HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, March 26, 2023

KAPOMBE, ZIMBWE WAITWA TAIFA STARS

 


Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KOCHA  Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Adel Amrouche amewaita kwenye Kikosi cha timu hiyo, Walinzi wawili wa pembeni wa Simba SC, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein (Zimbwe Jr) ambao aliwaacha katika safari ya Misri kwenye mchezo dhidi ya Uganda (The Cranes).

Katika Kikosi cha Wachezaji 31 walioitwa awali, kuelekea kwenye mchezo huo wa kuwania kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), Kocha Adel aliwaacha Walinzi hao licha ya kukutana nao na kuteta nao baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Horoya AC kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amesema Kocha Adel amewajumuisha Wachezaji hao kwenye Kikosi hicho cha Stars ambacho kinatarajiwa kucheza mchezo wa nne wa Kundi F la kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Uganda, Machi 28, 2023 kwenye dimba la Mkapa.

“Shomari Kapombe na Mohammed Hussein, kwa sasa watakuwa wamejumuika na wenzao kambini kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Uganda siku ya Jumamne (Machi 28, 2023) kwenye uwanja nyumbani, Benjamin Mkapa,” amesema Wallace Karia

“Mwalimu tulikuwa naye siku nyingi (miezi miwili nyuma) alikuwa anakuja kuangalia Ligi Kuu hapa nyumbani, kwa ajili ya kusaka vipaji kwa ajili ya kuunda Kikosi cha timu ya taifa, na alipokuja alipewa orodha ya Wachezaji na Wasaidizi wa timu (Taifa Stars),” ameeleza Karia

Hata hivyo, Rais Karia ameeleza kuwa maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika na timu ipo tayari kwa ajili ya mchezo, amesema licha ya kukabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Uganda ambao ni washindani wakubwa wa Taifa Stars, ameeleza kujipanga vizuri kwa Kikosi hicho ili kujihakikishia mazingira mazuri ya kufuzu AFCON.

Mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye dimba la Suez Canal, Ismailia nchini Misri, Taifa Stars ilishinda bao 1-0 dhidi ya Uganda waliokuwa nyumbani, bao hilo lilifungwa na Mshambuliaji Simon Msuva kwenye dakika ya 68’ na hivyo kufikisha alama nne na kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi F lenye timu za taifa za Algeria, Uganda na Niger.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad