FANYENI KAZI MSIBUBIRI VYEO - AG FELESHI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 17, 2022

FANYENI KAZI MSIBUBIRI VYEO - AG FELESHI

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akisisitiza jambo wakati Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Luhende na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sara Mwaipopo walipomtembelea Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma na kisha kuwa na mazungumzo ya pamoja na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawakili Wakuu wa Serikali na Mawakili Waandamizi wa Serikali.

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amerejea wito wake wa kuwataka Watumishi waliopo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majumuku yao kwa weledi , uaminifu na uadilifu na siyo kusubiri teuzi au vyeo.

Ametoa rai hiyo leo, alhamisi wakati wa mazungumzo yake na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt Bonifance Luhende na Naibu Wakili Mkuu Bi. Sara Mwaipopo waliofika Ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo na ambayo pia yalihudhuriwa na Menejimenti, Mawakili Wakuu na Mawakili wa Waandamizi wote kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Feleshi amesema, uongozi hautafutwi ,uongozi unakuja kwa kufanya kazi.

“ Niwapongeze kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwenu na Mhe. Rais kushika nafasi hizo za uongozi. Uongozi hautafutwi, tekeleza majukumu yako, jukumu ulilonalo mkononi ndilo lako, timiza wajibu wako na mengine yatafuata”. Amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesisitiza haja na umuhimu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa na ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo kimsingi Ofisi hiyo inatekeleza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali .

Akielezea Zaidi kuhuhusu haja na umuhimu wa Ofisi hizo mbili wa kufanya kazi kwa Karibu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kuwa taratibu kadhaa zimeshawekwa zikiwamo za kuwa na maafisa dawati wanaoratibu mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa kwa haraka na kwa wakati baina ya Ofisi hizo mbili.

Naye Wakili Mkuu Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance Luhende amemhakikishia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba, yeye binafsi, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi yote wanalichukulia suala na uhusiano na Ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni jambo la kipaumbele.

Dkt Lunhede amesema, Ofisi hizo mbili ni kiungo muhimu katika kuisadia Serikali kufikia malengo yake yakiwamo ya kuwaleta wananchi maendeleo, lakini pia ni Ofisi ambazo mambo mengi na mazito yanapita kwenye Ofisi hizo, mambo ambayo wakati mwingine yanahitaji ushauri wa haraka au maamuzi ya haraka hivyo ushirikiano na mawasiliano kati yake ni jambo ambalo halikwepeki.

“Ofisi zetu hizi zina mambo mazito yanayopita mikononi mwetu, mambo yanayohitaji wakati mwingine kutoa ushauri na maamuzi ya haraka kwa Serikali ili mambo yaweze Kwenda. Kwa hiyo kwetu sisi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jambo la ushirikiano na Ofisi yako, Mhe Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunalipa kipaumbele” amesisitiza Wakili Mkuu wa Serikali .

Amebainisha kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo ni muhimu kwa Ofisi hizo kuwa na mwelekeo na maono ya Pamoja ili kuisaidia Serikali .

“Tunatekeleza majukumu yetu kwa niaba yako Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunapaswa kuwa na maono na uelewa wa Pamoja, tunapaswa kucheza kama timu moja, hakuna mchezaji anayeweza kushinda bila ya ushiriki wa wachezaji wengne , lengo letu si kushindana bali kuisaidia serikali ishinde” Akasema Wakili Mkuu wa Serikali.

Aidha katika mazungumzo hayo, Ofisi hizo mbili pia zimekubaliana kuwatumia Mawakili wa Serikali waliomo katika Kanzi Data ya Mawakili wa Serikali inayoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pale watakapohitajika kuisaidia serikali kwa mijibu wa taaluma zao, uwezo na uzoefu wako katika masuala mbalimbali.

Octoba 10, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwateua Dkt. Boniface Christopher Luhende kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na alimteua Bi. Sara Duncan Mwaipopo kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad