HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 15, 2022

NDEJEMBI AKEMEA TABIA YA WIZI KWA WATUMISHI INAYOKINZANA NA DHAMIRA YA RAIS DKT. SAMIA YA KUJENGA UADILIFU

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala (hawapo pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika Halmashauri hiyo ya Jiji.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya kuzungumza na watumishi wa Wilaya ya Ilala (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Wilaya ya Ilala (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika wilaya hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Jiji la Ilala wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (aliyekaa meza kuu katikati), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo ya Jiji.
Na. Veronica E. Mwafisi-Ilala
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma nchini kujihusisha na vitendo vya wizi ambavyo vinakwenda kinyume na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ndejembi amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maono makubwa ya kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu, hivyo amewataka watumishi wa umma nchini kutokumuangusha badala yake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa katika kulitumikia taifa.

“Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua wazi kututhamini watumishi wa umma kwa kuboresha maslahi na stahili zetu hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuunga mkono kwa vitendo dhamira yake ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kutafakari madhara ya wizi na kutathmini mienendo yao ili kutokuwa ni sehemu ya kukwamisha dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma kwa wananchi na kuliletea taifa maendeleo katika sekta zote muhimu kama vile afya, kilimo, uvuvi, biashara, uwekezaji na miundombinu.

Sanjari na hilo, Mhe, Ndejembi amewataka Waajiri na Maafisa Utumishi Serikalini kuwasimamia vema watumishi wanaowaongoza badala ya kusubiria mpaka viongozi wa juu wa kitaifa kufika katika maeneo yao ya kazi kukemea uovu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

Akizungumzia matumizi ya fedha za umma, Mhe. Ndejembi amesema kuwa fedha za umma zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali kwani kinyume na hilo ni ukosefu wa maadili katika Utumishi wa Umma.

Mhe Ndejembi ameeleza bayana kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haitomvumilia mtumishi yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma kwa kujihusisha na vitendo vya wizi katika eneo lake la kazi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameendelea na ziara ya kikazi Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad