HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 5, 2022

WAHANDISI WASIOWAJIBIKA KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU NA KISHERIA

 

Na Benny Mwaipaja, Singida
SERIKALI inakusudia kuanza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria wahandisi wa Serikali wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutosimamia kikamilifu miradi inayoibuliwa na kutekelezwa na wananchi maeneo mbalimbali nchini lakini wamekuwa wakikatishwa tamaa wananchi baada ya kukamilisha miradi hiyo kwa madai kuwa haijakidhi viwango.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, baada ya kukagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Mukulu na kuelezwa kuwa moja ya jengo la utawala lililojengwa kwa nguvu za wananchi, ujenzi wake ulizuiwa kwa madai kuwa haukufuata taratibu za ujenzi na ramani inayotakiwa.

Dkt. Nchemba alisema kuwa hali hiyo inaonesha namna wahandisi hao katika ngazi za TAMISEMI, wanavyoshindwa kuwajibika ipasavyo wakati wanalipwa mishahara na Serikali kila mwezi kwa ajili ya kufuatilia na kukagua ujenzi wa aina yoyote unaoendelea katika maeneo yao lakini hawafanyi hivyo na kuisababishia serikali na wananchi hasara.

"Jambo hili halikubaliki na linatia aibu. nitawasiliana na Waziri mwenzangu wa TAMISEMI (Mhe. Angela Kairuki) ili tuweke pendekezo ikitokea wilaya yoyote au halmashauri yoyote likajengwa jengo likaonekana halifai huyo mhandisi atakuwa amejifukuzisha kazi" alisema Dkt. Nchemba


Dkt. Nchemba alisema kuwa kutowajibika ipasavyo kwa wataalam hao kunakwaza jitihada za wananchi za kujiletea maendeleo kwasababu walipaswa kuwaongoza kikamilifu wananchi wanaojenga miundombinu mbalimbali kuanzia hatua za awali badala ya kuwaacha wakamilishe miradi husika na kuwakataza ama kuwazuia kuendelea na ujenzi husika.


Diwani wa Kata ya Makulu, Stephen Apolo, alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo la utawala katika shule ya Sekondari Kizaga umesimama muda mrefu ukisubiri mwongozo mwingine kutoka kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya elimu katika wilaya hiyo ya Iramba.


Mapema, Dkt. Mwigulu Nchemba alitembelea na kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari Kizaga ambapo mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi. Emerensiana Luena na baadae akafanyaziara ya aina hiyo katika Shule ya Sekondari Mukulu ambapo Mkuu wa Shule ya Sekondari hiyo Bi. Magreth Yusufu, walitoa taarifa ya maendeleo ya mradi na namna shilingi milioni 40 ambazo kila shule ilipatiwa na Serikali kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa zilivyotumika.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali imepanga kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa mengine elfu kumi na sita nchi nzima katika Bajeti ya Mwaka huu wa fedha baada ya kujenga mengine elfu 15 mwaka wa fedha uliopita baada ya kupata maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua mabayo itapunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa nchini.


Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi Mkoani Singida ambapo anakagua ujenzi wa miradi ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya elimu, maji, barabara na afya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad