HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 29, 2022

Kanali Abas: Kateni bima za afya kuwa na uhakika wa matibabu

 

Na Mwandishi Maalum – Mtwara
WANANCHI wa Mkoa wa Mtwara na mikoa ya jirani wametakiwa kukata bima za afya kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwani matibabu ya kibingwa hugharimu fedha nyingi ambapo mara nyingi wananchi hao hushindwa kugharamia matibabu hayo pale wanapoyahitaji.

Akizungumza na wananchi hao leo wakati wa uzinduzi wa kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini (SZRH) Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas alisema kumekuwa na changamoto kwa wananchi wengi kutokukata bima za afya hivyo kushindwa kulipia gharama za matibabu haswa matibabu ya kibingwa.

Kanali Abbas alisema ni muhimu kwa wananchi wanaopata huduma katika Hospitali hiyo kuhakikisha wanakata bima za afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwani matibabu ya kibingwa hugharimu fedha nyingi na mara nyingi sio rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuweza kuwa na fedha taslim anapopatwa na changamoto za afya.

“Mkoa wa Mtwara umepata bahati ya kupata Hospitali kubwa kwa ajili ya kanda nzima ya Kusini bahati ambayo inaendelea kwa wataalam mabingwa wa moyo kutembelea Hospitali hiyo na kutoa huduma za kibingwa za moyo ambazo kwa asilimia kubwa wananchi wa mkoa huo ingekuwa ngumu kuzifuata Dar es Salaam,”.

“Tunaishukuru Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa jitihada kubwa inayofanya ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ikiwepo eneo la afya kwani hii ni bahati kwa mkoa wetu kupata hospitali kubwa pamoja na kutuletea wataalam mbalimbali wakiwemo wa magonjwa ya moyo ili huduma za magonjwa hayo ziweze kusogea hadi kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kusafiri kufuata huduma mahali zilipo”, alisema Kanali Abbas.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia mabingwa wa magonjwa ya moyo wanaenda kutatua changamoto za wananchi sio tu kwa watu wa Mkoa wa Mtwara lakini pia katika mikoa ya jirani ya Lindi na Ruvuma pamoja na wananchi waliopo nchi za jirani na Tanzania za Msumbiji na Comoro.

Aidha Kanali Abbas aliwataka mabingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kuwa walezi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini ili hapo baadaye watalaam wa Hospitali hiyo waweze kuendelea kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo bila ya usimamizi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Tatizo Waane alisema JKCI imeanzisha zoezi endelevu la kuwafuata wananchi mahali walipo na kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya magonjwa wa moyo ili kuhakikisha watu wote wanaohitaji matibabu ya moyo wanafikiwa kwa wakati.

“Sisi kama JKCI Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alituelekeza kuzilea Hospitali tatu za kanda ikiwemo Hospitali hii ya Rufaa Kanda ya Kusini, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Rufaa ya Kigoma ili nazo ziweze kupata uzoefu kama tulionao JKCI na kwa kutimiza hilo hadi sasa tumeshaifikia Hospitali ya Chato na sasa tupo hapa Kanda ya Kusini”, alisema Dkt. Waane.

Dkt. Waane alisema kambi hiyo maalum imelenga kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo, elimu kwa wataalam wa afya ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kukusanya taarifa kuhusu magonjwa ya moyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuweza kuisaidia serikali katika mikakati yake ya huduma za afya ili iweze kujua hali halisi ilivyo kuhusu magonjwa hayo.

“JKCI itaendelea kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wote wa Tanzania ambapo kwa kuanzia imejipanga kutembelea mikoa 15 ikiwemo mkoa wa Lindi, Tanga, Zanzibar, Kilimanjaro, Katavi, Mbeya na mikoa mingine,” alisema Dkt. Waane.

Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo George Liwenga alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu pamoja kisukari kwa muda mrefu hivyo aliposikia ujio wa mabingwa wa moyo akavutiwa kufika katika kliniki zao ili naye afanyiwe uchunguzi wa moyo kwani magonjwa aliyonayo yanaweza yakamsababishia kupata magonjwa ya moyo.

“Nimepata huduma za kufanyiwa uchunguzi katika moyo wangu, nimefurahi sana kuwa miongoni mwa wananchi tuliojitokeza kuchunguza afya zetu kwani maradhi ya moyo yanampata kila mtu hivyo ni vyema wananchi wakawa na tabia ya kuchunguza afya zao,”.

“Ninaomba huduma kama hizi ziendelee kutolewa mara kwa mara hapa mkoani kwetu ili sisi watu wazima tusioweza kusafiri kwa muda mrefu tuweze kupata huduma hizi karibu na maeneo tunayoishi”, alisema Liwenga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad