HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 1, 2022

Watoto 22 wafanyiwa upasuaji wa moyo ndani ya siku sita

 


Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
30/11/2022 Watoto 22 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.

Kambi hiyo ya siku sita ilifanywa na wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel.

Katika kambi hiyo mtoto mdogo aliyefanyiwa upasuaji alikuwa na umri wa mwezi mmoja na wiki mojo huku mkubwa akiwa na umri wa miaka 12, hali za watoto zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema mtoto mdogo aliyefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo alizaliwa mishipa yake ya damu ya moyo ikiwa imejigeuza hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji wa kuirekebisha.

“Mtoto huyu mwenye umri mdogo mbali na kurekebishiwa mishipa ya damu alihitaji pia kutengenezewa tundu kubwa kwenye moyo kuleta mchanganyiko mzuri zaidi wa damu ili aweze kupata unafuu kama sehemu ya kumuandaa kwa ajili ya matibabu makubwa zaidi ya upasuaji wa moyo,” alisema Dkt. Stella.

Dkt. Stella alisema katika kambi hiyo watoto 13 walizibwa matundu yaliyokuwa katikati ya mishipa mikubwa miwili ya moyo (Patent Ductus Arteriosus - PDA) na wengine tisa walikuwa na matundu katikati ya vyumba mbalimbali vya moyo ambapo matundu hayo yamezibwa.

“Ushirikiano wa JKCI na Shirika la Save a Child’s Heart ni ushirikiano ambao umesaidia kuwasomesha wataalam wa kada mbalimbali wa magonjwa ya moyo kwa watoto pamoja na kuhakikisha wanabadilishana uzoefu nasi kuhakikisha tunaendeleza ujuzi wetu,”.

“Miaka ya mwanzoni wamekuwa wakifanya upasuaji pamoja na sisi lakini katika siku za hivi karibuni hasa awamu hii wamekuwa ni wasimamizi wa kuangalia nini tunafanya na kutoa ushauri pale ambapo unahitajika, kwa hakika haya ni maendeleo makubwa,” alisema Dkt. Stella.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Save a Child’s Heart Simon Fisher alisema anaamini kila watalam wa shirika hilo wanapokuja JKCI wataalam wa JKCI wanapata nafasi ya kupanda angalu hatua moja katika kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa watoto.

“Tumeshuhudia maendeleo makubwa kutoka kwa wataalam wa hapa JKCI kwani mara nyingi tulivyokuwa tunakuja tulikua tukidhamiria kufanya upasuaji kwa watoto wengi kwa kipindi kifupi lakini kipindi hiki tulilenga kufundisha zaidi kuliko kufanya matibabu kwa watoto wengi,” alisema Simon.

Simon alisema Ushirikiano wa shirika la Save a Childs Heart unazidi kuendelea sio tu kwa mafunzo na kwa kufika JKCI kwa ajili ya matibabu pia ni miongoni mwa mashirika machache hapa duniani ambalo limekuwa likichukua watoto kutoka Tanzania bara na Visiwani na kuwapeleka nchini Israel kwa ajili ya matibabu mbalimbali hasa ya upasuaji wa moyo.

“Ushirikiano wa shirika letu na Tanzania umekuwepo kwa zaidi ya miaka 20, kwa sasa hivi tumepunguza kwa asilimia zaidi ya 90 kuwapeleka watoto Israel kwa ajili ya matibabu kwasababu tayari kituo cha kutoa huduma hizo kipo hapa Tanzania na wataalam wake wanaendelea siku hadi siku kuwa mabingwa wabobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto,” alisema Simon.

Naye mama ambaye mtoto wake alifanyiwa upasuaji katika kambi hiyo Josephina Emmanuel kutoka mkoani Kigoma alisema mtoto wake alikuwa na matundu mawili kwenye moyo ambapo tatizo hilo liligundulika mtoto akiwa na umri wa miezi mitatu na kuanza kupatiwa matibabu.

“Nawashukuru sana madaktari ambao wamemfanyia upasuaji mwanangu maana mwanzoni mtoto alitibiwa kwa dawa watalaam wakasema huenda matundu hayo yangejifunga lakini kwa bahati mbaya tundu moja tu ndio lilifunga na lililobaki leo hii wataalamu wamemfanyia upasuaji na kulifunga na nimeambiwa sasa mtoto kapona kabisa,”.

“Niliambiwa gharama za matibabu ni shilingi milioni nne laki mbili na elfu sitini lakini kutokana na hali yangu nimepata msamaha wa matibabu na kulipia shilingi laki moja tu na kupatiwa matibabu haya kwakweli nawashukuru sana watalaam hawa maana sisi watu wa hali ya chini sijui tungewezaje kupata hizi huduma kama Taasisi hii isingekuwepo hapa nchini kwetu,” alisema Josephina.

Watoto hao walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo.

Wataalam wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel wakifanya upasuaji wa bila kufunua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kuziba tundu la moyo wa mtoto katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku sita iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi hiyo ambapo jumla ya watoto 22 walifanyiwa upasuaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad