HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 4, 2023

KTO INAUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA SEKTA ZA ELIMU, MICHEZO KWA VITENDO- BI MNIGA


SHIRIKA la Karibu Tanzania Organization (KTO,) Limepongezwa kwa jitihada na hatua wanazochukua katika kuunga mkono jitihada za Serikali hususani katika sekta za elimu na michezo ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezipa kipaumbele.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wiki mbili ya ukocha wa ngazi ya chini kwa makocha wanawake kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's) kupitia programu ya Mpira Fursa inayotolewa kwa vyuo 54 nchini; Mjumbe wa kamati tendaji ya TFF Bi. Hawa Mniga amesema KTO inaunga mkono jitihada za Serikali katika elimu kwa kuhakikisha watoto wa kike waliokatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito wanarudi shule na kupata elimu ya Sekondari na elimu ya ufundi.

"Tumeona Rais wetu anavyopambana kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora na hata wale waliokatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na hali ngumu ya maisha wanarudi shule....KTO wamelibeba hili na kulitekeleza kwa vitendo na kupitia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo kote nchini wanawake vijana wanapata masomo ya Sekondari pamoja na ujuzi wa ziada ikiwemo ufundi." Amesema.

Amesema, kupitia programu ya Mpira Fursa inayotekelezwa na KTO lengo la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ( TFF,) la kufundisha Mpira na kutoa wachezaji bora wa soka, waamuzi na walimu wa mpira wa miguu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na Shirika hilo kutoa mafunzo ya ukocha na kuongeza idadi ya makocha wanawake wanaotambuliwa na TFF kwa jitihada za KTO.

Bi. Mniga amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kutumia maarifa hayo kwa bidii ili kuweza kutoa matunda bora katika soka la wanawake Tanzania.

Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa kurugenzi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (TVET) katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Margareth Massai amesema, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's) inatambua jitihada za KTO hasa kupitia programu zake ikiwemo programu ya Elimu haina mwisho na wamekuwa wakishirikiana katika kuhakikisha watoto wa kike waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito wanarejea darasani na kuendelea na masomo yao.

" Katika kutekeleza programu ya Elimu Haina Mwisho tukaona gap katika utekelezaji KTO wakaja na wazo hili la Mpira Fursa ambalo limeleta matokeo chanya kwa kuwachangamsha, kujiamini na kuondoa mawazo potofu kwamba Wasichana hawawezi." Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO,) Maggid Mjengwa amesema kuwa Taasisi hiyo inatekeleza kwa vitendo falsafa ya ‘Mpira uchezwe kila Kona na kila Mtaa’ na kwenda sambamba na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amelipa jicho la pekee sekta hiyo ambayo imeanza kuonesha matumaini makubwa baada ya baadhi timu kushiriki mashindano kwa ngazi mbalimbali za kimataifa.

Mjengwa amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa michezo katika kuhakikisha mpango mkakati wa ushiriki wa Taifa katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo ya kombe la dunia 2030 unafikiwa kwa mafanikio makubwa na hiyo ni pamoja na kuendelea kunoa vipaji kuanzia ngazi ya chini.

Akieleza kuhusu programu ya Mpira Fursa Mkurugenzi wa programu wa KTO Bi. Mia Bergdahl Mjengwa amesema programu hiyo imelenga kuendeleza soka la wanawake na Wasichana nchini na ilianzishwa na KTO kwa kushirikiana na TFF na inaendeshwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI,) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC's) vilivyopo kote nchini.

Amesema, mafunzo hayo kwa makocha wa ngazi ya chini kutoka vyuo hivyo kwa wiki mbili chini ya wakufunzi wa TFF itasaidia kufikia timu zipatazo 216 za soka za Wasichana ambazo zitaanzishwa katika shule za Msingi 54 katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54.

"Pia kupitia programu hii tunataraji wanawake vijana na Wasichana 10,000 wa Shule za Msingi na FDC's watakuwa wanacheza soka, pia timu 108 za msingi na FDC's 54 katika mikoa 24 zinashiriki kikamilifu katika soka la wanawake zikiwa na timu zake kutoka kila chuo.... kupitia mafunzo haya ya Ukocha wa ngazi ya chini tunatarajia mapinduzi makubwa katika soka la wanawake Tanzania." Amesema .

Mia amesema programu hiyo inasaidia vijana na wanawake katika kujiamini, kujithamini pamoja na kupata fursa za ajira ndani na nje ya Nchi.

"Kupitia programu hii Wasichana na wanawake vijana wananufaika kwa kujifunza na kuwa wachezaji soka, kuwawezesha kutambua haki zao za msingi na kuleta usawa wa kijinsia katika jamii, kupenda shule, kuburudika, kujenga afya na kujiamini na kuondoa dhana potofu ya kwamba Wasichana hawawezi." Ameeleza.

Akizungumza kwa niaba ya ya washiriki wa mafunzo hayo Consolatha Luhende kutoka Malya FDC Mwanza amesema, kwa wiki mbili wamepata mafunzo ambayo yatawasaidia kujenga na kuendeleza soka nchini kuanzia ngazi ya chini wakiwa walezi.

"Tumejifunza mbinu za kufahamu tabia za watoto kuanzia miaka 4 hadi 12 kwa kuzingatia tabia na mahitaji, tiba za michezo, kuwalinda pamoja na kuwakinga watoto dhidi ya Ajali." Amesema.

Aidha amesema, kupitia mafunzo hayo suala la usalama, kukagua uwanja pamoja na kuwajengea ari ya kupenda soka wanafunzi kuanzia ngazi ya chini litazingatiwa zaidi ili kujenga kizazi bunifu kitakachonufaika na fursa ya ajira kupitia Mpira wa miguu ndani na nje ya Nchi.

Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo na kueleza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika sekta ya Elimu na kunoa vipaji kuanzia ngazi ya chini.



Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wakipokea vyeti kutoka kwa Mjumbe wa kamati tendaji ya TFF Bi. Hawa Mniga.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad