuu amesema programu hiyo imekuja kutoa suluhisho kamili kwa biashara changa za vijana na wanawake nchini kwa kuzijengea uwezo wa kujiendesha hususani kupitia mafunzo ya kimkakati ambayo yamepangwa kutolewa kwa kushirikiana na ICTC, COSTECH, pamoja na wadau wengine katika programu za uwezeshaji wanawake kupitia vikundi.

“Ukweli ni kuwa tatizo la kushindwa kuendelea kwa biashara changa si kukosekana kwa mitaji. Mitaji ipo na taasisi zetu za fedha zipo tayari kufadhili, lakini hatari ya uchechefu ni kubwa kwani biashara changa nyingi zimekuwa zikishindwa kujisimamia. Niwashukuru Benki ya CRDB kwa kuliona hili na kuambatanisha programu ya iMBEJU na ushauri na mafunzo,” alisema.
Waziri Mkuu aliwataka vijana na wanawake kutumia vizuri mitaji watakayopewa kwa kuwekeza katika maeneo waliyoyaainisha kupitia mipango yao ya biashara, huku akiwasisitiza kuwa waaminifu. Alizitaka pia taasisi za Serikali kutoa fursa kwa vijana waliokuja na bunifu zinazoweza kutatua changamoto za jamii, akitolea mfano wa vijana waliobuni mfumo wa kuongoza magari barabarani kupewa fursa na Wizara ya Ujenzi.

Waziri Mkuu aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuja na programu hiyo, na kusema inaendana na dira ya serikali ya kuchochea ubunifu kwa vijana na wanawake ili kutengeneza ajira, na kuchochea maendeleo nchini. Waziri Mkuu aliwahakikishia vijana kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kufanikisha bunifu zao zinakuwa na tija kwao na kwa jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema programu ya iMBEJU itakwenda Kuchochea uanzishwaji wa bidhaa na huduma mpya zinazoendana na mazingira na mahitaji halisi ya Watanzania. Nape aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kuja na bunifu zitakazoweza kushindana ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed aliwahimiza vijana na wanawake kutoka Zanzibar kuitumia fursa hiyo vizuri, huku akibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kuboresha mazingira ya kuchochea ubunifu na ukuaji wa biashara changa, na kuhakikisha programu wezeshi kama iMBEJU zinatekelezwa kwa mafanikio.

Akielezea sababu za kuanzishwa kwa programu ya iMBEJU, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Prof. Neema Mori alisema programu hiyo ni sehemu ya jitihada za Benki ya CRDB katika kuchochea maendeleo na kujenga ujumuishi wa kiuchumi kwa vijana na wanawake.
Prof. Mori alisema iMBEJU ni sehemu ya programu endelevu ambazo zitakuwa zikitekelezwa kupitia kampuni tanzu ya CRDB Bank Foundation ambayo imepewe jukumu la kubuni, kuanzisha na kusimamia miradi endelevu ya uwezeshaji katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema programu ya iMBEJU ina malengo makubwa ya kuwezesha vijana na wanawake wengi kukuza biashara zao ili kujikwamua kiuchumi wao na familia zao huku wakitoa mchango kwa Taifa kupitia kulipa kodi za biashara lakini pia kutoa ajira kwa Watanzania wengine.
Nsekela alisema pamoja na mtaji wa Shilingi bilioni 5 ambazo zimetengwa, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA na COSTECH pia itakuwa ikitoa mafunzo ya uendeshaji wa biashara. Alisema programu hiyo inalenga biashara za wanawake, pamoja na biashara changa za vijana katika sekta mbalimbali huku msisitizo ukiwekwa katika bunifu za teknolojia.

Akielezea namna ya kushiriki katika programu ya IMBEJU, Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema ili kupata mitaji wezeshi vijana na wanawake watahitajika kupitia mafunzo, na baada ya kuhitimu wataunganishwa na Akaunti ya IMBEJU na kisha kupatiwa mitaji.
“Kwa upande wa biashara changa za vijana maombi yatawasilishwa kupitia tovuti za Tume ya TEHAMA na COSTECH, kisha watapitishwa katika hatua mbalimbali za mafunzo. Wanawake wao watapitia katika matawi yetu, ambao watafanyiwa mafunzo kabla ya kupewa mitaji,” aliongezea Tully.

Akizungumza kwaniaba ya vijana ya wenye biashara changa, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa kampuni ya HACK IT, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuja na programu ya IMBEJU, huku akiwahamasisha vijana wengine kutumia fursa hiyo vizuri ili iweze kuwa na manufaa kwa vijana wengi zaidi.
Semina ya CRDB Bank Uwekezaji Day mwaka huu 2023 imehudhuriwa na washiriki zaidi ya 7,000 ambapo sehemu kubwa ni vijana ambao walishiriki kupitia mtandao kutokea pande zote za nchi, bara na visiwani. Semina hiyo ilihusisha mijadala mbalimbali ya jinsi ya kuongeza uwezeshaji kwa vijana na wanawake, na kukuza ubunifu wa kiteknolojia.














No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad