HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 10, 2023

LSF YAKUTANA NA MASHIRIKA MAPYA YATAKAYOPOKEA RUZUKU YA USIMAMIZI UPATIKANAJI WA HAKI

 Meneja Programu wa Legal Services Facility (LSF), Wakili Deogratias Bwire.


SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) limefanya kikao kazi cha pamoja na mashirika (Zonal Mentors Organizations – ZMOs) yatakayosimamia mashirika takribani 92 ya wasaidizi wa kisheria katika kanda sita nchini ili kuongeza ubora,uwezo, na maendeleo ya kitaasisi katika kutoa huduma za msaada wa kisheria katika jamii.

Kikao hicho cha siku mbili kinalenga kupitia maandiko mradi (proposals), mipango kazi (workplans) pamoja na bajeti za mashirika simamizi (ZMOs) kwa ajili ya kuangalia upya shughuli mbalimbali zilizopangwa ikiwa zinaakisi malengo ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki nchini kupitia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho, Meneja Programu LSF, Wakili Deogratias Bwire, amesema kuwa kikao kinalenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa watendaji wa mashirika simamizi (ZMOs) kwa ajili ya kuonyesha uelekeo mzuri wa utekelezaji programu ya upatikanaji haki nchini,kuleta matokeo tarajiwa kulingana na miongozo ya LSF ikiwemo mpango mkakati wa miaka mitano pamoja na mpango wa taifa wa maendeleo.

“Kikao hiki kinafanyika ili kukidhi mahitaji ya mabadiliko ya mfumo wa utekelezaji wa program yetu ya upatikanaji wa haki nchini hasa katika utoaji wa ruzuku’alisema Mwire.

Awali,LSF ilikuwa na mfumo wa kutoa ruzuku kwa mashirika ya wasaidizi wa kisheria kupitia mashirika simamizi katika mikoa(Regional Mentors Organizations – RMOs), kisha baadae iliamua kutoa ruzuku moja kwa moja(direct funding modality). Sasa tumeamua kuwa na usimamizi wa kikanda ili kuongeza ufanisi Zaidi.

Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi na Matokeo LSF, Said Chitung amesema kuwa kikao hicho kinalenga kuongeza usimamizi wa programu kwa kujenga uwezo kwa mashirika ya msaada wa kisheria ambayo ZMOs watayasimamia katika kanda zao.

“ZMOs hawa kazi yao kubwa ni kufanya usimamizi wa programu ya LSF katika mikoa mbalimbali ambayo watakwenda kuisimamia kulingana na kanda zao tulizowapa.Tunategemea mfumo

huu utupe matokeo makubwa zaidi mwisho wa programu yetu kama tulivyokubaliana katika kikao hiki muhimu,” amesema Chitung.

Naye Afisa fedha kutoka Shirika la Morogoro Paralegal Centre (MPLC), Regina Solomon ameeleza kuwa kikao kimesaidia kujenga uelewa wa pamoja katika utoaji wa taarifa (reporting) zenye matokeo kuhusu utekelezaji wa mradi katika maeneo ambayo ZMOs atakwenda kuyasimamia chini ya ufadhili wa Legal Services Facility.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Centre for Widows and Children Assistance (CWCA), Wakili Jane Kapufi amesema taasisi yake ambayo imechaguliwa kusimamia (ZMO) mikoa ya Mara,Mwanza, Simiyu na Shinyanga watahakikisha mashirika ya msaada wa kisheria yanakuwa haizaidi kiutendaji kwa kuendelea kuyajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya utoaji wahuduma za msaada wa kisheria ikiwemo kutoa mafunzo ya sheria ambazo zimekuwa na tabia yakubadilika kila wakati.

Kikao kazi hicho cha pamoja kimeandaliwa na LSF kwa siku mbili kuanzia 09-10 Februari 2023 Jijini Dar es Salaam, ambapo mashirika simamizi (ZMOs), waratibu wa kanda wa programu na usimamizi wa ruzuku LSF (LSF zonal Coordinators) kwa pamoja watashirikiana na secretarieti ya LSF kujenga uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa programu ya upatikanaji wa haki kupitia usimamizi wa kanda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad