HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 15, 2022

WAZIRI BASHUNGWA AJIVUNIA KUONGEZEKA UZALISHAJI MAZAO SHIRIKA LA MZINGA

 





WAZIRI wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb) amesema kuwa anajivunia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la msingi katika Shirika la Mzinga. Ameyasema hayo leo tarehe 13 Disemba, 2022, alipofanya ziara ya kutembelea Shirika hilo.

Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na Mheshimiwa Bashungwa katika Shirika la Mzinga kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo ambalo ni moja ya mashirika chini ya Wizara yake, tangu ateuliwe na kuapishwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT tarehe 03 Oktoba, 2022.

Akiwa katika Shirika hilo. alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea shughuli zinazoendelea, ambapo aliweza kupatiwa maelezo ya kina kuhusu maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika kuzalisha mazao ya msingi, kuangalia matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano (2017/18 – 2021/22), mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mipango waliyojiwekea.

Maeneo aliyoyatembelea ni pamoja na Kiwanda kinachozalisha mazao mbalimbali, ya msingi na mbadala, karakana, kuangalia maboresho ya hospitali ya Shirika yenye hadhi ya Wilaya pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Baadhi ya mafanikio ya Shirika ni pamoja na utengenezaji wa risasi za kuwindia wanyama, kuendelea kuagiza na kuuza silaha zenye kaliba ndogo, kuendelea kutekeleza miradi ya ujenzi kupitia Kampuni Tanzu ya Mzinga Holding Company Limited, kukamilika kwa nyumba ya kulala wageni Magadu Hotel pamoja na maboresho ya Hospitali ya Shirika na Mzinga Vocational Training Centre (MVTC).

Akitoa taarifa ya Shirika kwa Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu, Brigedia Seif Hamis alisema Kuwa Shirika la Mzinga lilianzishwa rasmi mwaka 1971, ukiwa ni mradi kwa ajili ya kuzalisha mazao kwa matumizi ya JWTZ. Na ilipofiika tarehe 13 Septemba, 1974 mradi huu ulibadilishwa na kuwa Shirika la Umma (Public Corporation) chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT kwa Tamko la Serikali Na. 219.

Aidha, Brigedia Jenerali Hamis aliongeza kusema kuwa Shirika la Mzinga kisheria linao wajibu wa kuzalisha mazao ya msingi na mitambo, kufanya tafiti mbalimbali, kukarabati vifaa na mitambo mbalimbali na kutekeleza majukumu yote muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Shirika la Mzinga linajishughulisha na shughuli kuu mbili, kwanza, ni shughuli za kuzalisha mazao ya msingi ya mwaka 1971 na yale mazao yaliyoongezwa mwaka 2012 ambapo uzalishaji wake umeongezeka kutoka asilimia 11 hadi kufikia asilimia 87 mwaka 2022. Pili, Shirika pia, linajishughulisha na shughuli za uzalishaji mazao mbadala ili kujiongezea kipato kwa lengo la kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini.

Shirika la Mzinga lilianzishwa mnamo mwaka 1971 kama mradi wa mazao ya msingi chini ya Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kuzalisha mazao kwa matumizi ya JWTZ. Ilipofika tarehe13 Septemba, 1974 mradi huu ulifanywa kuwa Shirika la Umma (Public Corporation) kwa Tamko la Serikali Na. 219.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad