HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 5, 2022

MWAFRIKA AZUA GUMZO KUCHEZA TIMU YA TAIFA YA AUSTRALIA KOMBE LA DUNIA 2022



Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
GARANG MAWIEN KUOL alizaliwa nchini Misri, Septemba 15, 2004 wazazi wake ni raia wa Sudan Kusini, familia yake ilihamia nchini Australia katika miji ya Shepparton na Victoria kama Wakimbizi kupitia nchini Misri alipozaliwa.

Kijana Garang anatoka kwenye familia ya mpira, Kaka yake aliyezaliwa mwaka 2001, Alou Kuol anacheza Klabu ya VfB Stuttgart inayoshiriki Ligi Kuu Soka nchini Ujerumani (Bundesliga), familia yake ni familia ya soka, pia Garang ana Kaka zake wengine watatu.

MMwaka 2017, Garang akiwa na umri mdogo, alianza kucheza Soka katika Klabu ya Central Coast Mariners. Ndoto zake hazikuishia hapo, mwezi Septemba mwaka huu aliitwa timu ya taifa ya Australia, na ameweka historia ya kuwa miongoni mwa Mchezaji waliocheza Michuano ya Kombe la Dunia 2022 akiwa na umri mdogo.

Awali tetesi barani Ulaya zilidai kuwa Klabu mbalimbali zinahitaji huduma ya Nyota huyo, zikiwemo Klabu za Barcelona na Chelsea, na hatimaye Newcastle United ya Uingereza ilimuona Kijana huyo na ikafanikiwa kukamilisha usajili wa awali ambapo atajiunga rasmi na timu hiyo mwezi Januari 2023.

KIPAJI CHAKE CHA SOKA KILIPOANZIA
Kuol alipewa udhamini baada ya kuonyesha kipaji cha kusakata kabumbu akiwa nchini Australia na alisajiliwa katika ‘Academy’ ya Central Coast Mariners. Januari 2021, Kuol alipandishwa daraja na kucheza timu ya wakubwa ya Mariners akiwa na umri wa miaka 17 tu.

Kwa mara ya kwanza, Desemba 21, 2021 aliingia kwenye mchezo wao dhidi ya APIA Leichhardt FC, akitokea benchi, kwenye mchezo huo wa mashindano ya 2021 FFA Cup, timu yake ya Mariners ilishinda mabao 6-1 na yeye akifunga bao moja dakika saba tu baada ya kuingia uwanjani.

Mnamo, Aprili 5, 2022 akiwa na Klabu hiyo ya Mariners alianza kucheza Ligi Kuu Soka nchini Australia (A-League Men) na alifunga bao moja katika mchezo dhidi ya Wellington Phoenix kwenye ushindi wa mabao 5-0.

Kuol alifunga mabao manne katika michezo saba ya Ligi Kuu Australia akiwa na timu hiyo, mnamo Juni 2022 rasmi alipewa mkataba wa miaka miwili na Klabu yake ya Mariners. Kuol alikuwa mmoja wa Wachezaji waliounda Kikosi cha Wachezaji waliocheza Ligi Kuu nchini Australia, Kikosi hicho kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Barcelona na kufungwa mabao 3-2.

MAJUKUMU KATIKA TIMU YA TAIFA YA VIJANA YA AUSTRALIA
Kuol aliwahi kuitwa katika timu ya taifa ya vijana ya Australia (U-20) mwezi Agosti 2022, alifunga bao akiwa na timu hiyo iliyoitwa kwa lengo la kuweka kambi ya kutambua vipaji. Oktoba 2022 Kuol aliitwa kwenye timu hiyo ya taifa (U-20) ambayo iliitwa kwa ajili ya mashindano maalum yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Asia (2023 AFC U-20 Asia Cup qualification) nchini Kuwait.

Kocha wa Kuol katika Klabu ya Central Coast Mariners, Nick Montgomery alisema kuwa Mchezaji huyo ana kipaji cha hali ya juu na ataisaidia timu ya taifa ya Australia katika Michuano ya Kombe la Dunia 2022, baada ya kuonyesha kiwango bora katika hicho cha Mariners msimu wa 2022-23.

Kuol alifunga bao katika mchezo wa pili wa kufuzu Michuano ya Kombe la Dunia 2022 kati ya timu yake ya Australia dhidi ya India baada ya kupiga ‘shuti’ kali lililomshinda Golikipa wa India katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Michuano hiyo.

MAJUKUMU KATIKA TIMU YA TAIFA YA WAKUBWA
Septemba 2022, Kuol aliitwa kwenye Kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa, wakati Kikosi cha timu hiyo kinajiandaa kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya New Zealand, alianza kucheza timu hiyo akiwa na umri wa miaka 18 na siku 10 akiingia kipindi cha pili.

Baada ya kuonyesha makali katika Kikosi hicho cha timu ya taifa, Kuol aliitwa tena kwenye Kikosi cha timu hiyo kilichofuzu kucheza Michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, wakati huo akiwa na miaka 18, hivyo kuwa Mchezaji mwenye umri mdogo kucheza Michuano hiyo.

Mchezo wa kwanza wa Michuano hiyo dhidi ya Ufaransa, Kuol aliingia kipindi cha pili, aliweka historia ya kucheza Kombe la Dunia akiwa na Australia akiwa na umri mdogo katika Kikosi hicho licha ya Australia kufungwa mabao 4-1 na Bingwa mtetezi, Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad