HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 21, 2022

NCC WATAKIWA KUANDAA MIONGOZO BORA YA UJENZI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe.Atupele Mwakibete ameitaka Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na miongozo bora itakayosimamia na kuleta maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

Akizindua Bodi mpya ya NCC jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mwakibete amesema maendeleo endelevu katika sekta ya ujenzi nchini yatapatikana endapo uwepo wa Sheria, Miongozo ya Majenzi, na Viwango Msawazo vya majengo na nyumba za Serikali vitakuwepo na kuzingatiwa na wadau wote wa sekta ya majenzi.

“Naagiza zoezi hili lifanyike haraka, lakini kwa umakini na weledi kwa kuwashirikisha wadau wote ili kuleta tija inayotarajiwa,” amesema Mwakibete.

Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuandaa miongozo ya gharama za ujenzi wa miradi ya barabara ili miongozo na sheria zote zitumike katika mwaka wa fedha ujao wa 2023/2024.

“Ninavyozungumza hivi sasa hatuna Sheria ya Majenzi, hatuna Miongozo ya Majenzi, hatuna Kanuni za Majenzi. Hivyo mtaona kwamba mnayo mambo mengi ambayo mnatakiwa kuyafanyia kazi kwa haraka ili kubadili mtazamo wa wadau na Serikali juu ya Baraza la Taifa la Ujenzi,” alisisitiza Mwakibete.

Hata hivyo ameitaka NCC kufanya kazi kwa bidii ili kuleta ubunifu na tija katika sekta ya majenzi kwa ujumla.

" Sekta ya ujenzi katika nchi yoyote ni sekta muhimu kwa jinsi inavyochangia maendeleo ya uchumi wa nchi na kwa Tanzania sekta hii inachangia wastani wa asilimia 14 za pato la Taifa kwa mwaka,"amebainisha Naibu Waziri huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo ya NCC Dakta, Fatma Mohamed amesema Bodi hiyo itafanya kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya kwa kuwa wajumbe wa Bodi hiyo ni wataalam waliobobea katika Sekta ya Ujenzi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atuple Mwakibete (katikati), akimkabidhi makabrasha ya vitendea kazi Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dkt. Fatma Mohamed (kushoto), mara baada ya kuzindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dkt. Fatma Mohamed (kushoto), akionesha makabrasha ya vitendea kazi alivokabidhiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atuple Mwakibete (kulia), wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atuple Mwakibete (kulia), akiteteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Ludovick Nduhiye (katikati), mara baada ya kuzindua Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atuple Mwakibete, akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi na viongozi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), mara ya baada ya kuzindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad