TACHA YAIOMBA SERIKALI KUFUNGUA ANGA LA UWINDAJI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 19, 2022

TACHA YAIOMBA SERIKALI KUFUNGUA ANGA LA UWINDAJI

 
CPL Fedson Misonge kutoka Shirika  la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi Tanzania (TPFCS,) akitoa mada katika mafunzo hayo yaliyofanyika leo katika viwanja vya Shabaha Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Uhifadhi na Uwindaji Tanzania (TACHA,) Kanali Thomas Ndonde (rtd) akizungumza wakati wa mafunzo hayo na kuiomba Serikali kufungua rasmi shughuli za uwindaji zilizozuiwa kwa miaka mitatu sasa, Leo jijini Dar es Salaam.


WAMILIKI na Watumiaji wa silaha za moto za kiraia wanaojihusisha na shughuli za uwindaji kupitia Chama cha Uhifadhi na Uwindaji (TACHA) wamepewa mafunzo maalum ya kujengewa uwezo, umahiri na kujiamini zaidi katika matumizi ya silaha hizo, huku ombi kubwa likitolewa kwa  Serikali kuruhusu kuendelea kwa shughuli za uwindaji zilizofungwa kwa miaka mitatu mfululizo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shabaha leo jijini Dar es Salaam Mratibu msaidizi wa mafunzo ya umahiri wa utumiaji na utunzaji wa silaha za moto za kiraia nchini  kutoka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi (TPFCS,) Ravent Vedasto amesema, mafunzo hayo yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria ya The Firearms and Ammunition Control Act ya mwaka 2015.

"Leo tupo katika viwanja hivi vya shabaha chini ya Jeshi la Wananchi Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chama cha Uhifadhi na Uwindaji  (TACHA,) ambao ni wamiliki na watumiaji wa silaha maalum kwa shughuli za uwindaji...Tunafanya hivi ili kuwajengea uwezo wa kuzitumia na kubaini wale wanaozitumia kimakosa na kuwajengea kujiamini zaidi ili waweze kuzitumia vizuri zaidi." Amesema.

Aidha amesema, kwa miezi mitatu kuanzia Julai hadi Oktoba mwaka huu jumla ya raia 1200 kupitia mwavuli wa TACHA wamesajiliwa na kupatiwa mafunzo na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi Tanzania ( TPFCS.) ambalo pia linahusika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi, umahiri wa matumizi na utunzaji wa silaha pamoja na ulinzi binafsi.

Awali akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Uhifadhi na Uwindaji na Tanzania (TACHA) Kanali. Thomas Ndonde (rtd) alieleza kuwa mafunzo hayo ni kwa mujibu ya sheria ya umiliki wa silaha na kuwataka raia wanaomiliki silaha kushiriki katika mafunzo hayo adhimu ya umiliki wa silaha.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo pia yanakwenda sambamba na maandalizi na msimu wa Uwindaji ikiwa Serikali itaridhia na kuruhusu Uwindaji na Uhifadhi baada ya kutoruhusu zoezi hilo kwa miaka mitatu mfululizo.

"Serikali yetu ni sikivu na elewa tunaamini itafungua tena anga la uwindaji na sisi kama wahusika tuna uelewa kupitia mafunzo mbalimbali ya namna hii yanayotolewa na tupo tayari kwa uwindaji kwa kufuata sheria na matakwa ya Serikali."

Vilevile ametoa wito kwa Wizara ya Utalii na Maliasili kutoa kibali kwa wawindaji kwa msimu ujao wa uwindaji ambao kwa kiasi kikubwa huchangia kukua kwa uchumi wa Nchi, uhifadhi wa rasilimali za utalii pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa ajira.

Chama cha Uhifadhi na Uwindaji Tanzania ( TACHA,) kina jukumu la kuwinda na kuhifadhi rasilimali za utalii kwa kuzingatia kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali na ombi lao kubwa kwa sasa ni kwa Serikali kufungua anga la uwindaji lililofungwa kwa miaka mitatu mfululizo.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza kwa nadharia mapema leo na yatahitimishwa kwa vitendo ili kuwapika vilivyo wamiliki hao juu ya umiliki na matumizi ya silaha na yamedhaminiwa na kampuni ya Orexy Gas kupitia kampeni ya kutumia nishati ya gesi na kutunza mazingira.
Mafunzo yakiendelea.
Insp. wa Polisi Vincent Buluba kutoka TPFCS akitoa mada katika mafunzo hayo.

 ASP Hamis Luyeko akitoa mada katika mafunzo hayo ya umiliki wa silaha kwa wanachama wa Uhifadhi na Uwindaji (TACHA,) yaliyolenga kuwajengea umahiri zaidi katika kuzitumia, Leo jijini Dar es Salaam.

S/sgt Venus Mwamtembe akitoa mada katika mafunzo hayo kwa wanachama wa TACHA, mafunzo hayo ni kwa mujibu wa sheria na utekelezaji  ya mwaka 2015.Mafunzo yakiendelea.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad