HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 1, 2022

BURUNDI WAOMBA USHIRIKIANO NA TANZANIA UJENZI WA MIUNDOMBINU

 


WAZIRI wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane amezungumzia umuhimu wa ushirikiano katika ujenzi wa barabara kati ya Tanzania na Burundi ili kurahisisha huduma ya usafiri na uchukuzi baina ya nchi hizo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo alipotembelea Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhe. Dukundane ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyojenga Barabara nzuri na nyingi katika ushoroba wa Kati hali inayochochea maendeleo na kurahisisha huduma za uchukuzi katika ukanda huo.

“…Tunawashukuru sana kwa kazi kubwa ya ujenzi wa barabara nzuri, asilimia 80 ya magari ya Burundi yanayobeba mizigo yanatumia barabara za Tanzania,” amesema Mhe. Dukundane.

Aidha amesema Burundi itatuma wataalam wake wa masuala ya barabara kuja kujifunza TANROADS ili barabara za Burundi zifanane na za Tanzania kwa ubora na usalama.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila ameahidi kutoa ushirikiano kwa taasisi ya Ujenzi ya Burundi ili kuiwezesha kiutaalam na uwezo katika kufikia malengo yake na ya nchi za ushoroba wa Kati kwa ujumla.

Eng. Mativila amebainisha kuwa asilimia 90 ya mizigo inayoingia na kutoka Tanzania hutumia njia ya barabara hivyo ushirikiano kati ya nchi hizo utaleta tija kwa pande zote katika sekta ya usafiri na uchukuzi na hivyo kuchochea biashara na ujirani mwema.

Waziri Dukundane yuko nchini kwa ziara ya kujifunza namna sekta za ujenzi na uchukuzi zinavyofanya kazi kwa pamoja katika kuleta tija na ufanisi ambapo tayari ameshatembelea taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi za TPA, TRC na TANROADS.
Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane akizungumza katika kikao na Menejimenti ya TANROADS (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kubadilishana uzoefu leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila akizungumza jambo katika kikao cha pamoja na Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane na ujumbe wake (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kubadilishana uzoefu jijini Dar es salaam.
Kikao kati ya Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane na ujumbe wake pamoja na Menejimenti ya TANROADS kikiendelea leo jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane na ujumbe wake pamoja na Menejimenti ya TANROADS mara baada ya mazungumzo yao jijini Dar es salaam.
Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane (kushoto), akizungumza jambo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila (kulia) mara baada ya ziara yake ya kutembelea TANROADS jijini Dar es salaam.
Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Captain Dieudonne Dukundane (kushoto), akizungumza jambo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila (kulia) mara baada ya ziara yake ya kutembelea TANROADS jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad