HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 5, 2022

Chuo cha VETA Chang'ombe kujenga chuo kingine Kigamboni

Mkuu wa Chuo cha VETA Chang'ombe  Mhandisi Jeseph Mwanda akizungumza kuhusiana historia ya Chuo hicho kwenye mahafali ya 25 yaliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam. 
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Aimbola Nko akizungumza katika Mahafali ya 25 ya Chuo cha VETA Chang'ombe  jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa VETA Kanda Dar es Salaam Angelus Ngonyani akizungumza malengo ya Kanda kuhusiana upanuzi wa Chuo cha VETA Chang'ombe katika eneo la Kigamboni kwenye mahafali ya chuo hicho jijini Dar es Salaam.




Matukio katika picha kwenye mahafali ya Chuo cha VETA Chang'ombe Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wazazi wakiwa katika mahafali ya 25 ya chuo cha VETA Chang'ombe jijini Dar es  Salaam.

*Ni kutokana na kuelemewa na idadi ya wanaojiunga 

Na Chalila Kibuda, Michuzi Tv
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Dar es Salaam inatarajia kujenga Chuo cha ufundi stadi na huduma Wilaya ya Kigamboni ili kuongeza vijana wengi kupata  ujuzi watakaochochea mapinduzi ya viwanda nchini.

Akizungumza  katika mahafali ya 25 ya Chuo cha VETA Chang'ombe, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Veta Kanda hiyo, Angelus Ngonyani amesema kuwa tayari wametenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya chuo baada ya kuona hicho kinaelemewa na wanafunzi.

Alisema kuna vijana wengi waliomaliza elimu ya msingi, sekondari pamoja vyuo vikuu  ambao wanatakiwa kujiunga na vyuo hivyo ili kupata ujuzi mbalimbali hivyo, wanahakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosheleza mahitaji yaliyopo.

"Tunawaomba wazazi muendelee kuwaleta watoto wenu katika vyuo vyetu kwa sababu watapata ujuzi mbalimbali katika ufundi na kuwawezesha kujiajiri na kuendesha maisha yao," alisema Ngonyani.

Aidha, aliziomba halmashauri kuwafikiria vijana wanaohitimu katika chuo hicho ili waweze kupata mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa ajili ya kuendeleza kazi zao za kibunifu na kujiajiri kutokana na jamii kuwa na mahitaji mengi ya masuala ya kiufundi.

Pia alisema wataendelea kuhakikisha wanatoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko  na yanayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Chang'ombe Mhandisi  Joseph Mwanda alisema kuwa kwa mwaka huu wamesajili wanafunzi 1,516 ambao wanasomea kozi mbalimbali za ufundi.

Alisema wanachukua wanafunzi wenye ulemavu kwa kuwa  wanafursa sawa  na wengine katika kuwafundisha masuala ya ufundi na kuwalea kwa pamoja.

"Kozi ya forklift (uendeshaji wa mtambo wa kubebea mizigo viwandani) ina soko kubwa sana kwa sababu maeneo mengi wanawahitaji wataalamu wa kozi hii ndani na nje ya nchi nasi tumeombwa orodha ya wanafunzi waliomaliza hapa na tumepeleka hivyo tunaamini wataajiriwa. Tunaomba wazazi mlete watoto wenu kusomea fursa hii kwani naamini watajiajiri na kuajiriwa," alisema Mwanda.

Pia alisema chuo hicho kina upungufu wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia kuendana na sayansi na teknolojia ili kufikia lengo la Tanzania ya viwanda.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya, Aimbola Nko alisema vijana hao wamekuwa wakibuni vitu mbalimbali kwa ajili ya kutatua changamoto katika jamii.

Alisema serikali inawategemea katika kuhakikisha wanakuza uchumi kupitia taaluma zao hivyo, wasisubiri kuajiriwa badala yake wajiajiri ili kujipatia kipato.

"Mnatakiwa kufanyia kazi elimu mliyoipata kwani waajiri wako tayari kuwapokea kwa sababu wanaamini Veta ni kitovu cha elimu na ujuzi  hivyo muwe mabalozi wa serikali kwani inawategemea kung'arisha na kuinua uchumi, mkatawaliwe na ujuzi, nidhamu na uzalendo kwa ajili ya maendeleo," alisema Nko.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad