HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 18, 2022

BENKI YA CRDB, VISA KULETA MAPINDUZI SEKTA YA UTALII NA USAFIRISHAJI KUPITIA KADI ZA KIDIJITALI

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akifanya mazungumzo na Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa Visa International, Alfred Kelly kuhusu ushirikiano baina ya taasisi hizo katika kuanzisha huduma za malipo ya kidijitali katika sekta ya utalii. Mkutano huo ulifanyika wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika Washington DC Marekani siku ya Ijumaa tarehe 16 Desemba 2022.

Washington DC 16 Desemba 2022 - Benki ya CRDB Plc, Benki inayoongoza kwa uvumbuzi wa kidijitali nchini, na kampuni ya kimataifa ya mifumo ya malipo ya Visa International, leo wamekubaliana kuhusu ushirikiano wa kuanzisha huduma ya kadi za kidijitali kwa ajili ya kuboresha huduma za malipo katika sekta ya utalii nchini.

Kupitia kadi hizo, Benki ya CRDB na Visa wanatarajia kutoa njia rahisi zaidi ya kufanya na kupokea malipo kwa wateja na makampuni ya sekta ya utalii na usafirishaji kwa usalama na uharaka kulinganisha na mifumo mingine ya malipo.

Ushirikiano huo mpya na Visa, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, ni hatua muhimu katika kufikia lengo la Benki hiyo katika kuleta mapinduzi katika mfumo wa kiikolojia wa malipo ya katika sekta ya utalii na usafiri nchini.

“Sekta ya malipo iko katikati ya mapinduzi na kuna hitaji kubwa la makampuni na mamlaka za utalii na usafiri kusimamia vyema uzoefu mzima wa malipo,” alisema Nsekela.

Aliendelea kusema kuwa, sekta hiyo inazidi kushamiri na kwamba kuna wimbi kubwa la watalii nchini kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia kipindi cha Televisheni cha ‘Royal Tour’.

Sekta ya utalii nchini Tanzania inazidi kuimarika baada ya janga la UVIKO-19. Ripoti ya Benki Kuu (BOT) inaonyesha kuwa mapato ya sekta hiyo yameongezeka maradufu hadi kufikia dola milioni 2,243.8 mwezi Septemba kutoka dola milioni 1,106. Watalii pia wameongezeka kwa asilimia 63.5 hadi 1,332,476.

Katika muktadha huo, Nsekela alisema kuwa makampuni katika sekta ya utalii na usafirishaji yanahitaji ufumbuzi wa hali ya juu na muunganisho katika mifumo ya kisasa ya malipo ambayo itakidhi mahitaji ya wateja wao ambao wengi wanapendelea huduma za kidijitali ambazo ni rahisi kutumia.

"Ushirikiano huu mpya na Visa utaisaidia Benki ya CRDB katika kuboresha mifumo yake ya kidijitali hususan katika huduma za kadi, jambo ambalo litakwenda kuboresha uzoefu wa huduma za malipo kwa taasisi, makampuni na wateja," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Visa, Alfred Kelly Jr alisema mfumo huo wa malipo kupitia Kadi za Kidijitali utakwenda kusaidia kuongeza ufanisi wa malipo na kutaimarisha mikakati ya malipo kwa wadau wote walio katika mnyororo wa tahamani wa sekta ya utalii na usafirishaji nchini Tanzania.

"Tunafurahia kuendeleza ushirikiano wetu na Benki ya CRDB, ushirikiano uliojikita zaidi katika kutumia utaalamu na ubunifu wa mifumo ya malipo kutoka kwa mashirika yote mawili ili kusaidia kukua kwa sekta ya utalii na usafirishaji," alisema na kubainisha zaidi kuwa watafanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha ajenda ya ujumuishi wa kifedha nchini.

Benki ya CRDB na Visa pia walikubaliana kuanzisha huduma ya kutuma fedha kuvuka mipaka ili kurahisisha kuchochea biashara na kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi kutuma fedha nyumbani kwa urahisi na usalama.

"Rais Samia amefanya kazi kubwa sana ya kufungua nchi; biashara inapanuka, hivyo tunatakiwa kuweka miundombinu imara ya malipo ili kusaidia kuichochea. Hii ni pamoja na kuwawezesha Watanzania walioko ughaibuni kuwekeza nchini," alisema Nsekela.

Mkutano kati ya Benki ya CRDB na Visa ulifanyika pembezoni mwa Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika. Mapema mwezi huu viongozi wa mashirika hayo walikutana Qatar, ambapo yanashirikiana kuwapatia mashabiki wa Kombe la Dunia FIFA huduma za malipo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad