HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 13, 2023

Matumizi sahihi ya kiteknolojia yalete uwiano wa kijinsia

 

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kitaadhimisha siku ya wanawake dunia tarehe 15/3/2023 kwa kuandaa kongamano litakalojadili masuala ya matumizi sahihi ya teknolojia, changamoto na faida zake kwa wanawake na jamii kwa ujumla, sambamba na kuangalia umuhimu wa matumizi ya kiteknolojia katika taasisi za sheria ili kuharakisha upatikanaji wa haki.


Hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) uliopo Kikwajuni kuanzia saa 2:30 asubuhi ambapo itahusisha washiriki muhimu kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya kisheria, haki za binadamu, elimu na wanamtandao wa kupinga vitendo vya udhalilishaji.


Matumizi ya teknolojia kwa taasisi zinazo simamia sheria yatasaidia kurahisisha upatikanaji wa haki kwani yatawezesha kufanyika upelelezi na kukusanya ushahidi kwa njia mbalimbali, kama ilivyoelezwa katika sheria ya ushahidi Na.9 ya mwaka 2016.


Sehemu ya tatu kifungu Na. 16 cha sheria hiyo kinaeleza mbele ya Mahakama ushahidi wa kieletroniki unakubalika “Kukubali maana yake ni, maelezo ya mdomo au maandishi au yaliyomo katika mfumo wa kieletroniki, ambayo yanatoa muelekeo katika hoja inayobishaniwa au hoja inayohusika na ambayo imefanywa na watu wa aina yoyote na katika mazingira yaliyotajwa.”


Katika kifungu 42 katika mienendo ya kesi za jinai kifungu kidogo cha (a),(b)na(c) vinaelezea ushahidi wa kielotroniki, kifungu kidogo (a) kinaeleza kuwa “taarifa zilizopatikana kutoka katika mfumo wa kompyuta, mitandao au mfumo wa kuhifadhia taarifa yatakubaliwa katika ushahidi”. wakati kifungu kidogo (b) kinaeleza kuwa “kumbukumbu zilizopatikana kupitia uchunguzi kwa njia za kulinda taarifa zinazojumuisha mashine ya barua pepe, uwasilishaji wa kielektroniki,” (c) mfumo wa kurikodi matukio ya sauti au ya picha au tabia au mazungumzo ya watu walioshtakiwa, yatakubaliwa katika ushahidi.


Aidha, TAMWA ZNZ inatoa wito kwa taasisi zote zinazosimamia vitendo vya udhalilishaji kuhakikisha miundombinu inaimarishwa na kuwa ya kisasa zaidi ili kuwezesha matumizi ya kiteknolojia yatakayorahisisha upatikanai wa haki na kwa wakati. Moja ya agenda kuu ya serikali zote mbili ni suala zima la haki jinai ambalo ndio msingi mkuu wa utawala wa sheria na upatikanaji wa haki.


Matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa yatarahisisha uwajibikaji na upatikanaji haki ili kuwajengea imani wananchi.


Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wanawake duniani jamii inapaswa kuelewa umuhimu wa wanawake unaoenda sambamba na matumizi sahihi ya teknolojia yatakayoleta maendelo kwa wote na kufikia uwiano wa kijinsia na sio matumizi yatakayochangia kuendeleza udhalilishaji na ukatili.


Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi ikiwa na lengo la kutoa fursa kwa wanawake, taasisi za kiserikali na asasi za kiraia na wadau mbalimbali kupata fursa ya kukaa pamoja kujadili mafanikio na changamoto zinazomkabili mwanamke katika jamii na pia kutafakari jinsi ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.


Bado kuna changamoto nyingi zinazowaandama wanawake zikiwemo matumizi yasio sahihi ya teknolojia yanayopelekea kuendeleza vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.


Kauli mbiu ya TAMWA ZNZ mwaka huu ni “Tuhimize mtumizi sahihi ya kiteknolojia ili yalete uwiano wa kijinsia” Kauli mbiu hii inakwenda sambamba na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Wekeza Ubunifu na matumizi sahihi ya Teknolojia kwa usawa wa Kijinsia” ambapo kauli mbiu zote zinasisitiza umuhimu wa mtumizi sahihi ya teknolojia katika nyaja zote ili kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu kwa wote.


Dkt Mzuri Issa
Mkurugenzi
TAMWA –ZNZ





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad