HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 9, 2022

Wadau wa sekta ya habari Z’bar wataka ushirikishwaji zaidi utungwaji wa Sheria

 WADAU kutoka Asasi mbali mbali za kiraia na zile za Serikali wameona kuna haja ya ushirikishwaji kikamilifu kwa waandishi wa habari katika michakato ya uundwaji ama urekebishwaji wa sheria mbali mbali zinazohusu hapa nchini.

 

Wameyasema hayo katika ukumbi wa Chama hicho Tunguu Wilaya ya kati mkoa wa kusini Unguja walipokua wakizungumza na wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za kiserikali  katika mkutano wa siku moja uliokuwa na lengo la kuzipitia  na kutoa maoni yao kwa baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya Tume ya Uchaguzi, sheria ya habari na sheria ya Takwimu Zanzibar.

 

Wamesema kuna baadhi ya sheria zinazonekana kuleta mkanganyika katika utekelezaji wake huku baadhi ya sheria hizo zikionekana kuminya uhuru wa habari na waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa maslahi ya mapana zaidi.

 

‘’Ili kuepuka haya ni vyema sisi waandishi wa habari tukashirikishwa kikamilifu tangu hatua za awali kwenye uundwaji wa sheria ili kutoa maoni yetu pale tunapoona hapatakua sawa hususani katika utendaji wetu wa kazi’’wamesisitiza.

 

Awali mwanahabari  mwandamizi Zanzibar Salim Said Salim alisema kuna baadhi ya sheria ni za ajabu sana, alitolea mfano kipengele cha sheria ya Uchaguzi kinachomkataza mwandishi wa habari kutojumuisha matokeo ya uchaguzi yaliobandikwa ukutani katika vituo vya kupigia kura, matokeo ambayo tayari yamewekwa kwa ajili ya umma na maafisa wenyewe wa tume hiyo.

 

Alisema kipengele hicho cha sheria kinakiuka uhuru wa habari na kuwanyima tarifa wananchi na kueleza kuwa kuna haja ya kufanyiwa marekebisho ya haraka  ili waandishi wa habari waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.

 

‘’Kwa kuwa maafisa wenyewe wa tume ya uchaguzi ndio waliojumlisha na kubandika matokeo ya kura kwenye vituo vya kupigia kura huku karatasi hizo zikiwa tayari zimetiwa saini za wahusika kwanini mwaandishi wa habari azuiwe keshiria kufanya kazi yake ya kutoa taarifa hizo za  idadi ya kura husika kutoka kwenye vituo’’alihoji mwanahabari huyo.

 

Akichangia katika mkutano huo mwandishi wa habari kutoka shirika la magazeti ya Serikali Tanzania Bara (TSN) Issa Yussuf alisema kuna haja kubwa ya wanaohusika uandaaji na urekebishaji wa sheria kuratibu mpango mzima wa awali wa kukusanya maoni ya wananchi  kabla ya kufikisha miswaada katika Baraza la Wawakilishi, ukizingatia kwamba wananchi ndio walengwa wakubwa wa sheria zinazotungwa hivyo ni wajibu wao kutoa maoni yao na kuzingatiwa.

 

Nae mratib wa Baraza la Habari Tanzania MCT Shifaa Said Hassan alisema kuwepo kwa sheria bora katika nchi zitasaidia kuleta usawa na demokrasia, sambamba na hilo alisisitiza umuhimu wa kufuata na kutekeleza kwa vitendo mikataba ya Kikanda na Kimataifa ambayo nchi imeridhia ni jambo la msingi na linalopaswa kutiliwa mkazo zaidi.

 

Wadau hao wamekutana katika mkutano wa siku moja ulioandaliwa  na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Internews Tanzania uliokua na lengo la kupitia baadhi ya sheria Zanzibar na kutoa maoni yao  juu ya yale wanayoona yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

Wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali na kiraia wakionesha kuunga mkono kwa pamoja maadhimio ya mkutano huo.

Mwandishi wa habari mwandamizi Zanzibar Salim Said Salim akichangia katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad