HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 30, 2022

BENKI YA CRDB YAZINDUA PROGRAMU YA UWEZESHAJI KWA VIJANA NA WANAWAKE WAJASIRIAMALI KIUCHUMI (IMBEJU)

 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi milioni 50 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ikiwa ni uwezeshaji kwa biashara bora changa za TEHEMA (digital startups)  kupitia programu ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake ya benki hiyo inayofahamika kama "IMBEJU" ambayo imezinduliwa katika Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar Ijumaa iliyopita. Wengine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib, Iddrisa Kitwana (watatu kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (wapili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdull (wakwanza kushoto),Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, Prof. Leornad Mselle (wapili kulia), na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga. Picha zote na Othman Michuzi.

=======  =======  =======

Ikiendeleza jitihada zake za kukuza ujumuishi wa kiuchumi nchini, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA imezindua programu mpya ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake wajasiriamali, Sh. bilioni 5 zatengwa.
 
Programu hiyo iliyopewa jina la ‘IMBEJU’ imezinduliwa katika kilele cha Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Golden Tulip na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akielezea kuhusu programu hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kupitia ‘IMBEJU’, benki hiyo itakuwa ikitoa mitaji wezeshi kwa vijana na wawawake wajasiriamali wenye biashara na mawazo bunifu.
 
Nsekela alisema kupitia programu hiyo vijana watakuwa wakiwasilisha mpango wa biashara zao, na mawazo bunifu kwa upande wa wanafunzi, kisha wataalamu wabobezi watakuwa wakichambua na kuidhinisha mtaji na mafunzo kulingana na vigezo.
 
“Katika programu ya IMBEJU tutakuwa pia tukitoa mafunzo ya usimamizi wa biashara, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, elimu ya fedha na masoko, na usaidizi wa kuboresha bidhaa na mawazo bunifu,” alisema Nsekela.
Aliongezea kuwa Benki hiyo pia imeanzisha kituo maalum cha mafunzo na ubunifu wa biashara katika Makao Makuu ya zamani ya Benki hiyo mtaa wa Azikiwe jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitasimamiwa kwa ushirikiano na Tume ya TEHAMA nchini.
 
“Katika programu za vijana wajasiriamali tumeweka mkazo mkubwa zaidi katika biashara zinazoanza katika sekta ya TEHAMA tukilenga zaidi kuchochea uchumi wa kidijitali. Biashara katika sekta nyengine pia zitakuwa zikipata uwezeshaji,” alifafanua. 
Kwa upande wa uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali, Nsekela alisema Benki hiyo itakuwa ikifanya kazi na taasisi na mashirika yaliyojikita katika kufanya uwezeshaji kwa wanawake. Uwezeshaji utafanyika kwa vikundi na wajasiriamali mmoja mmoja.
 
Kwa kuanzia katika uzinduzi huo wa programu ya IMBEJU Benki ya CRDB imekabidhi jumla ya shilingi milioni 50 kwa Tume ya TEHAMA ikiwa ni uwezeshaji kwa biashara change katika sekta ya TEHAMA (digital startups).
Akizindua programu hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha programu hiyo ya ‘IMBEJU’ akisema itasaidia kukuza ujumuishi wa kiuchumi kwa vijana na wanawake.
 
“Idadi kubwa ya watu hapa nchini ni vijana na wanawake. Licha ya hivyo ndio watu tegemezi zaidi kiuchumi. Serikali imekuwa ikiweka jitihada kubwa katika kuliwezesha kundi hili. Niipongeze Benki ya CRDB kwa kuunga mkono,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema wamejipanga vilivyo kuhakikisha programu ya ‘IMBEJU’ inakwenda kuchochea kwa kasi ukuaji wa biashara changa nchini.
 
IMBEJU inaenda sambamba na kauli mbiu ya “Leave No One Behind” ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SGD) 2030 inayosisitiza uwezeshaji kwa makundi yaliyotengwa na kukabiliana na ukosefu wa usawa katika fursa za kiuchumi.
 
 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza wakati akifunga Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar Ijumaa iliyopita.
 Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Iddrisa Kitwana akizungumza wakati katika Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar Ijumaa iliyopita.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad