HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 23, 2023

TANZANIA NA UFARASA WASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO YA USAFIRI WA ANGA

 Serikali ya Tanzania imeingia mkataba wa makubaliano ya Usafiri wa Anga na serikali ya Ufaransa wakati wa Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya  yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo Tarehe 23 Februari 2023. 

Makubaliano hayo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ambapo amesema makubaliano hayo yataleta tija hasa kwenye biashara kati ya Tanzania na nchi za Ulaya kupitia nchi ya Ufaransa kwa kutumia Shirika la ndege la Ufaransa kuanza safari za kuja nchini Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema mkutano huu ni mkubwa na wenye tija kwa Taifa letu  hasa kwenye sekta ya Anga kwa kuweza kusaini makubaliano ya Usafiri wa Anga kati ya Nchi ya Tanzania na nchi ya Ufaransa.

Amesema mkataba huu ni muhimu sana kwasababu mkataba uliokuwepo ulisainiwa mwaka 1978 hivyo kuanzia mwaka huo mpaka sasa kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana kwenye sekta ya usafiri wa Anga hivyo kuanzia mwaka jana wataalamu wa Tanzania waliweza kukaa pamoja na wataalamu kutoka Ufaransa ili kupitia mkataba huo ambapo umeweza kuleta mafanikio kwenye mkataba huu mpya.

"Mkataba huu utaweza kutoa fursa nyingi sana kwa sekta ya Anga  kati ya Tanzania na Ufaransa kwa kuweza kuongeza watalii wengi zaidi wa kuja kutembelea nchi yetu wakitokea nchi mbalimbali za Ulaya pamoja na nchi nyingine kwa kupitia nchi ya Ufaransa." Alisema Mbarawa

Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga amesema kupitia mkataba huo utaleta biashara ya mizigo kati ya Tanzania na Ufaransa pamoja na kuwepo viwanja vya ndege vya kutua vitano mpaka sasa nchini Ufaransa.

Amesema kutokana na kusaini mkataba huu hivyo Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania ni kuwezesha usafiri wa Anga kati ya nchi na nchi unaimarika na hii kitu ni muhimu kwa ukuaji wa Sekta ya Usafiri hapa Nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akishuhudia utiaji Saini wa Mikataba makubaliano baina ya Tanzania na Wawekezaji kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wakati akifungua Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 23 Februari 2023. Kulia ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa na Kushoto ni Waziri wa Uchumi na Biashara za Kimataifa wa Ufaransa Olivier Becht .
Mkutano wa Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ukiendelea 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari mara baada kusaini mkataba wa makubaliano ya Usafiri wa Anga na serikali ya Ufaransa wakati wa Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya  yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 23 Februari 2023. 
Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa kusaini mkataba wa makubaliano ya Usafiri wa Anga na serikali ya Ufaransa wakati wa Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya  yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 23 Februari 2023.  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad