HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 14, 2023

SIMBA SC: KAULI YA RAIS KWETU NI AGIZO

 

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wanachukulia kauli ya Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kama agizo kwao baada ya kuahidiwa kiasi cha Tsh. Milioni 5/- kwa kila goli litakalofungwa na Klabu hiyo dhidi ya Raja AC.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Ahmed Ally amesema kauli hiyo kutoka kwa Dkt. Samia maana yake anataka kuona magoli mengi yanafungwa na timu za ndani ya nchi na timu hizo zinapata ushindi katika michezo ya Kimataifa wikiendi hii.

“Sisi Simba SC kauli ya Mhe. Rais Samia tunaichukulia kama agizo kwetu, kuahidi kutoa kiasi cha fedha, Tsh. Milioni 5/- kila goli, hiyo ni kama motisha tu, lakini kauli hiyo kwetu tunachukulia agizo na tutatekeleza agizo hilo la Mhe. Rais, Jumamosi ya Februari 18, 2023 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja,” amesema Ahmed Ally

Hata hivyo, Ahmed Ally amesema Wachezaji wa Simba SC wamesikia kauli hiyo ya Rais Samia na watakata kumfurahisha Mheshimiwa katika mchezo huo kwa kumfunga mabao mengi mgeni kutoka nchini Morocco, Raja Casablanca kwenye dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, Ahmed Ally amethibitisha watamkosa Kiungo wao, Sadio Kanoute katika mchezo huo dhidi ya Raja AC, Kanoute ana idadi ya Kadi tatu za njano ambazo alizipata kwenye michezo mitatu tofauti, huku akithibitisha kurejea kwa Mshambuliaji wao Sadio Ntibazonkiza katika mchezo huo, na huenda akawepo Winga wa timu hiyo, Peter Banda endapo jopo la Madaktari litathibitisha uwepo wake.

Kuhusu muda wa mchezo huo, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limepanga mchezo kuchezwa saa 1 kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, Ahmed amesema tayari wameandika barua kwenda kwa Shirikisho hilo kuomba mchezo huo kuchezwa majira ya saa 10 kamili alasiri, hata hivyo wanasubiri majibu kuhusu ombi lao.

Aidha, Rais wa Heshima wa Klabu hiyo, Mohammed Dewji (MO Dewji) ameiomba Menejimenti ya Klabu kupunguza viingilio vya mchezo huo ili kutoa fursa kwa Mashabiki kuhudhuria zaidi na kutoa hamasa kwa timu hiyo ili ifanye vizuri zaidi kwenye mchezo huo muhimu kwao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad