HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 11, 2022

UFARANSA INATOA KIPAUMBELE KATIKA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA – BALOZI GUILLON



 

 Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Axel-David Guillon akizungumza wakati wa hafla ya  kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous ambaye yupo nchini katika ziara ya kikazi na kuadhimisha siku kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani inayoadhimishwa Oktoba 11, Balozi Guillon amesema ajenda ya kimataifa ya Ufaransa inatoa kipaumbele cha kukuza usawa wa kijinsia na utekelezaji wa diplomasia ya wanawake.
 
 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous akizungumza katika hafla hiyo na kuipongeza Tanzania katika utekelezaji ya miradi na mipango mahususi kwa wanawake na kuishukuru Ufaransa kwa kuwa wachangiaji na wafadhili wakubwa kwa UN-Women.
 
 

 

UBALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania umeeleza kuwa usawa wa kijinsia ni hatua muhimu ya sera ya maendeleo ya Ufaransa na katika sehemu kubwa inaingizwa katika program za maendeleo za Ufaransa kama ilivyoelezwa katika mikakati ya kimataifa  ya usawa wa jinsia 2018-2022 ambapo Tanzania na Ufaransa zimekuwa na mjadala wa kina kuhusu masuala yaliyopendekezwa na jukwaa hilo.

Hayo yameelezwa na Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Axel-David Guillon wakati wa kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous ambaye yupo nchini katika ziara ya kikazi na kuadhimisha siku kimataifa ya Mtoto wa Kike duniani inayoadhimishwa Oktoba 11.

Balozi Guillon amesema ajenda ya kimataifa ya Ufaransa inatoa kipaumbele cha kukuza usawa wa kijinsia na utekelezaji wa diplomasia ya wanawake na kwa miaka mingi Ufaransa imekuwa ikifanya kazi na UN- WOMEN katika kupambana na ukosefu wa usawa wa kijinsia na kukuza uwezeshaji wa wanawake.

‘’Julai 2021 Ufaransa ilishirikiana na UN-Women na Serikali ya Mexico katika kongamano la usawa wa jinsia mjini Paris ambapo Tanzania iliwakilishwa na ngazi ya juu na wadau mbalimbali ambao walikaa pamoja ili kuchochea hatua za pamoja kati ya mataifa , sekta binafsi, mashirika ya vijana, mashirika ya kiraia na makundi ya wanawake…washiriki 40,000 walitoka na mpango uliopitishwa wa kuongeza kasi wa kimataifa wa usawa wa kijinsia wa miaka mitano ambao ulilenga uwekezaji wa dola Bilioni 40 ili kufikia usawa wa kijinsia’’ Amesema.

Amesema Rais Macron wa Ufaransa amelipa kipaumbele suala la jinsia tangu mwaka 2018 alipozindua mpango wa ufadhili taasisi za masuala ya jinsia duniani kote na kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 hadi 2022 imefadhili Euro milioni 120 kwa shughuli za harakati za wanawake ulimwenguni kote hasa kwa nchi zenye kipato cha chini ambapo Euro milioni 333 zimetolewa katika sekta ya elimu kupitia mradi wa elimu.

Vilevile amesema wanajivunia mafanikio katika sehemu walizoonesha ushiriki wao ikiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya kwa akina Mama waoishi na VVU na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika hospitali ya Vijibweni na hiyo ni pamoja na kutoa Euro milioni 77 katika benki ya CRDB ili kutoa fursa ya mikopo kwa wanawake huku katika sekta ya kilimo ambayo asilimia 80 ya nguvu kazi ni wanawake wameunga mkono kupitia mradi wa uwezeshaji kiuchumi wanawake kupitia mradi wa kilimo hai kwa Dola 5000,000 na wanashirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Msichana Initiative.

Aidha amesema kuwa Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD,) limewekeza Euro milioni 900 kwa mwaka 2021 kwa ajili ya miradi inayolenga usawa wa kijinsia katika maeneo kadhaa ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake, afya ya uzazi pamoja na masuala ya uongozi wa wanawake na ushiriki wa kisiasa na Ufaransa inahusika katika mazungumzo na pande nyingi sambamba na kuchangia mashirika ya kimataifa  yanayojitolea kwa usawa wa jinsia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous amesema Ufaransa wamekuwa wachangiaji na wafadhili wakubwa kwa UN-Women hasa kupitia michango yao na hivi karibuni ilitangaza mchango wa Euro Bilioni 1.6 kwa ajili ya mfuko wa kimataifa wa kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria na kuishukuru kwa kuandaa miradi kadhaa na UN-Women Tanzania na kuzungumza masuala ya uongozi kwa vijana wakike na ushiriki wao katika kufanya maamuzi sambamba na suala la teknolojia na uvumbuzi unaofanywa na wanawake.

Bi.Sima ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa masuala ya kijinsia kwa kiwango bora na kuwa kinara kwa kuteuliwa kuongoza jukwaa la uwezeshaji usawa hususani katika uchumi kwa wanawake.

Pia ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa kushirikiana na Serikali na Asasi za kiraia katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa kwa kiwango cha juu katika kujenga kizazi chenye usawa na kuzipongeza taasisi za sekta binafsi Tanzania zikiwemo benki kwa kuwa na vitengo maalum vya kuwainua wanawake kiuchumi kupitia mikopo ya riba nafuu kupitia benki.

‘’Ni dhahiri COVID-19 imeleta madhara kwa wanawake katika Nyanja za uchumi na inahitajika nguvu katika kuleta maendeleo imara, niipongeze Tanzania kupitia benki za NMB na CRDB ambazo zimekuwa na vitengo maalumu vya kuinua uchumi wa wanawake kupitia mikopo.’’ Amesema.

Awali Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameeleza kuwa Ufaransa ni washirika wazuri wa shughuli za maendeleo na jamii ambapo Septemba mwaka huu Tanzania ilichaguliwa kuongoza  jukwaa la uwezeshaji usawa hususani katika uchumi kwa wanawake na Ufaransa ni miongoni mwa nchi saba zilizochaguliwa kuongoza jukwaa hilo linalotegemewa kuleta matokeo bora.

Amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuandaa mazingira wezeshi ya kuwasaidia wanawake na vijana wakike hasa katika kufikia usawa katika Nyanja ya kiuchumi ifikapo 2026 na nchi imedhamiria kutekeleza mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayolenga wanawake.

‘’Mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa Tanzania bara na Zanzibar unatoa dira na mwongozo wa sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, madini, viwanda, utalii na utoaji huduma na mpango huo umezingatia jinsia katika kukuza uchumi.’’ Amesema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika hafla hiyo na kueleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuandaa mazingira wezeshi ya kuwasaidia wanawake na vijana wakike hasa katika kufikia usawa katika Nyanja ya kiuchumi ifikapo 2026 na nchi imedhamiria kutekeleza mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayolenga wanawake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki akizungumza katika hafla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN-Women) Bi. Sima Sami Bahous iliyofanyika katika Ubalozi wa Ufaransa Tanzania, Kairuki ameishukuru UN-Women kupitia ubalozi huo kwa jitihada za kumkomboa mwanamke kiuchumi kupitia miradi mbalimbali.


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad