HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 19, 2022

KIKUNDI CHA SAUTI YA JAMII CHAZINDUA OFISI KIPUNGUNI, WAASWA KUELIMISHA WANANCHI

Muonekano wa Jengo la ofisi ya kikundi cha kijamii kinachoitwa Sauti ya Jamii

 

Jengo la ofisi ya kikundi cha kijamii kinachoitwa Sauti ya Jamii lililozinduliwa leo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima kwaajili ya Ofisi na sehemu ya kujifunzia ufundi chelehani kwa wanajamii ya kipunguni.

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara hiyo itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sera na Sheria inazozisimamia huku akiwa mstari wa mbele kufika katika maeneo ambapo jamii ipo na kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Dkt. Gwajima, leo Oktoba 19, 2022 wakati akizungumza na wanajamii ya Kipunguni jimbo la Ukonga, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, wakati akizindua jengo la ofisi ya kikundi cha kijamii kinachoitwa Sauti ya Jamii.

Amesema taarifa zinaonesha kuna kushamiri kwa matukio ya ukatili, watu wanauana kwenye jamii, watoto na wanawake wanakatiliwa kwenye jamii, wanaume pia wanasema wanakatiliwa huku takwimu za mwaka 2021 zikionesha watoto 11499 walikatiliwa ambapo kati yao 5899 walibakwa. Asilimia 60 wamebakwa majumbani kwao na asilimia 40 mtaani na mashuleni.

Amesema vitendo vingi vya ukatili vinatokea kwenye jamii kwa asilimia kubwa ikiwa ni nyumbani hivyo Jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa nyumbani kunakuwa sehemu nzuri na salama kwa watoto kuishi.

Amesema kuwa hatutaki kuletewa namba na kuzikariri, bila kuona kinachoendelea kwenye mitaa mbalimbali ya jamii, kama kuna changamoto zisikilizwe , zijadiliwe na kielezwe kinachotakiwa kufanywa.

Halikadhalika amezitaka kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zilizopo ngazi za kata, mitaa na vijiji kuiga mfano wa ubunifu wa kikundi cha Sauti ya Jamii kwa kuwa na shughuli zinazowaimarisha kiuchumi hivyo kutatua changamoto ya umaskini ambao ni chanzo kimojawapo cha vitendo vya ukatili.

Amesisitiza kuelimisha wananchi kuzifikia na kuzitumia fursa mbalimbali zinazopatikana nchini ili kujikwamua kiuchumi akibainisha mifuko na programu 85 zilizoainishwa kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi chini ya uongozi wa Bi. Beng'i Issa, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hili.

Awali akieleza kuhusu kikundi hicho mmoja wa wajumbe wa kikundi hicho Juma Rashid amesema waliamua wao wenyewe kuanzisha kikundi kwa lengo la kujiinua kiuchumi kupitia fedha zao wenyewe na hatimaye kujenga ofisi hiyo kwa gharama ya zaidi ya mil 11, yenye chumba cha mafunzo ya cherehani na ujasiriamali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuwawezesha wananchi hasa kwa kata ya Kupunguni ambapo jumla ya mikopo ya Halmashauri iliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2021/22 ni zaidi ya sh. Milioni 500.

"Kwenye Kata yetu hadi sasa tuna zaidi ya vikundi 50 na bado maombi ni mengi, tunashukuru pia kwa mfumo mpya wa kielekroniki utarahisisha kupata kwa wakati na kuondoa urasimu" amesema Mushi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wizalubi Ludigija amesema jitihada za Waziri Mhe. Gwajima za kuingia ndani ya jamii zimesaidia kufanya wanajamii kuifahamu Wizara na majukumu yake tofauti na hapo awali.

Amesisiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kutokomeza vitendo vya ukatili kwa maendeleo na ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa Kipunguni, Jimbo la Ukonga wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2022.
Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi akizungumza na wananci wa Kipunguni leo Waziri Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea kuzindua jengo la Ofisi ya Jamii Kipunguni.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na viongozi mbalimbali wakizindua jengo la Ofisi Sauti ya Jamii Kipunguni jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija akizungmza na wananchi wa Kipunguni mara baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Sauti ya jamii leo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akipokea zawadi ya Mboga mboga kutoka kwa Bi Esta ambaye alikuwa mmojawapo wa mangariba wa eneo hilo. Kwa Sasa Bi. Ester ameacha Ungariba baada ya kuwezeshwa kiuchumi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akitoa cheti kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwa kutambua mchango wake katika kuanzisha kikundi ca Sauti ya jamii.



Baadhi ya wanankikundi cha Sauti ya jamii pamoja na wananchi wakiwa katika Uzinduzi wa Ofisi waliyoijenga katika Kata ya Kipunguni Ilala jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad