HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 17, 2022

SERIKALI KUANGALIA UPYA TOZO ZA STEMPU YA KIELEKTRONIKI


 Eva Ngowi

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inataka kuangalia upya tozo za stempu za kielektroniki (ETS) ambazo kwa miaka mitatu iliyopita sekta ya viwanda imekuwa ikilalamika kuwa tozo hizi zimekuwa kubwa, hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru alipokuwa katika ziara ya kutembelea viwanda vya kutengeneza bia vyaTanzania Breweries Ltd na Serengeti Breweries Ltd jijini Dar es Salaam.

“Kuna haja ya Serikali kusikiliza hoja hii haiwezekani kwamba kuna kitu ambacho wenzetu wanakiona na sisi hatukioni. Kwa mrejesho ambao tumeupata na sisi tumejionea mfumo unavyofanya kazi, lakini pia tumepata fursa ya kuona mfumo mwingine ambao unafanya kazi sambamba na mfumo unaolalamikiwa, sasa huo mwingine unatumia ‘block chain technology’ ni almost bure na sasa tunajiuliza nini ambacho hatukioni; ambacho wenzetu wanakiona,”Alisema Bw. Mafuru

Bw. Mafuru alisema kuwa atawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waeleze kwa kina ni nini hasa ambacho wamekibaini kwenye huo mfumo.

“Wawekezaji hawa ambao wako tayari na hawapingi mfumo wa stempu za kielektroniki wanausapport kabisa ila wanachokisema una gharama na kwa hakika ukiangalia gharama zinazozungumzwa kama zingekuwa hazilipwi maana yake ni kwamba zingekuwa sehemu ya mapato ya Serikali.” Alisema Bw. Mafuru

Bw. Mafuru alisema nia hasa ya kufanya ziara hii ni kutimiza wajibu wa Wizara ya Fedha katika eneo la kusimamia uchumi kwani maendeleo ya nchi pamoja na uchumi wa Tanzania unategemea sana ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na utoaji wa ajira.

“Ziara hii imelenga kutuwezesha sisi kuelewa kwanza changamoto ambazo wenzetu kwenye sekta hii hasa sekta ya utengenezaji wa vinywaji, changamoto gani wanazopitia Pamoja na kupata mrejesho kutoka kwao kuhusu sera za hivi karibuni za kibajeti ambazo tumezipitisha kupitia bajeti ya Serikali, Sheria ya fedha lakini pia utekelezaji wa ile blue print, ambayo Serikali imekuwa ikiendelea kutekeleza. Hivyo tunafanya jitihada ya kupata mrejesho na hatimae tuweze kujua wapi ambapo tunahitaji kuongeza jitihada, wapi tunafanya vizuri na wapi hatufanyi vizuri ili tuweze kurekebisha kwa kujua kwamba tutakapoendelea kurekebisha maeneo hayo basi tutaendelea kuifungua nchi yetu kiuchumi” Alisema Bw. Mafuru

Aidha Bw. Mafuru alisema jambo muhimu sana ambalo ameliona ni kwamba; kuna haja Serikali kufanya kazi kwa Pamoja kwani kila mtu akifanya kazi kwenye eneo lake peke yake atairudisha nyuma na kuiuchelewesha Serikali.

Alisema kuwa Kuna hoja ambazo viwanda hivyo vimeziibua ambazo zinahitaji Taasisi na Wizara zingine za kisekta ziweze kuingilia na kufanya maamuzi kwani kuna maamuzi yako tangu mwaka 2016 ambayo yangetakiwa kufanyika ili kwa wanaohitaji kuwekeza waweze kuwekeza. Hivyo amesema wamechukua hili angalizo na watakaa na TRA ili kujua nini hasa hoja yao.

Bw. Mafuru aliongeza kuwa ili kuongeza uwekezaji nchini inapaswa kuwawekea mazingira rafiki ya kuwa na uhakika kama mitaji yao iliyopo hapa Tanzania italindwa ili waweze kuleta mitaji mingine.

“Makampuni yote mawili tuliyoyatembelea leo yana mipango ya kuongeza uwekezaji wao nchini lakini kuna kitu kinang’ang’ania kwenye mawazo yao ya kutokuwa na uhakika kama mambo yale ambayo yana miaka mitatu, minne hayajashughulikiwa ni kitu gani kinawapa guarantee waje kuongeza mitaji yao, kwa hiyo kuna hoja hapa ambayo na sisi tumepata mrejesho ambao tutakwenda kushare na wenzetu Serikalini na Mamlaka zinazohusika kwa lengo la kuratibu na jitihada za Serikali ili tuweze kuyashughulikia haya mambo ambayo ni kikwazo katika ukuzaji wa hizi sekta”. Alisema Bw. Mafuru

Bw. Mafuru alisema kuhusu fursa za uwekezaji, kuna changamoto ya upungufu kwenye soko la chupa za kujaza bia na uzalishaji huo umekuwa kwa muda mrefu unategemea kiwanda kimoja tu hapa nchini. Kwa kuwa wametuambia wengine wako chini ya kiwango chao cha uzalishaji na kwa sababu tu ya ukosefu wa chupa, hii inatuambia kisera inabidi kufanyike jitihada za kuwezesha sekta hiyo ya uzalishaji wa chupa ili kuweza kuongeza uzalishaji huu.

“Kwa hivyo ni sekta ambayo iko coordinated tukijua kwamba sasa kuna changamoto ya chupa na tutaongea na Wenzetu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji waweze kuangalia namna gani wana fast truck wawekezaji ambao wanaweza kuwekeza katika ilo eneo kwa sababu kuna fursa na bahati nzuri fursa hii sio tu kwa Tanzania chupa zetu zinauzwa hadi nchi Jirani kwa hiyo itatusaidia kupata fedha za kigeni kwa hivyo ukiona ni bia lakini inapanua na mambo mengine ambayo ndio uchumi wenyewe. Alisema Bw. Mafuru

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka alisema wana matumaini kwamba mazungumzo yaliyofanyika leo na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango yataleta tija kwa nchi na wako tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa lengo la kutanua wigo wa kukusanya kodi. Pia aliongezea kwenye suala la stempu za kielektroniki alisema kuwa ni mfumo mzuri ambao ulianzishwa na TRA lakini bei ni kubwa japo wanaamini kuwa Serikali inalifanyika kazi.

Naye Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John Wanyancha alisema wamerafijika sana kwa ujio wa viongozi kutoka Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango kusikilia malalamiko yao na kuona jinsi ambavyo wanafanya kazi. Wanaamini kwamba hii ziara ya Serikali kuja kuwasilikiliza wawekezaji ni njia nzuri sana ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya viwanda hapa Tanzania.

Katika suala la huduma za kijamii Serengeti Breweries Company Ltd. wameweza kuzalishaji ajira za moja kwa moja katika kiwanda chao, pia jukumu la usafirishaji linafanywa na kampuni binafsi ya Watanzania ambao wanapata kipato chao kutokana na sekta hii ya uzalishaji bia. Pia wanatoa ufadhili kwa wataalamu wa kilimo kwa sababu wana utaratibu wa kununua ngano ambayo wanaitumia kutengeneza bia. Hivyo wataalamu ambao waliwasomesha ndio wanaosaidia kutoa elimu ya kuboresha mazingira ya uzalishaji kwenye mashamba yao.

Sekta hizi za vinywaji ndio hasa zimekuwa kinara katika uchangiaji kwenye eneo la kodi ni vyema Serikali ifanye jitihada za kutatua changamoto zao ili waendelee kuchangia kwa sehemu kubwa na waendelee kukua na kuongeza ajira, kuleta maendeleo ya kiuchumi ambayo ndiyo matarajio ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad