HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 22, 2022

WATAALAMU WA MFUTA NA GESI WANOLEWA

Mkurugenzi Mtendaji wa EREA Dkt.  Geoffrey Mabea akizungumza na wadau wa mafuta na gesi wakati wa mafunzo kwa wataalamu wa mafuta na gesi 230 kutoka nchi 27 Afrika kutambua namna ya kuandaa mikataba inayohusu sekta hiyo ili kujiinua na kuchangia pato la Taifa.
Mkurugenzi Mkuu Rasilimali Watu East Africa Community ( EREA) Ruth Simba akikabidhi cheti cha kutambua mchango wa mkufunzi Dr. Aloys Rugazia katika hafra yakuhitimisha mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi Karibuni.
Moja Kati ya wakufunzi wa mafunzo ya mafuta na gesi, Dkt.  Aloys Rugazia akitoa mafunzo kwa wataalamu sekta hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam
Moja Kati ya wakufunzi wa mafunzo ya mafuta na gesi, Dkt.  Aloys Rugazia akitoa mafunzo kwa wataalamu sekta hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Dkt. Shirley Baldwin Mushi akipokea cheti cha kutambua mafunzo aliyotoa kwa Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ruth Mtoi Simba mara baada ya mafunzo ya wadau wa Mafuta na gesi yaliyofanyika jijini Arusha.

Na Karama Kenyunko, Michuzi Blog
TAASISI za Udhibiti wa huduma za Mafuta na Umeme kwa nchi sita za Afrika Mashariki (EREA) iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imesema mpaka sasa imetoa mafunzo kwa wataalamu wa mafuta na gesi 230 kutoka nchi 27 Afrika.

Imesema mafunzo hayo yanalenga kuwafanya wataalamu watambue namna ya kuandaa mikataba inayohusu mafuta na gesi na namna watakavyoshiriki kuinua sekta ya mafuta na gesi na kuchangia pato la taifa.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa EREA, Dk Geoffrey Mabea wakati akizungumzia mafunzo wanayoyatoa .

"Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa katika nchi mbalimbali lakini sisi tuliona tuyafanyie hapa kwetu kwa kuwatumia watalaam wa ndani Dr. Aloys Rugazia na Dr. Shirley Mushi ambapo tumeweza kuwakutanisha wataalamu wa nchi za Tanzania na Kenya," amesema Dk Mabea.

Ameongeza kuwa huu ni mwaka wa pili wanatoa mafunzo ya uelewa kuhusu sekta hiyo na mpaka sasa wataalamu 230 wamenufaika na mafunzo wanayoyatoa kupitia mtandao na chuoni.

Hata hivyo, amesema katika mafunzo yaliyofanyika Novemba 14-18 mwaka huu, wataalamu hao walijadiliana kwa kina kuhusu uchakataji wa mafuta ghafi na gesi chini ya wakufunzi toka hapa hapa Tanzania, Dr. Aloys Rugazia na Dr. Shirley Mushi na kushauri haja ya kuwepo kwa mitambo ya Kuchakata Mafuta (Refinery) katika nchi za EAC ili nchi zipate manufaa yakuchakata Mafuta nyumbani badala yakuagiza Mafuta ambayo yamechakatwa tayari.

Dk Mabea ameeleza kuwa biashara ya mafuta imekuwa changamoto kubwa kutokana na gharama zake hivyo wangekuwa na mitambo ya kuchakata mafuta ghafi ingesaidia nchi za Afrika Mashariki kufanya biashara wenyewe na hivyo kupunguza utegemezi na kudhibiti bei za Mafuta na mbolea zitokanazo na Mafuta ghafi.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kuwaleta pamoja wadhibiti kwa lengo la kupandisha miundo mbinu ya nchi za EAC, kusaidia nchi hizo kuwa na misingi bora ya udhibiti na kutekeleza wajibu wao kwa kuwa na wataalamu wengi.

Amesema wameanzisha Chuo kinachotoa mafunzo kwa wadhibiti kilichopo Arusha, ambacho kinatoa mafunzo kuhusu nishati za mafuta na gesi na lengo ni kuwaelimisha namna ya kuchimba na kuchakata gesi kwa matumizi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad