HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 15, 2023

UKUTA WA MIRERANI UMEONGEZA USALAMA WA MADINI YA TANZANITE

 

Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, Vitus Ndakize.

Joseph Lyimo, Mirerani
UKUTA unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, umekuwa faraja kwa wachimbaji kwani hivi sasa matukio ya wizi na uporaji yamekomeshwa kutokana na kuwepo kwa lango moja la kuingia na kutokea.

Ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 25 na kwenda juu urefu wa mita 3.5 uliotumia gharama ya sh6 bilioni, ulichimbwa na wanajeshi 271 mwaka 2018.

Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Franone Mining and Gems Ltd, Vitus Ndakize akizungunza na waandishi wa habari amesema ukuta huo umekuwa na manufaa makubwa kwa wachimbaji madini ya Tanzanite.

"Tangu kujengwa kwa ukuta wa Mirerani kumekuwepo na mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama kwenye shughuli za uchimbaji, biashara na usafirishaji wa madini sambamba na kupungua kwa vitendo vya wizi kwenye migodi," amesema.

Ametaja mabadiliko mengine ni kupungua kwa gharama za uendeshaji kwani huduma zote za uthaminishaji na masoko ya madini zinapatikana ndani ya eneo la Mirerani.

“Kabla ya ujenzi wa ukuta huu, wachimbaji wa madini walikuwa wanahangaika na kutafuta masoko ya kuuzia madini yao, hali ambayo ilikuwa ni hatari, wakati mwingine walikuwa wakiuza kwa bei ndogo kutokana na kutokujua thamani halisi ya madini ila ulipojengwa ukuta, madini yanathaminishwa na wataalam wa Tume ya Madini, kuuzwa kwa bei halisi huku Serikali ikipata kodi na tozo mbalimbali,” amesema Ndakize.

Ofisa madini mkazi wa Mirerani, mhandisi Menard Msengi amesema kuwepo ukuta huo kumekomesha utoroshaji wa madini ya Tanzanite na kusababisha Serikali kupata kodi zake na tozo.

Msengi amesema kutokana na ukuta huo hivi sasa madini yanadhibitiwa na watumishi wa Tume ya madini na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mwenyekiti wa wanawake wa magonga Mirerani Tanzanite (MIWOTAMA), Joyce Mkilanya amesema katika lango la ukuta kumekuwepo na maboresho eneo la ukaguzi ambapo watu wamekuwa wakikaguliwa kwa kuzingatia utu na heshima.

Mkilanya amepongeza kuwa upekuzi wa stara na ukuta wa Mirerani umesababisha kuimarika kwa usalama na kupungua kwa vitendo utoroshaji wa madini tofauti na awali kabla ya kujengwa kwake.

"Wadau wa madini, ya Tanzanite, wachimbaji, wafanyabiashara na wanaoendesha shughuli zao ndani ya ukuta wa Mirerani, tunaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini, Tume ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na usimamizi mzuri wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ndani ya ukuta huu,"

Hata hivyo, amesema katika kuiunga mkono serikali kuisaidia jamii kikundi chao cha MIWOTAMA kimetoa sh4 milioni ya kujenga maabara ya shule ya sekondari Tanzanite ya kata ya Mirerani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad