HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 27, 2022

TRC YAPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KONGAMANO LA MASHIRIKA YA RELI UKANDA WA SADC

 

Picha ya Pamoja.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli (mwenye koti jekundu) na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Jamila Mbarouk (wakwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Reli kusini mwa Afrika Bi. Sizakele Mzimela, Mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho hilo Bw. Babe Botana (wakwanza kulia) na Rais mstaafu wa Shirikisho hilo Bw. Johny Smith, baada ya ufunguzi wa kongamano la mashirika ya Reli ya Ukanda wa SADC Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.
Muonekano wa banda la Shirika la Reli Tanzania katika maonesho ya mashirika ya reli ya ukanda wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SARA Rail Conference and Exhibition 2022, yanayofanyika Johannesburg nchini Afrika ya Kusini tarehe 26 hadi 28 Oktoba, 2022.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli, na mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Jamila Mbarouk,wakiwa katika Kongamano la Mashirika ya Reli ya Ukanda wa SADC linaloendelea jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.

SHIRIKA la Reli Tanzania- TRC limeshiriki kongamano na maonesho ya 11 ya Mashirika ya Reli katika Ukanda wa SADC (SARA RAIL conference and Exhibition 2022) yanayoendelea jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 26 hadi 28 Oktoba,2022.

Kongamano na maonesho ya mwaka huu yamebeba ujumbe unaolenga Ubunifu katika mabadiliko ya Teknolojia za uendeshaji wa Reli, ambapo pamoja na Tanzania inayowakilishwa na TRC, mataifa mengine ni wenyeji Afrika ya Kusini,Botswana,Eswatini,Msumbiji, Angola, DRC, Malawi na Zambia.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa Kongamano hilo,aliemuwakilisha Mkurugenzi mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli, ameeleza kuwa Tanzania imethibitisha kuwa mbele katika mipango ya mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya Reli kusini mwa Afrika kama ujumbe wa kongamano la mwaka huu unavyosisitiza.

“Kupitia SGR ukilinganisha na mataifa mengine ya ukanda huu, tunaonekana tuko mbele zaidi kwa ujenzi wa miundombinu hii ya kisasa ambayo itasaidia sana katika kupunguza muda wa safari na ufanisi katika uendeshaji” alisema Bi. Amina.

Awali akifungua Kongamano hilo, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Reli kusini mwa Afrika Bi. Siza Mzimela, ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya Usafirishaji kwa njia ya Reli katika ukanda wa SADC kuchukua jukumu la kuboresha hali ya miundombinu kwa ufanisi zaidi.

“umuhimu wa reli katika kusukuma gurudumu la maendeleo haupingiki, na endapo njia hii ya usafiri haitaboreshwa Afrika haitaweza kuona umuhimu wa Reli katika ufanisi wa matumizi ya rasilimali zake na utajiri tuliojaaliwa” alisema Bi. Mzimela.

Aidha ameogeza kuwa, wadau wote wanatambua hali ya uchakavu wa miundombinu na vifaa vya uendeshaji wa reli katika ukanda wa SADC na Afrika kwa ujumla, na kwasababu hiyo kunahitajika ubunifu wa mifumo ya biashara na uendeshaji ili kujikwamua na kuleta ufanisi.

Kupitia maonesho yanayoenda sambamba na kongamano hilo, Shirika la Reli Tanzania limeshiriki kuonesha juhudi na mikakati ya Serikali katika kuleta mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya Reli.

“kupitia ushiriki wa TRC kwenye maonesho haya tumekutana na wenzetu kutoka nchi mbalimbali, kuanzia mashirika yanayotoa huduma kama za TRC mpaka makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyotumika katika uendeshaji wa Reli, kwahiyo kwetu imekuwa ni fursa ya kukutana na wadau wapya lakini pia kuona wenzetu wanafanya nini, au wao kujifunza kutoka kwetu” alisema Mkuu wa Kitengo cha Habari TRC Bi. Jamila Mbarouk.

Pamoja na mashirika ya Reli, makampuni mbalimbali ya utengenezaji vifaa vya uendeshaji, teknolojia ya Reli, mitambo na vifaa vya usalama kazini, yameshiriki kongamano la mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad