SERIKALI YAITAKA JAMII KUACHA KUTEKETEZA TAKA HATARISHI KIHOLELA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 13, 2022

SERIKALI YAITAKA JAMII KUACHA KUTEKETEZA TAKA HATARISHI KIHOLELA

 

Baadhi ya wadau wakipata maelezo katika Banda la Tindwa Medical Health Services (TMHS) leo Oktoba 13, 2022 katika mkutano mkuu wa Afya wa 2022 mara baada ya kumaliza mkutano mdogo wa kujadili namna ya kuteketeza Taka hatari katika jamii. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Oktoba 13, 2022.Na Karama Kenyunko Michuzi TV

SERIKALI imeitaka jamii kuacha kuchoma hovyo taka harishi ikiwemo dawa na rasta kwani ni kinyume na sheria na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.

Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa ameyasema hayo leo Oktoba 13, wakati wa kujadili uteketezaji wa taka hatarishi ulioandaliwa na kampuni ya Tindwa Medical health services (TMHS) ya jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la tisa la afya (Health Summit) lililomalizika leo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa sheria ya usimamizi wa kemikali za viwandani na majumbani ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2020 inaeleza kuwa ni kosa kwa mtu yoyote kuingiza na kuzalisha kemikali taka nchini.

Amesema adhabu za makosa hayo ni faini au ikaenda pamoja na vifungo kwa wale wataobainika kuzalisha kemikali taka bila kuchukua hatua yoyote ya kuzuia au kuteketeza.

"Tunaendelea kuelimisha watu wasizalishe kemikali taka, wachukue hatua ya kupeleka sehemu husika ambazo zina vifaa vya kuteketeza kwa njia salama bila kuathiri afya zao wenyewe pamoja na mazingira," amesema Mkapa.

Ameongeza kuwa yapo makasha ya kuhifadhia kemikali yanatumiwa kuhifadhi chakula, hivyo huweza kuathiri watu hivyo alishauri wasitumie kwani wanakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo bvya sheria.

Pia amesema suala la gharama kuwa juu linatokana na watoa huduma wachache wa kuteketeza taka hizo hivyo aliomba wadau wengi kujitokeza ili kuwepo kwa ushindani jambo ambalo litasaidia kupungua kwa gharama za uteketezaji wa takataka hatarishi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya uteketezaji wa taka hatarishi wa Kampuni hiyo ya TMHS, Charles Luvubhu amesema zipo namna nzuri za uteketezaji wa taka hatarishi kutoka kwa mteja ikiwemo hospitali, duka la dawa, viwanda vya kemikali na bidhaa zilizokaa kwa muda mrefu ikiwemo kemikali.

Amesema wao kama wahusika wakuteketeza taka hatarishi wanajukumu la kuteketeza pia biashara za magendo zinazotakiwa kuharibiwa ambazo zinashikiliwa na serikali.

"Bado safari ndefu kuhakikisha tunaelimisha jamii kufikia malengo ya ukusanyaji wa takataka, zimetapakaa majumbani kwa sababu hakuna uelewa . Kwenye fukwe za bahari pia kuna takataka hatarishi," amesema Luvubhu.

Amesema wanapita katika viwanda na miradi mbalimbali ili wajue kazi wanazozifanya ili utambue mazingira ya sasa na ya baadae iko mikononi mwao.

Amesema ili kuwe na afya bora ya jamii, wanapaswa waone umuhimu wa kutunza takataka hususani zile hatarishi bila kuzitupa hovyo ili zikateketezwe katika sehemu maalumu zilizotengwa

Mkurugenzi wa Jielimishe Kwanza, Henry Kazula amesema asilimia 15 ya taka zilizopo ni hatarishi na asilimia 85 ni takataka zisizohatarishi ambazo zinadhibitiwa na halmashauri.

Amesema kuwa taka hizo zinamadhara kiafya na husababisha ueneaji wa magonjwa kwa sababu zinahitaji kudhibitiwa kwa umakini hivyo ni vema jamii kuzitambua.

‘’Taka hatarishi ni pamoja na baadhi ya vifaa vinavyotumika katika saluni za kike na za kiume ikiwemo sindano, rasta, pampas na pedi hizi zote ni taka hatarishi na kwenye jamii utazikuta kwenye mazingira yetu hivyo ni muhimu kuzijua na kuzidhibiti kwa sababu hazitakiwi kuchanganywa na taka za nyumbani kwa kuwa zitatupwa kiholela ,’’ amesema Kazula.

Pia amesema taka hizo hazitakiwi kuchomwa moto kwani zinatoa gesi za aina mbalimbali ambazo husababisha kuharibu tabaka la juu la dunia na moshi wake husababisha athari kama vile saratani na mfumo wa upumuaji.

Naye, Ofisa Masoko wa TMHS, Ester Ngazi amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika jamii kwamba watu hawawezi kutofautisha takataka hatarishi na za kawaida hivyo, imewataka kuweka utaratibu wa kukusanya takataka hatarishi ikiwemo dawa na kuzipeleka katika hospitali za karibu ili viweze kuteketezwa kwa utaratibu unaofaa.

Amesema wanatoa huduma mbalimbali kama vile ukusanyaji na uharibifu wa takahatarishi kutoka viwandani, hopitali na miradi ya mafuta.

Amesema kuwa wateja wanaowahudumia kwenye ukusanyaji na uharibifu wa taka hatarishi ni viwanda, hospitali, maduka ya dawa na taasisi zozote ambazo zinatengeneza takataka zisizotupwa eneo la jamii.

Ameeleza kuwa gharama ya kazi hiyo inategemea na kiasi cha takataka alichonacho mteja wao kwa mfano wenye maduka ya dawa wanadawa zilizopita muda wake hivyo watapima.

‘’Mteja atatupitisha katika eneo lake tutaangalia ni mzigo kiasi gani na namna gani tutateketeza takataka hizo. Lakini pia tunatoa huduma za gari na ndege za kubeba wagonjwa kutoka nyumbani kwenda hospitalini, kutoka hospitali moja kwenda nyingine na kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi,’’ amesema
Mkuu wa Idara ya uteketezaji wa taka hatarishi wa Kampuni hiyo ya TMHS, Charles Luvubhu akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano mkuu wa Afya wa 2022 mara baada ya kumaliza mkutano mdogo wa kujadili namna ya kuteketeza Taka hatari katika jamii. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Oktoba 13, 2022.
Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano mkuu wa Afya wa 2022 mara baada ya kumaliza mkutano mdogo wa kujadili namna ya kuteketeza Taka hatari katika jamii. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Oktoba 13, 2022.

Wadau wa Uteketezaji taka hatarishi wakiwa katika Picha ya pamoja mara baada  kumaliza mkutano mdogo wa kujadili namna ya kuteketeza Taka hatari katika jamii. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Oktoba 13, 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad