HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 3, 2022

POLISI YAONYA TOHARA KWA WATOTO WA KIKE

 

Na Makao Makuu ya Polisi- Dodoma.
JESHI la Polisi nchini limejipanga katika kudhibiti shughuli za tohara kwa watoto wa kike hususani katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ambapo baadhi ya watu hapa nchini wameanza kuhamasisha vitendo hivyo ambavyo vinaambatana na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto.

Hayo yalisemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma.

Misime alisema Jeshi hilo limebaini njia mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kuandaa tohara hizo ambapo katika Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya mzee mmoja amebainika kuandaa kadi za mialiko kuhamasisha shughuli za tohara kwa watoto wa kike jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu.

Alisema Jeshi la Polisi limeanza kuwakamata watu hao wanaohamasisha shughuli za tohara kwa watoto wa kike zinazokiuka sheria za nchi na ukiukwaji wa haki za binaadamu kama vile ukeketaji.

“Tunatoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, wenyeviti wa vitongoji, mtaa, vijiji, watendaji wa mitaa, vijiji na kata na wananchi wema kuwa macho katika maeneo yao na kutokuruhusu vitendo hivyo vikiwepo vya ukeketaji kufanyika katika maeneo yao na pia watoe taarifa polisi wanapoona maandalizi au vitendo hivyo vikifanyika” Alisema Misime.

Katika hatua nyingine, Misime ameonya vitendo vya watu kukiuka sheria za nchi ikiwemo utapeli kwa kigezo cha kutafuta fedha za kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo amesema Jeshi hilo litawashughulikiwa kwa mujibu wa sheria bila kujali nafasi zao katika jamii.

Pia Misime alisema Jeshi la Polisi, limeanza kuchukua hatua kali zaidi za kuimarisha doria za barabarani ili kuwadhibiti watumiaji barabara ambao kwa makusudi wanavunja sheria za usalama barabarani na kupelekea ajali zinazoleta madhara kwa watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad